Luka
17 Ndipo akawaambia wanafunzi wake: “Haiepukiki kwamba ni lazima sababu za kukwazika zije. Hata hivyo, ole wake ambaye hizo zaja kupitia yeye! 2 Lingekuwa jambo lenye faida zaidi kwake kama jiwe la kusagia lingening’inizwa shingoni mwake naye atupwe ndani ya bahari kuliko yeye kukwaza mmoja wa wadogo hawa. 3 Kazieni uangalifu kwa nyinyi wenyewe. Ndugu yako akifanya dhambi mpe kemeo, na akitubu msamehe. 4 Hata ikiwa akutenda dhambi mara saba kwa siku naye arudi kwako mara saba, akisema, ‘Natubu,’ lazima umsamehe.”
5 Sasa mitume wakamwambia Bwana: “Tupe sisi imani zaidi.” 6 Ndipo Bwana akasema: “Kama mngekuwa na imani yenye ukubwa wa punje ya haradali, mngeambia mforsadi mweusi huu, ‘Ng’olewa upandwe katika bahari!’ nao ungewatii nyinyi.
7 “Ni nani kati yenu aliye na mtumwa anayelima kwa plau au anayetunza kundi ambaye atamwambia aingiapo kutoka kwenye shamba, ‘Njoo hapa mara moja uegame mezani’? 8 Badala ya hivyo, je, yeye hatamwambia, ‘Nitayarishie kitu fulani ili mimi nipate mlo wangu wa jioni, nawe vaa aproni unihudumie mpaka niwe nimemaliza kula na kunywa, na baadaye wewe waweza kula na kunywa’? 9 Yeye hatahisi shukrani kwa huyo mtumwa kwa sababu aliyafanya mambo aliyoagizwa, je, atahisi? 10 Ndivyo na nyinyi, pia, wakati mmefanya mambo yote mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi ni watumwa wasiofaa kitu. Lile ambalo tumefanya ndilo tulilopaswa kufanya.’”
11 Naye alipokuwa akienda Yerusalemu alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. 12 Naye alipokuwa akiingia katika kijiji fulani wanaume kumi wenye ukoma walikutana naye, lakini wakasimama mbali. 13 Nao wakainua sauti zao na kusema: “Yesu, Mfunzi, uwe na rehema juu yetu!” 14 Naye alipopata kuwaona aliwaambia: “Nendeni mkajionyeshe wenyewe kwa makuhani.” Basi walipokuwa wakienda zao kutakaswa kwao kukatokea. 15 Mmoja wao, alipoona ameponywa, alirudi, akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa. 16 Naye akaanguka kifudifudi kwenye miguu ya Yesu, akimshukuru; zaidi ya hilo, yeye alikuwa ni Msamaria. 17 Kwa kujibu Yesu akasema: “Wale kumi walisafishwa, sivyo? Basi, wako wapi wale wengine tisa? 18 Je, hawakupatikana wowote waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mtu huyu wa taifa jingine?” 19 Naye akamwambia: “Inuka ushike njia yako uende; imani yako imekufanya upone.”
20 Lakini alipoulizwa na Mafarisayo ni wakati gani ufalme wa Mungu ulikuwa unakuja, aliwajibu na kusema: “Ufalme wa Mungu hauji kwa wonyesho wenye kutokeza sana, 21 wala watu hawatakuwa wakisema, ‘Ona hapa!’ au, ‘Pale!’ Kwa maana, tazameni! ufalme wa Mungu uko katikati yenu.”
22 Ndipo akawaambia wanafunzi: “Siku zitakuja wakati nyinyi mtakapotamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa binadamu lakini hamtaiona. 23 Na watu watawaambia nyinyi, ‘Oneni pale!’ au, ‘Oneni hapa!’ Msitoke kwenda wala msiwafuatie mbio. 24 Kwa maana kama vile umeme, kwa kumweka, hung’aa kutoka sehemu moja chini ya mbingu hadi sehemu nyingine chini ya mbingu, ndivyo Mwana wa binadamu atakavyokuwa. 25 Hata hivyo, kwanza lazima yeye apatwe na mateso mengi na kukataliwa na kizazi hiki. 26 Zaidi ya hayo, sawa na vile ilivyotukia katika siku za Noa, ndivyo itakavyokuwa pia katika siku za Mwana wa binadamu; 27 walikuwa wakila, walikuwa wakinywa, wanaume walikuwa wakioa, wanawake walikuwa wakiozwa, hadi siku ile ambayo Noa aliingia katika safina, na furiko likawasili na kuwaangamiza wote. 28 Hivyohivyo, sawa na vile ilivyotukia katika siku za Loti: walikuwa wakila, walikuwa wakinywa, walikuwa wakinunua, walikuwa wakiuza, walikuwa wakipanda, walikuwa wakijenga. 29 Lakini siku ambayo Loti alitoka Sodoma ilikunya moto na sulfa kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote. 30 Itakuwa hivyohivyo siku ile ambayo Mwana wa binadamu atapaswa kufunuliwa.
31 “Siku hiyo mwacheni mtu aliye juu ya paa ya nyumba lakini ambaye vitu vyake vyenye kuchukulika vimo katika nyumba asiteremke kuvichukua, na mtu aliye nje katika shamba, mwacheni yeye hivyohivyo asirudi kwenye vitu vilivyo nyuma. 32 Mkumbukeni mke wa Loti. 33 Yeyote yule atafutaye kuitunza salama nafsi yake kwa ajili yake mwenyewe ataipoteza, lakini yeyote yule aipotezaye ataihifadhi hai. 34 Mimi nawaambia nyinyi, Usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atachukuliwa, lakini yule mwingine ataachwa. 35 Kutakuwa na wanawake wawili wakisaga kwenye kinu kilekile; mmoja atachukuliwa, lakini yule mwingine ataachwa.” 36 —— 37 Kwa hiyo kwa kujibu wakamwambia: “Wapi, Bwana?” Yeye akawaambia: “Ulipo mwili, hapo pia tai watakusanyika pamoja.”