Luka
16 Ndipo akaendelea kuwaambia wanafunzi pia: “Mtu fulani alikuwa tajiri naye alikuwa na msimamizi-nyumba, na huyu alishtakiwa kwake kuwa atumia bidhaa zake kwa kuzipoteza bure. 2 Kwa hiyo akamwita na kumwambia, ‘Ni nini hili nisikialo juu yako? Toa hesabu ya usimamizi-nyumba wako, kwa maana huwezi tena kuisimamia nyumba.’ 3 Ndipo huyo msimamizi-nyumba akajiambia mwenyewe, ‘Nitafanya nini, kwa kuwa bwana-mkubwa wangu atauondolea mbali nami usimamizi-nyumba? Sina nguvu za kutosha kulima, naaibika kuombaomba. 4 Ah! Najua nitakalofanya, ili, wakati niondolewapo kwenye usimamizi-nyumba, watu watanipokea nyumbani mwao.’ 5 Naye akiita kwake kila mmoja wa wale wadeni wa bwana-mkubwa wake akaendelea kumwambia wa kwanza, ‘Ni kadiri gani ambayo wewe unawiwa na bwana-mkubwa wangu?’ 6 Akasema, ‘Vipimo mia vya bathi vya mafuta ya mzeituni.’ Akamwambia, ‘Chukua tena hati yako ya mapatano na uketi uandike upesi hamsini.’ 7 Halafu, akaambia mwingine, ‘Sasa wewe, ni kadiri gani ambayo unawiwa?’ Akasema, ‘Vipimo mia vya kori vya ngano.’ Akamwambia, ‘Chukua tena hati yako ya mapatano uandike themanini.’ 8 Na bwana-mkubwa wake akasifu yule msimamizi-nyumba, kwa sababu alitenda kwa hekima itumikayo, ingawa si mwadilifu; kwa maana wana wa mfumo huu wa mambo ni wenye hekima zaidi kwa njia itumikayo kuelekea kizazi chao wenyewe kuliko vile walivyo wana wa nuru.
9 “Pia, mimi nawaambia nyinyi, Jifanyieni wenyewe marafiki kupitia mali zisizo za uadilifu, ili, wakati zipungukapo wapate kuwapokea nyinyi ndani ya mahali pa kukaa padumupo milele. 10 Mtu aliye mwaminifu katika lililo dogo zaidi sana ni mwaminifu katika lililo kubwa pia, na mtu asiye mwaminifu katika lililo dogo zaidi sana ni asiye mwaminifu katika lililo kubwa pia. 11 Kwa hiyo, ikiwa nyinyi hamjajithibitisha wenyewe kuwa waaminifu kuhusiana na mali zisizo za uadilifu, ni nani atakayewakabidhi nyinyi kilicho cha kweli? 12 Na ikiwa nyinyi hamjajithibitisha wenyewe kuwa waaminifu kuhusiana na kilicho cha mwingine, ni nani atakayewapa nyinyi kilicho chenu wenyewe? 13 Hakuna mtumishi wa nyumbani awezaye kutumikia kama mtumwa wa mabwana-wakubwa wawili; kwa maana, ama atachukia mmoja na kupenda mwingine, au atashikamana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kuwa watumwa wa Mungu na wa mali.”
14 Sasa Mafarisayo, waliokuwa wapenda-fedha, walikuwa wakisikiliza mambo yote haya, nao wakaanza kumcheka kwa dharau. 15 Kwa sababu hiyo yeye akawaambia: “Nyinyi ni wale mjitangazao wenyewe kuwa waadilifu mbele ya macho ya wanadamu, lakini Mungu aijua mioyo yenu; kwa sababu kilichoinuka sana miongoni mwa wanadamu ni kitu chenye kuchukiza sana machoni pa Mungu.
16 “Sheria na Manabii walikuwa mpaka Yohana. Tangu wakati huo na kuendelea ufalme wa Mungu unatangazwa kuwa habari njema, na kila namna ya mtu anakaza mwendo mbele kuuelekea. 17 Kwa kweli, ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupitilia mbali kuliko nukta moja ya herufi ya Sheria kupita bila kutimizwa.
18 “Kila mtu atalikiye mke wake na kuoa mwingine afanya uzinzi, naye aoaye mwanamke aliyetalikiwa kutoka kwa mume afanya uzinzi.
19 “Lakini mtu fulani alikuwa tajiri, naye alikuwa na kawaida ya kujipamba kwa mavazi ya zambarau na kitani, akijifurahisha mwenyewe siku hadi siku kwa fahari. 20 Lakini mwombaji fulani aitwaye jina Lazaro alikuwa na kawaida ya kuwekwa kwenye lango lake, mwenye kujaa vidonda 21 na akitamani kushibishwa kwa vile vitu vyenye kuanguka kutoka kwenye meza ya yule mtu tajiri. Ndiyo, pia, mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake. 22 Sasa baadaye yule mwombaji alikufa naye akachukuliwa na malaika hadi kwenye mahali pa kifua cha Abrahamu.
“Pia, yule mtu tajiri akafa na kuzikwa. 23 Na katika Hadesi aliinua macho yake, akiwako katika kuteswa-teswa kwingi, naye akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro akiwa katika mahali pa kifua pamoja naye. 24 Kwa hiyo akaita na kusema, ‘Baba Abrahamu, uwe na rehema juu yangu umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake katika maji apoze ulimi wangu, kwa sababu nimo katika maumivu makali katika moto huu wenye kuwaka vikali.’ 25 Lakini Abrahamu akasema, ‘Mtoto, kumbuka kwamba wewe ulipokea kwa ukamili vitu vyako vyema katika muda wa maisha yako, lakini Lazaro kwa ulinganifu alipokea mambo mabaya. Hata hivyo, sasa yeye anapata faraja hapa lakini wewe umo katika maumivu makali. 26 Na mbali na mambo yote haya, ufa mkubwa umewekwa kati yetu na nyinyi watu, hivi kwamba wale wanaotaka kuvuka kutoka hapa kwenda kwenu nyinyi watu hawawezi, wala watu hawawezi kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’ 27 Ndipo yeye akasema, ‘Ikiwa ni hivyo mimi nakuomba, baba, umtume kwenye nyumba ya baba yangu, 28 kwa maana nina ndugu watano, ili yeye apate kuwapa ushahidi kamili, ili wao pia wasiingie katika mahali hapa pa kuteswa-teswa.’ 29 Lakini Abrahamu akasema, ‘Wana Musa na Manabii; na wawasikilize hawa.’ 30 Ndipo yeye akasema, ‘La, hasha, baba Abrahamu, lakini mtu fulani kutoka kwa wafu akiwaendea watatubu.’ 31 Lakini yeye akamwambia, ‘Ikiwa hawasikilizi Musa na Manabii, wala hawatashawishwa ikiwa mtu fulani afufuliwa kutoka kwa wafu.’”