Luka
15 Sasa wakusanya-kodi wote na watenda-dhambi wakafuliza kumkaribia ili wamsikie. 2 Kwa sababu hiyo Mafarisayo na pia waandishi wakafuliza kunung’unika, wakisema: “Mtu huyu hukaribisha watenda-dhambi na hula pamoja nao.” 3 Ndipo akawaambia kielezi hiki, akisema: 4 “Ni mtu gani kati yenu mwenye kondoo mia, apotezapo mmoja wao, hataacha nyuma wale tisini na tisa nyikani na kwenda kumtafuta aliyepotea mpaka ampate? 5 Na akiisha kumpata humweka juu ya mabega yake na kushangilia. 6 Naye afikapo nyumbani huita marafiki wake na majirani wake pamoja, akiwaambia, ‘Shangilieni pamoja nami, kwa sababu nimempata kondoo wangu aliyekuwa amepotea.’ 7 Mimi nawaambia nyinyi kwamba ndivyo kutakuwa na shangwe zaidi mbinguni juu ya mtenda-dhambi mmoja atubuye kuliko juu ya waadilifu tisini na tisa wasio na uhitaji wa toba.
8 “Au ni mwanamke gani mwenye sarafu za drakma kumi, ikiwa apoteza sarafu moja ya drakma, asiyewasha taa na kufagia nyumba yake na kutafuta kwa uangalifu mpaka aipate? 9 Naye akiisha kuipata huwaita wanawake walio marafiki wake na majirani pamoja, akisema, ‘Shangilieni pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu ya drakma niliyoipoteza.’ 10 Hivyo, mimi nawaambia nyinyi, ndivyo shangwe hutokea miongoni mwa malaika za Mungu juu ya mtenda-dhambi mmoja atubuye.”
11 Ndipo yeye akasema: “Mtu fulani alikuwa na wana wawili. 12 Na yule kijana zaidi kati yao akamwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali iliyo fungu langu.’ Ndipo yeye akawagawia njia zake za kujipatia riziki. 13 Baadaye, baada ya siku zisizokuwa nyingi, huyo mwana aliye kijana zaidi alikusanya pamoja vitu vyote akasafiri nchi ya nje akaingia katika nchi ya mbali, na huko akafuja mali yake kwa kuishi maisha ya ufasiki. 14 Alipokuwa ametumia kila kitu, njaa kali sana ilitokea kotekote katika nchi hiyo, naye akaanza kuwa katika uhitaji. 15 Hata alienda na kujiambatanisha mwenyewe kwa mmoja wa raia wa nchi hiyo, naye akamtuma aingie katika mashamba yake ili achunge mifugo ya nguruwe. 16 Naye alikuwa na kawaida ya kutamani kushibishwa kwa matumba ya mkarobu ambayo hao nguruwe walikuwa wakila, na hakuna yeyote aliyekuwa akimpa kitu chochote.
17 “Aliporudiwa na fahamu zake, alisema, ‘Ni wanaume wangapi walioajiriwa wa baba yangu ambao wanazidi katika kuwa na mkate, na huku mimi ninaangamia hapa kutokana na njaa kali! 18 Hakika mimi nitainuka nifunge safari niende kwa baba yangu na kumwambia: “Baba nimefanya dhambi dhidi ya mbingu na dhidi yako wewe. 19 Sistahili tena kuitwa mwana wako. Unifanye kama mmoja wa watu wako walioajiriwa.”’ 20 Kwa hiyo akainuka akamwendea baba yake. Alipokuwa angali mbali sana, baba yake alimwona mara hiyo naye akasukumwa na sikitiko, naye akakimbia akaangukia shingo yake na kumbusu kwa wororo. 21 Ndipo yule mwana akamwambia, ‘Baba, nimefanya dhambi dhidi ya mbingu na dhidi yako. Sistahili tena kuitwa mwana wako. Unifanye niwe kama mmoja wa wanaume wako walioajiriwa.’ 22 Lakini yule baba akawaambia watumwa wake, ‘Upesi! leteni nje kanzu, iliyo bora zaidi, mmvike hiyo, na mtie pete mkononi mwake na makubazi miguuni mwake. 23 Nanyi leteni fahali mchanga aliyenoneshwa, mchinjeni na acheni tule na kujifurahisha wenyewe, 24 kwa sababu huyu mwana wangu alikuwa amekufa naye akaja tena kwenye uhai; alikuwa amepotea naye akapatikana.’ Nao wakaanza kujifurahisha wenyewe.
25 “Sasa mwana wake mwenye umri mkubwa zaidi alikuwa katika shamba; naye alipokuja akaikaribia nyumba alisikia utumbuizo wa kimuziki na uchezaji-dansi. 26 Kwa hiyo akaita mmoja wa watumishi kwake akaulizia habari mambo hayo yalimaanisha nini. 27 Yeye akamwambia, ‘Ndugu yako amekuja, na baba yako amechinja fahali mchanga aliyenoneshwa, kwa sababu alimpata tena akiwa na afya njema.’ 28 Lakini yeye akawa na hasira ya kisasi na hakutaka kuingia. Ndipo baba yake akatoka akaanza kumsihi sana. 29 Kwa kujibu akamwambia baba yake, ‘Hii ni miaka mingi sana ambayo mimi nimekutumikia wewe kama mtumwa na kamwe hata mara moja sijakiuka amri yako, na bado kamwe hata mara moja hukunipa mwana-mbuzi ili mimi nijifurahishe mwenyewe pamoja na marafiki wangu. 30 Lakini mara tu alipowasili huyu mwana wako aliyekula kabisa pamoja na makahaba njia zako za kujipatia riziki, ulimchinjia fahali mchanga aliyenoneshwa.’ 31 Ndipo akamwambia, ‘Mtoto, wewe umekuwa pamoja nami sikuzote, na vitu vyote vilivyo vyangu ni vyako; 32 lakini ilitupasa tu kujifurahisha wenyewe na kushangilia, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa naye akaja kwenye uhai, naye alikuwa amepotea naye akapatikana.’”