2 Wakorintho
11 Laiti nyinyi mngechukuliana nami katika kukosa kidogo akili. Lakini, kwa kweli, mnachukuliana nami! 2 Kwa maana nina wivu juu yenu nikiwa na wivu wa kimungu, kwa maana mimi binafsi niliwaposea nyinyi mume mmoja ili nipate kuwatoa nyinyi mkiwa bikira safi kiadili kwa Kristo. 3 Lakini naogopa kwamba kwa njia fulani, kama nyoka alivyomshawishi Hawa kwa ujanja wake, huenda akili zenu zikafisidiwa kutoka kwenye weupe wa moyo na usafi wa kiadili ambao wamstahili Kristo. 4 Kwa maana, kama ilivyo, mtu fulani akija na kuhubiri Yesu mwingine tofauti na yule tuliyehubiri, au mkipokea roho nyingine tofauti na ile mliyopokea, au habari njema nyingine tofauti na ile mliyokubali, mwachukuliana naye kwa urahisi. 5 Kwa maana nafikiria kwamba sijathibitika hata katika jambo moja kuwa hafifu kwa mitume wenu walio bora sana. 6 Lakini hata ikiwa sina ustadi katika usemi, hakika sivyo nilivyo katika ujuzi; lakini katika kila njia tulidhihirisha hilo kwenu katika mambo yote.
7 Au je, nilifanya dhambi kwa kujinyenyekeza mwenyewe ili nyinyi mpate kukwezwa, kwa sababu bila gharama nilitangaza kwenu kwa mteremo habari njema ya Mungu? 8 Makutaniko mengine niliyapokonya kwa kupokea maposho kusudi niwahudumie nyinyi; 9 na bado nilipokuwa pamoja nanyi nami nikapatwa na uhitaji, sikuwa mzigo wenye kulemea kwa mtu hata mmoja, kwa maana ndugu waliokuja kutoka Makedonia walijazia kwa wingi upungufu wangu. Ndiyo, katika kila njia nilijitunza mwenyewe bila kuwa mzigo wenye kuwalemea nyinyi na hakika mimi nitajitunza mwenyewe hivyo. 10 Ni kweli ya Kristo katika kisa changu kwamba hakika hakuna kikomo chochote kitakachowekwa kwenye kujisifu kwangu huku katika mikoa ya Akaya. 11 Kwa sababu gani? Kwa sababu siwapendi nyinyi? Mungu ajua nawapenda.
12 Basi lile ninalofanya bado hakika mimi nitalifanya, ili nipate kukatilia mbali kisingizio kutoka kwa wale wanaotaka kisingizio cha kupatikana kuwa sawa nasi katika cheo ambacho wao wajisifia. 13 Kwa maana watu wa namna hiyo ni mitume wasio wa kweli, wafanyakazi wenye udanganyifu, wakijigeuza umbo wenyewe kuwa mitume wa Kristo. 14 Na si ajabu, kwa maana Shetani mwenyewe hufuliza kujigeuza umbo mwenyewe kuwa malaika wa nuru. 15 Kwa hiyo si jambo kubwa ikiwa wahudumu wake pia wafuliza kujigeuza umbo wenyewe kuwa wahudumu wa uadilifu. Lakini mwisho wao utakuwa kulingana na kazi zao.
16 Nasema tena, Acheni mtu yeyote asifikiri mimi nakosa akili. Bado, ikiwa kwa kweli mwafikiri hivyo, nikubalini mimi hata ikiwa ni kama nakosa akili, ili mimi vilevile nipate kujisifu kwa kiasi fulani kidogo. 17 Lile nisemalo nasema, si kwa kufuatisha kielelezo cha Bwana, bali kama katika ukosefu wa akili, katika uhakika huu wa kupita kiasi ulio kawaida ya kujisifu. 18 Kwa kuwa wengi wanajisifu kulingana na mwili, hakika mimi vilevile nitajisifu. 19 Kwa maana nyinyi mwachukuliana kwa mteremo na watu wenye kukosa akili, kwa kuwa nyinyi ni wenye akili. 20 Kwa kweli, nyinyi mwachukuliana na yeyote yule awafanyaye watumwa, yeyote yule anyafuaye kile mlicho nacho, yeyote yule anyakuaye kile mlicho nacho, yeyote yule ajikwezaye mwenyewe juu yenu, yeyote yule awapigaye usoni.
21 Nasema hili kwa kutuvunjia heshima, kama kwamba cheo chetu kilikuwa dhaifu.
Lakini ikiwa mwingine yeyote atenda kwa ujasiri katika jambo fulani—mimi ninaongea kwa kukosa akili —mimi vilevile ninatenda kwa ujasiri katika hilo. 22 Je, wao ni Waebrania? Mimi pia. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia. Je, wao ni mbegu ya Abrahamu? Mimi pia. 23 Je, wao ni wahudumu wa Kristo? Mimi najibu kama mtu mwenye kichaa, kwa kutokeza zaidi ndivyo nilivyo: katika kazi za jasho kwa utele zaidi, katika magereza kwa utele zaidi, katika mapigo kwa kuzidi mno, katika mikaribio ya kifo mara nyingi. 24 Kwa Wayahudi nilipokea mara tano mapigo arobaini kasoro moja, 25 mara tatu nilipigwa kwa fito, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nilipata kuvunjikiwa na meli, usiku mmoja na mchana mmoja nimetumia katika kilindi; 26 katika safari mara nyingi, katika hatari za kutokana na mito, katika hatari za kutokana na wanyang’anyi wa njia kuu, katika hatari za kutokana na jamii yangu mwenyewe, katika hatari za kutokana na mataifa, katika hatari za jijini, katika hatari za nyikani, katika hatari za baharini, katika hatari za miongoni mwa ndugu wasio wa kweli, 27 katika kazi ya jasho na kumenyeka, katika masiku bila usingizi mara nyingi, katika njaa na kiu, katika kuepukana na chakula nyakati nyingi, katika baridi na uchi.
28 Mbali na mambo yale ya aina ya nje, kuna kinachonisonga ndani sana siku kwa siku, kuhangaikia makutaniko yote. 29 Ni nani aliye dhaifu, nami si dhaifu? Ni nani amekwazika, nami siwaki hasira?
30 Ikiwa ni lazima kuwe kujisifu, nitajisifu juu ya mambo yenye kuhusiana na udhaifu wangu. 31 Mungu na Baba ya Bwana Yesu, naam, Yule aliye wa kusifiwa milele, ajua sisemi uwongo. 32 Katika Damasko gavana aliye chini ya Aretasi mfalme alikuwa akilinda jiji la Wadamasko ili kunikamata, 33 lakini kupitia dirisha katika ukuta nikateremshwa katika kapu la vifito vilivyosukwa nikaponyoka katika mikono yake.