2 Wakorintho
10 Basi mimi mwenyewe, Paulo, nawasihi sana nyinyi kwa upole na fadhili ya Kristo, ingawa mimi ni wa hali ya chini katika kuonekana miongoni mwenu, lakini nisipokuwapo mimi ni jasiri kuwaelekea nyinyi. 2 Kwa kweli naomba kwamba, niwapo, nisipate kutumia ujasiri kwa uhakika huo ambao kwa huo nategemea kuchukua hatua za kijasiri dhidi ya wengine ambao watukadiria sisi kama kwamba tulitembea kulingana na tulivyo katika mwili. 3 Kwa maana ingawa twajiendesha katika mwili, hatufanyi shughuli ya vita kulingana na tulivyo katika mwili. 4 Kwa maana silaha za shughuli yetu ya vita si za kimwili, bali zenye nguvu kupitia Mungu kwa ajili ya kupindua mambo yaliyotiwa kwa nguvu sana katika mahandaki. 5 Kwa maana sisi tunapindua mawazowazo na kila jambo lililoinuka sana lililoinuliwa dhidi ya ujuzi wa Mungu; nasi tunaingiza kila fikira katika utekwa ili kuifanya iwe tiifu kwa Kristo; 6 nasi tunajichukua wenyewe katika utayari ili kuadhibu kila kutokutii, mara tu utii wenu wenyewe ukiisha kuwa umetekelezwa kikamili.
7 Nyinyi mwatazama mambo kulingana na thamani yayo ya uso. Ikiwa yeyote ajiitibari mwenyewe kwamba ni wa Kristo, acheni yeye azingatie tena jambo hili kwa ajili yake mwenyewe, kwamba, kama vile yeye alivyo wa Kristo, ndivyo na sisi pia. 8 Kwa maana hata nikijisifu mno kidogo juu ya mamlaka ambayo Bwana alitupa ili kuwajenga nyinyi na si kuwabomoa nyinyi, mimi singeaibishwa, 9 ili nisipate kuonekana kama nataka kuwaogofya nyinyi kwa barua zangu. 10 Kwa maana, wasema wao: “Barua zake ni zenye uzito na zenye kani nyingi, lakini kuwapo kwake mwenyewe binafsi ni dhaifu na usemi wake wa kudharaulika.” 11 Acheni mtu wa namna hiyo azingatie hili, kwamba kile tulicho katika neno letu kwa barua wakati hatupo, tutakuwa hicho pia katika tendo wakati tuwapo. 12 Kwa maana hatuthubutu kujiainisha wenyewe miongoni mwa wengine au kujilinganisha wenyewe na wengine ambao hujipendekeza wenyewe. Hakika wao katika kujipima wenyewe kwa wenyewe na kujilinganisha wenyewe na wao wenyewe hawana uelewevu.
13 Kwa upande wetu sisi tutajisifu, si nje ya mipaka yetu tuliyogawiwa, bali kulingana na mpaka wa eneo ambalo Mungu alitugawia kwa kipimo, akilifanya lifike hadi kwenu. 14 Kwa kweli sisi hatujitanui wenyewe kupita kiasi kama kwamba hatukuwafikia nyinyi, kwa maana tulikuwa wa kwanza kuja hadi kwenu katika kutangaza habari njema juu ya Kristo. 15 La, hatujisifu katika kazi za jasho za mtu mwingine nje ya mipaka yetu tuliyogawiwa, bali twashika tumaini kwamba, kadiri imani yenu inavyoongezwa, sisi tupate kufanywa wakubwa miongoni mwenu kuhusiana na eneo letu. Ndipo tutakapozidi hata zaidi, 16 kutangaza habari njema kwenye nchi za ng’ambo yenu, ili kusiwe kujisifu katika eneo la mtu mwingine ambako mambo yamekwisha kutayarishwa. 17 “Bali yeye ajisifuye, acheni ajisifu katika Yehova.” 18 Kwa maana si yule ajipendekezaye mwenyewe hukubaliwa, bali mtu ambaye Yehova hupendekeza.