2 Wakorintho
9 Basi kuhusu huduma iliyo kwa ajili ya watakatifu, hakuna uhitaji wa mimi kuwaandikia nyinyi, 2 kwa maana najua utayari wenu wa akili ambao juu ya huo najisifu kwa Wamakedonia juu yenu, kwamba Akaya imesimama tayari kwa mwaka mmoja sasa, na bidii yenu imechochea walio wengi kati yao. 3 Lakini ninawatuma akina ndugu, ili kujisifu kwetu juu yenu kusipate kuthibitika kuwa bure katika habari hii, bali ili mpate kuwa tayari kwa kweli, kama vile nilivyokuwa na kawaida ya kusema mngekuwa. 4 Kama sivyo, kwa njia fulani, Wamakedonia wakija pamoja nami na kuwakuta mkiwa hamko tayari, sisi—bila kusema nyinyi—tusije kuaibishwa katika uhakikisho wetu huu. 5 Kwa hiyo nilifikiri ni lazima niwatie moyo akina ndugu wawajie nyinyi kimbele na kutayarisha kimbele zawadi yenu yenye kujaa tele iliyoahidiwa hapo awali, ili kwamba ipate kuwa tayari kama zawadi yenye kujaa tele na si kama kitu cha kunyang’anywa.
6 Lakini kuhusu hili, yeye apandaye kwa uhaba atavuna pia kwa uhaba; na yeye apandaye kwa wingi atavuna pia kwa wingi. 7 Acheni kila mmoja afanye kama vile ameazimia moyoni mwake, si kwa kinyongo au kwa shurutisho, kwa maana Mungu hupenda mpaji mchangamfu.
8 Zaidi ya hayo, Mungu aweza kufanya fadhili yake yote isiyostahiliwa izidi kuwaelekea nyinyi, ili, ijapokuwa sikuzote mna ujitoshelevu kamili katika kila kitu, mpate kuwa na utele kwa ajili ya kila kazi njema. 9 (Kama vile imeandikwa: “Yeye amegawa kotekote, amewapa walio maskini, uadilifu wake waendelea milele.” 10 Basi yeye amgawiaye mpanzi-mbegu kwa wingi na mkate wa kula atagawa na kuwazidishia nyinyi mbegu ili mpande na ataongeza mazao ya uadilifu wenu.) 11 Katika kila kitu mnatajirishwa mwe na kila namna ya ukarimu, ambao hutokeza kupitia sisi wonyesho wa shukrani kwa Mungu; 12 kwa sababu huduma ya utumishi huu wa watu wote si tu kugawa kwa wingi mahitaji ya watakatifu bali pia kuwa tajiri kwa maonyesho mengi ya shukrani kwa Mungu. 13 Kupitia ithibati ambayo huduma hii hutoa, wao wamtukuza Mungu kwa sababu nyinyi ni wenye kunyenyekea habari njema juu ya Kristo, mtangazapo hadharani kuwa mko hivyo, na kwa sababu nyinyi ni wakarimu katika mchango wenu kwao na kwa wote; 14 nao wakiwa na dua kwa ajili yenu wana hamu sana kuwaona nyinyi kwa sababu ya fadhili isiyostahiliwa ya Mungu izidiyo juu yenu.
15 Shukrani ziwe kwa Mungu kwa ajili ya zawadi yake ya bure isiyoelezeka.