2 Wakorintho
8 Basi akina ndugu, twaacha nyinyi mjue juu ya fadhili isiyostahiliwa ya Mungu ambayo yamepewa makutaniko ya Makedonia, 2 kwamba wakati wa jaribu kubwa chini ya taabu kubwa, wingi wao wa shangwe na umaskini wa kina kirefu ulifanya utajiri wa ukarimu wao kuzidi. 3 Kwa maana hilo lilikuwa kulingana na uwezo wao halisi, ndiyo, mimi nashuhudia, kupita uwezo wao halisi, 4 huku wakifuliza kwa hiari yao wenyewe kutuomba kwa kusihi sana wapate pendeleo la kutoa kwa fadhili na kuwa na ushiriki katika huduma waliyokusudiwa watakatifu. 5 Na si kama tulivyokuwa tumetumaini tu, bali kwanza walijitoa wenyewe kwa Bwana na kwetu kupitia mapenzi ya Mungu. 6 Hili lilituongoza tumtie moyo Tito kwamba, kama vile alivyokuwa amekuwa ndiye mwenye kuanzisha hilo miongoni mwenu, ndivyo pia apaswavyo kukamilisha utoaji huuhuu wenye fadhili kwa upande wenu. 7 Hata hivyo, kama vile mnavyozidi katika kila jambo, katika imani na neno na ujuzi na hali yote ya bidii na katika upendo huu wetu kwa nyinyi, mpate pia kuzidi katika upaji huu wenye fadhili.
8 Sisemi kwa njia ya kuwaamuru nyinyi, bali ni kwa kufikiria hali ya bidii ya wengine na ili kuufanyia jaribu uhalisi wa upendo wenu. 9 Kwa maana nyinyi mwaijua fadhili isiyostahiliwa ya Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba ingawa alikuwa tajiri alipata kuwa maskini kwa ajili yenu, ili mpate kuwa matajiri kupitia umaskini wake.
10 Na katika hili mimi natoa kauli: kwa maana jambo hili ni lenye manufaa kwenu, kwa kuwa tayari mwaka mmoja uliopita nyinyi mlianzisha si kule kufanya tu bali pia kule kutaka kufanya; 11 basi, sasa malizeni pia kule kufanya hilo, ili, kama vile kulivyokuwa na utayari wa kutaka kufanya, ndivyo pia kuwe kumaliza hilo kutokana na kile mlicho nacho. 12 Kwa maana ikiwa utayari upo kwanza, hukubalika hasa kulingana na alicho nacho mtu, si kulingana na kile ambacho mtu hana. 13 Kwa maana sikusudii iwe rahisi kwa wengine, lakini vigumu kwenu; 14 bali kwamba kupitia usawazisho wa ziada yenu sasa hivi ipate kujazia upungufu wao, ili ziada yao ipate pia kujazia upungufu wenu, ili usawazisho upate kutukia. 15 Kama vile imeandikwa: “Mtu aliye na vingi hakuwa na vingi mno, na mtu aliye na vichache hakuwa na vichache mno.”
16 Basi shukrani zimwendee Mungu kwa kuweka hali ileile ya bidii kwa ajili yenu katika moyo wa Tito, 17 kwa sababu kwa kweli yeye ameitikia hicho kitia-moyo, lakini, akiwa mwenye bidii sana, anaenda kwa hiari yake mwenyewe kuja kwenu. 18 Lakini tunatuma pamoja naye ndugu ambaye sifa yake kwa uhusiano na habari njema imesambaa kupitia makutaniko yote. 19 Si hilo tu, bali pia aliwekwa rasmi na makutaniko kuwa mwandamani wetu mwenye kusafiri kuhusiana na zawadi hii ya fadhili itakayohudumiwa na sisi kwa utukufu wa Bwana na kwa ithibati ya akili yetu iliyo tayari. 20 Hivyo tunaepuka mtu yeyote asipate kosa kwetu kuhusiana na mchango huu wa ukarimu utakaohudumiwa nasi. 21 Kwa maana “twafanya uandalizi wa haki, si mbele ya macho ya Yehova tu, bali machoni pa wanadamu pia.”
22 Zaidi ya hayo, tunatuma pamoja nao ndugu yetu ambaye tumemthibitisha mara nyingi katika mambo mengi kuwa mwenye bidii, lakini sasa mwenye bidii nyingi zaidi kwa sababu ya uhakika wake mkubwa katika nyinyi. 23 Ingawa hivyo, kama kuna swali lolote juu ya Tito, yeye ni mshiriki pamoja nami na mfanyakazi mwenzi kwa ajili ya masilahi yenu; au kama ni juu ya ndugu zetu, wao ni mitume wa makutaniko na utukufu wa Kristo. 24 Kwa hiyo waonyesheni ithibati ya upendo wenu na ya yale tuliyojisifu juu yenu, mbele ya uso wa makutaniko.