2 Wakorintho
7 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna ahadi hizi, wapendwa, acheni tujisafishe wenyewe kila unajisi wa mwili na wa roho, tukikamilisha utakatifu katika hofu ya Mungu.
2 Ruhusuni nafasi kwa ajili yetu. Sisi hatujakosea yeyote, hatujafisidi yeyote, hatujatumia yeyote kwa kujifaidi. 3 Sisemi hili kuwalaumu nyinyi. Kwa maana nimesema hapo mbele kwamba nyinyi mumo katika mioyo yetu ili kufa na kuishi pamoja nasi. 4 Mimi nina uhuru mkubwa wa usemi kuwaelekea nyinyi. Nina kujisifu kukubwa kwa habari yenu. Nimejawa na faraja, ninafurika kwa shangwe katika taabu yetu yote iliyo kubwa.
5 Kwa kweli, tulipowasili katika Makedonia, mwili wetu haukupata kitulizo, bali tuliendelea kutaabishwa sana katika kila namna—kulikuwa na mapigano kwa nje, hofu kwa ndani. 6 Hata hivyo Mungu, ambaye hufariji wale walioshushwa chini, alitufariji kwa kuwapo kwa Tito; 7 lakini si kwa kuwapo kwake peke yake, bali pia kwa faraja ambayo kwayo alikuwa amefarijiwa juu yenu, kwa kuwa alituletea habari tena juu ya kuwa kwenu na hamu sana, kuomboleza kwenu, bidii yenu kwa ajili yangu; hivi kwamba nikashangilia tena zaidi.
8 Kwa sababu hiyo hata ikiwa niliwahuzunisha nyinyi kwa barua yangu, mimi sijutii hilo. Hata ikiwa hapo kwanza nilijutia hilo, (naona kwamba barua hiyo iliwahuzunisha nyinyi, ingawa kwa muda kidogo,) 9 sasa mimi nashangilia, si kwa sababu mlihuzunishwa tu, bali kwa sababu mlihuzunishwa kufikia kutubu; kwa maana mlihuzunishwa katika njia ya kimungu, ili msipatwe na hasara katika jambo lolote kwa sababu yetu. 10 Kwa maana huzuni katika njia ya kimungu hutokeza toba hadi kwenye wokovu ambao si wa kujutiwa; lakini huzuni ya ulimwengu hutokeza kifo. 11 Kwa maana, tazameni! jambo hilihili, kuwa kwenu wenye kuhuzunishwa katika njia ya kimungu, kulitokeza katika nyinyi hali ya bidii kubwa kama nini, ndiyo, kujiondolea wenyewe hatia, ndiyo, ghadhabu, ndiyo, hofu, ndiyo, kuwa na hamu sana, ndiyo, bidii, ndiyo, kusahihisha lililo kosa! Katika kila jambo mlijionyesha wenyewe kuwa safi kiadili katika jambo hili. 12 Hakika, ijapokuwa niliwaandikia nyinyi, nilifanya hilo, si kwa ajili ya yeye aliyetenda kosa, wala kwa ajili ya yeye aliyekosewa, bali ili hali yenu ya bidii kwa ajili yetu ipate kufanywa dhahiri miongoni mwenu machoni pa Mungu. 13 Hiyo ndiyo sababu sisi tumefarijiwa.
Hata hivyo, kwa kuongezea faraja yetu bado sisi tulishangilia kwa wingi zaidi kwa sababu ya shangwe ya Tito, kwa sababu roho yake imeburudishwa na nyinyi nyote. 14 Kwa maana ikiwa nimefanya kujisifu kokote kwake juu yenu, sijaaibishwa; lakini kama vile tumewaambia mambo yote katika kweli, ndivyo pia kujisifu kwetu mbele ya Tito kumethibitika kuwa kweli. 15 Pia, shauku zake nyororo ni nyingi zaidi kuwaelekea nyinyi, akumbukapo utii wenu nyote, jinsi mlivyompokea kwa hofu na kutetemeka. 16 Nashangilia kwamba katika kila njia nipate kuwa na moyo mkuu kwa sababu yenu.