2 Wakorintho
12 Yanibidi kujisifu. Si jambo lenye manufaa; lakini nitapita hadi kwenye maono yazidio nguvu za asili na mafunuo ya Bwana. 2 Najua mtu mmoja katika muungano na Kristo ambaye, miaka kumi na minne iliyopita—kama ni katika mwili sijui, au nje ya mwili sijui; Mungu ajua—alinyakuliwa akiwa wa namna hiyo hadi kwenye mbingu ya tatu. 3 Ndiyo, najua mtu wa namna hiyo—kama ni katika mwili au bila mwili, sijui, Mungu ajua— 4 kwamba alinyakuliwa kuingia katika paradiso na kusikia maneno yasiyotamkika ambayo hairuhusiki kisheria mtu kuyasema. 5 Juu ya mtu wa namna hiyo hakika mimi nitajisifu, lakini hakika mimi sitajisifu juu yangu mwenyewe, ila kwa habari ya udhaifu wangu. 6 Kwa maana ikiwa wakati wowote ningetaka kujisifu, singekuwa mwenye kukosa akili, kwa maana nitasema kweli. Lakini naepuka, ili yeyote asinihesabie sifa zaidi ya kile anionacho mimi kuwa au asikiacho kutoka kwangu, 7 kwa sababu tu ya kuzidi mno kwa hayo mafunuo.
Kwa hiyo, ili nisipate kuhisi kukwezwa mno, nilipewa mwiba katika mwili, malaika wa Shetani, afulize kunipiga kofi, ili nisipate kukwezwa kupita kiasi. 8 Kwa ajili ya hilo mara tatu nilimsihi sana Bwana kwamba upate kuniondoka; 9 na bado kwa kweli akaniambia: “Fadhili yangu isiyostahiliwa yakutosha wewe; kwa maana nguvu yangu inafanywa kamilifu katika udhaifu.” Kwa hiyo, kwa mteremo zaidi sana afadhali nijisifu kwa habari ya udhaifu wangu, ili nguvu ya Kristo ipate kubaki juu yangu kama hema. 10 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, katika matusi, katika visa vya uhitaji, katika minyanyaso na magumu, kwa ajili ya Kristo. Kwa maana niwapo dhaifu, ndipo niwapo mwenye nguvu.
11 Nimekuwa mwenye kukosa akili. Nyinyi mlinishurutisha kuwa hivyo, kwa maana nilipaswa kuwa nimependekezwa nanyi. Kwa maana sikuthibitika kuwa hafifu kwa mitume wenu walio bora sana katika hata jambo moja, hata ikiwa mimi si kitu. 12 Kwa kweli, ishara za mtume zilitokezwa miongoni mwenu kwa uvumilivu wote, na kwa ishara na mambo ya ajabu na kazi zenye nguvu. 13 Kwa maana ni katika jambo gani kwamba nyinyi mlipata kuwa punde kuliko makutaniko mengine, ila kwamba mimi mwenyewe sikupata kuwa mzigo wenye kuwalemea? Mnisamehe kosa hili kwa fadhili.
14 Tazameni! Hii ndiyo mara ya tatu niliyo tayari kuja kwenu, na bado sitakuwa mzigo wenye kulemea. Kwa maana ninatafuta sana, si mali zenu, bali nyinyi; kwa maana watoto hawapaswi kuweka akiba kwa ajili ya wazazi wao, bali wazazi kwa ajili ya watoto wao. 15 Kwa upande wangu hakika mimi nitatumia kwa mteremo zaidi sana na kutumiwa kabisa kwa ajili ya nafsi zenu. Kama nikiwapenda nyinyi kwa wingi zaidi, je, mimi nipendwe kidogo? 16 Lakini hata kama ikiwa hivyo, mimi sikuwalemea. Hata hivyo, nyinyi mwasema, mimi nilikuwa “mjanja” na niliwashika nyinyi “kwa hadaa.” 17 Kwa habari ya yeyote kati ya wale niliotuma kwenu, sikuwatumia nyinyi kwa kujifaidi kupitia yeye, sivyo? 18 Nilimhimiza Tito na nikamtuma ndugu aliyekuwa pamoja naye. Tito hakuwatumia nyinyi kwa kujifaidi hata kidogo, sivyo? Tulitembea katika roho ileile, sivyo? Katika hatua zilezile, sivyo?
19 Je, nyinyi mmekuwa mkifikiri muda huu wote kwamba sisi tumekuwa tukijitetea kwenu? Ni mbele ya Mungu kwamba tunasema kuhusiana na Kristo. Lakini, wapendwa, mambo yote ni kwa ajili ya kuwajenga nyinyi. 20 Kwa maana naogopa kwamba kwa njia fulani, niwasilipo, huenda nikawapata nyinyi si kama vile ambavyo mimi ningeweza kutaka na huenda nikathibitika kwenu kuwa si kama ambavyo nyinyi mngeweza kutaka, bali, badala ya hivyo, kwa njia fulani yaelekea kutakuwa na zogo, wivu, visa vya hasira, magomvi, masengenyo, manong’onezo, visa vya kuwa wenye kututumuka, mivurugo. 21 Labda, nijapo tena, huenda Mungu wangu akanitweza miongoni mwenu, na huenda nikaomboleza juu ya wengi kati ya wale ambao hapo zamani walitenda dhambi lakini hawajatubia ukosefu wao wa usafi na uasherati na mwenendo mlegevu ambao wamezoea kufanya.