2 Wakorintho
13 Hii ndiyo mara ya tatu ambayo ninakuja kwenu. “Kwa kinywa cha mashahidi wawili au cha watatu lazima kila jambo lithibitishwe.” 2 Nimesema hapo awali na, kama kwamba nipo mara ya pili lakini sipo sasa, nawaambia kimbele wale ambao wametenda dhambi hapo awali na kwa wale wengine wote, kwamba wakati wowote nikija tena hakika sitahurumia, 3 kwa kuwa mnatafuta ithibati ya Kristo akisema katika mimi, Kristo ambaye si dhaifu kuwaelekea nyinyi bali ni mwenye nguvu miongoni mwenu. 4 Ni kweli kabisa, yeye alitundikwa mtini kwa sababu ya udhaifu, lakini yuko hai kwa sababu ya nguvu ya Mungu. Ni kweli, pia, sisi ni dhaifu pamoja naye, lakini tutaishi pamoja naye kwa sababu ya nguvu ya Mungu kuwaelekea nyinyi.
5 Fulizeni kujijaribu kama nyinyi mumo katika imani, fulizeni kujithibitisha wenyewe nyinyi ni nini. Au je, hamtambui kwamba Yesu Kristo yumo katika muungano pamoja nanyi? Isipokuwa mwe mmekataliwa. 6 Kwa kweli natumaini nyinyi mtakuja kujua sisi hatukataliwi.
7 Basi twasali kwa Mungu kwamba nyinyi msipate kufanya jambo lolote lililo kosa, si kwamba sisi wenyewe tupate kuonekana kuwa waliokubaliwa, bali kwamba mpate kuwa mkifanya lililo bora, ingawa sisi wenyewe huenda tukaonekana kuwa waliokataliwa. 8 Kwa maana hatuwezi kufanya jambo lolote dhidi ya kweli, bali kwa ajili tu ya kweli. 9 Hakika sisi twashangilia wakati wowote ule tuwapo dhaifu lakini nyinyi ni wenye nguvu; na kwa ajili ya hili tunasali, kurekebishwa upya kwenu. 10 Hiyo ndiyo sababu naandika mambo haya nikiwa sipo, ili, niwapo, nisipate kutenda kwa ukali kulingana na mamlaka ambayo Bwana alinipa, ili kujenga na si kubomoa.
11 Mwishowe, akina ndugu, endeleeni kushangilia, kurekebishwa upya, kufarijiwa, kufikiri katika upatano, kuishi kwa kufanya amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi. 12 Salimianeni kwa busu takatifu. 13 Watakatifu wote wawapelekea nyinyi salamu zao.
14 Fadhili isiyostahiliwa ya Bwana Yesu Kristo na upendo wa Mungu na ushirika katika roho takatifu uwe pamoja nanyi nyote.