2 Wakorintho
3 Je, tunaanza tena kujipendekeza wenyewe? Au je, sisi, labda, kama watu fulani, twahitaji barua za pendekezo kuja kwenu au kutoka kwenu? 2 Nyinyi wenyewe ndio barua yetu, iliyoandikwa juu ya mioyo yetu na ijulikanayo na kusomwa na wanadamu wote. 3 Kwa maana nyinyi mwaonyeshwa kuwa barua ya Kristo iliyoandikwa na sisi tukiwa wahudumu, iliyoandikwa si kwa wino bali kwa roho ya Mungu aliye hai, si juu ya mabamba ya mawe, bali juu ya mabamba ya nyama, juu ya mioyo.
4 Basi kupitia Kristo tuna uhakika wa namna hii kuelekea Mungu. 5 Si kwamba sisi wenyewe tuna sifa za ustahili wa kutosha kuhesabu jambo lolote kuwa latoka kwetu wenyewe, bali kuwa kwetu na sifa za ustahili wa kutosha kwatoka kwa Mungu, 6 ambaye kwa kweli ametustahilisha vya kutosha kuwa wahudumu wa agano jipya, si wa mfumo wa sheria iliyoandikwa, bali wa roho; kwa maana mfumo wa sheria iliyoandikwa huleta adhabu ya kifo, bali roho hufanya kuwa hai.
7 Zaidi ya hayo, ikiwa mfumo wa sheria uhudumiao kifo na uliochongwa katika herufi kwenye mawe ulikuja kuwa katika utukufu, hivi kwamba wana wa Israeli hawangeweza kukodolea macho kwa mkazo uso wa Musa kwa sababu ya utukufu wa uso wake, utukufu uliopaswa kuondolewa mbali, 8 kwa nini kuhudumia kwa roho kusiwe kwenye utukufu zaidi sana? 9 Kwa maana ikiwa mfumo wa sheria wenye kuhudumia lawama ulikuwa wenye utukufu, kuhudumia uadilifu kwazidi zaidi sana kwa utukufu. 10 Kwa kweli, hata kile ambacho wakati mmoja kimefanywa chenye utukufu kimevuliwa utukufu katika habari hii, kwa sababu ya utukufu ukizidio ubora. 11 Kwa maana ikiwa kile kilichopaswa kuondolewa mbali kiliingizwa na utukufu, kile ambacho chabaki kingekuwa na utukufu zaidi sana.
12 Kwa hiyo, kwa kuwa tuna tumaini la namna hiyo, sisi tunatumia uhuru mkubwa wa usemi, 13 na si kufanya kama wakati Musa alipokuwa akiweka shela juu ya uso wake, ili wana wa Israeli wasikodolee macho kwa mkazo mwisho wa kile kilichopaswa kuondolewa mbali. 14 Lakini nguvu zao za akili zilitiwa uzito. Kwa maana hadi siku hii ya wakati wa sasa, shela ileile yadumu bila kuondolewa wakati wa usomaji wa agano la zamani, kwa sababu yaondolewa mbali kwa njia ya Kristo. 15 Kwa kweli, hadi leo wakati wowote ule Musa asomwapo, shela hukaa juu ya mioyo yao. 16 Lakini wakati kuna kugeuka kuelekea Yehova, shela huondolewa mbali. 17 Sasa Yehova ndiye Roho; na iliko roho ya Yehova, kuna uhuru. 18 Na sisi sote, wakati tukiwa na nyuso zisizo na shela tutoapo kama vioo mrudisho wa utukufu wa Yehova, twageuzwa umbo kuwa katika mfano uleule kutoka utukufu hadi utukufu, sawasawa kabisa na ifanywavyo na Yehova aliye Roho.