2 Wakorintho
2 Kwa maana hili ndilo nimejiamulia mwenyewe, nisiwajie nyinyi tena kwa huzuni. 2 Kwa maana nikiwafanya kuwa na huzuni, kwa kweli ni nani aliyeko wa kunichangamsha ila yeye afanywaye kuwa mwenye huzuni na mimi? 3 Na kwa hiyo niliandika jambo hilihili, ili, nijapo, nisipate kuhuzunika kwa sababu ya wale ambao juu yao napaswa kushangilia; kwa sababu nina uhakika katika nyinyi nyote kwamba shangwe niliyo nayo ni ile yenu nyote. 4 Kwa maana kwa sababu ya dhiki nyingi na maumivu makali ya moyo niliwaandikia nyinyi kwa machozi mengi, si ili mpate kuhuzunishwa, bali mpate kuujua upendo nilio nao hasa zaidi kwa ajili yenu.
5 Basi ikiwa yeyote amesababisha huzuni, amehuzunisha, si mimi, bali nyinyi nyote kwa kadiri fulani—kutokuwa mkali mno katika nisemayo. 6 Kemeo hili lenye kutolewa na walio wengi latosha kwa mtu wa namna hiyo, 7 ili kwamba, kinyume chake sasa, nyinyi mwapaswa kumsamehe kwa fadhili na kumfariji, ili kwa njia fulani mtu wa namna hiyo asipate kumezwa na huzuni yake ya kupita kiasi. 8 Kwa hiyo nawahimiza kwa bidii kumthibitishia upendo wenu. 9 Kwa maana kwa madhumuni haya pia naandika kuhakikisha ithibati yenu, kama nyinyi ni watiifu katika mambo yote. 10 Jambo lolote ambalo mwasamehe yeyote kwa fadhili, mimi vilevile namsamehe. Kwa kweli, kwa habari yangu mimi, lolote lile ambalo nimesamehe kwa fadhili, ikiwa nimesamehe kwa fadhili jambo lolote, imekuwa ni kwa ajili yenu machoni pa Kristo; 11 ili tusipate kushindwa akili na Shetani, kwa maana sisi si wasio na ujuzi kuhusu mbinu zake.
12 Basi nilipowasili Troasi kutangaza habari njema juu ya Kristo, na mlango ukafunguliwa kwangu katika Bwana, 13 sikupata kitulizo katika roho yangu kwa sababu ya kutomkuta Tito ndugu yangu, bali niliwaambia wao kwaheri nikaondoka kwenda Makedonia.
14 Lakini shukrani ziwe kwa Mungu ambaye sikuzote hutuongoza katika mwandamano wenye shangwe ya ushindi kwa ushirika na Kristo na huifanya harufu ya ujuzi juu ya yeye kufahamika kupitia sisi kila mahali! 15 Kwa maana kwa Mungu sisi ni harufu tamu ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na miongoni mwa wale wanaoangamia; 16 kwa hao wa mwisho harufu inayotoka katika kifo hadi kifo, kwa wale wa kwanza harufu inayotoka katika uhai hadi uhai. Na ni nani ambaye ana sifa za ustahili wa kutosha kwa ajili ya mambo haya? 17 Ni sisi; kwa maana sisi si wachuuzi wa neno la Mungu kama watu wengi walivyo, bali tunasema kwa weupe wa moyo, ndiyo, tukiwa waliotumwa kutoka kwa Mungu, mbele ya Mungu, kwa ushirika na Kristo.