2 Wakorintho
4 Hiyo ndiyo sababu, kwa kuwa sisi tuna huduma hii kulingana na rehema tuliyoonyeshwa, hatufi moyo; 2 bali tumeyakataa kabisa mambo ya kichinichini yaliyo ya kuaibikia, si kutembea kwa ujanja, wala tukilighushi neno la Mungu, bali kwa kufanya kweli iwe dhahiri tukijipendekeza wenyewe kwa kila dhamiri ya kibinadamu machoni pa Mungu. 3 Basi, ikiwa kwa kweli habari njema tutangazayo imetiwa shela, imetiwa shela miongoni mwa wale wanaoangamia, 4 ambao miongoni mwao mungu wa huu mfumo wa mambo amepofusha akili za wasioamini, ili mmuliko wa habari njema yenye utukufu juu ya Kristo, aliye mfano wa Mungu, usipate kung’aa kwa kupenya. 5 Kwa maana tunahubiri, si juu yetu wenyewe, bali juu ya Kristo Yesu kuwa Bwana, na sisi wenyewe kuwa watumwa wenu kwa ajili ya Yesu. 6 Kwa maana Mungu ndiye aliyesema: “Acha nuru ing’ae kutoka katika giza,” naye ameng’aa juu ya mioyo yetu ili kuimulika kwa ujuzi wenye utukufu juu ya Mungu kwa uso wa Kristo.
7 Hata hivyo, sisi tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili nguvu ipitayo iliyo ya kawaida ipate kuwa ya Mungu na si ile ya kutoka katika sisi wenyewe. 8 Twasongwa katika kila njia, lakini hatufinywi kupita tuwezavyo kusonga; twafadhaishwa, lakini si bila njia ya kutokea kabisa; 9 twateswa, lakini hatuachwi kabisa bila msaada; twaangushwa chini, lakini hatuangamizwi. 10 Sikuzote kila mahali katika mwili wetu twavumilia tendo lenye kuleta kifo alilotendewa Yesu, ili uhai wa Yesu upate pia kufanywa dhahiri katika mwili wetu. 11 Kwa maana sisi tunaoishi tunaletwa daima uso kwa uso na kifo kwa ajili ya Yesu, ili uhai wa Yesu upate kufanywa dhahiri pia katika mwili wetu uwezao kufa. 12 Kwa sababu hiyo kifo chafanya kazi katika sisi, lakini uhai katika nyinyi.
13 Basi kwa sababu tuna roho ileile ya imani kama ile ambayo juu yayo imeandikwa: “Mimi nilidhihirisha imani, kwa hiyo nikasema,” sisi pia hudhihirisha imani na kwa hiyo twasema, 14 tukijua kwamba yeye ambaye alimfufua Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu na atatutokeza sisi pamoja nanyi. 15 Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili fadhili isiyostahiliwa iliyozidishwa ipate kuzidi kwa sababu ya utoaji-shukrani wa wengi zaidi kwa utukufu wa Mungu.
16 Kwa hiyo hatufi moyo, lakini hata ikiwa mtu tuliye kwa nje anachakaa, hakika mtu tuliye kwa ndani anafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana ingawa dhiki ni ya dakika na ni nyepesi, yafanyiza kwetu utukufu ulio na uzito wenye kuzidi zaidi na zaidi na ni wa kudumu milele; 18 huku tukifuliza kuweka macho yetu, si juu ya vitu vionekanavyo, bali juu ya vitu visivyoonekana. Kwa maana vitu vionekanavyo ni vya muda, lakini vitu visivyoonekana ni vya kudumu milele.