2 Wakorintho
5 Kwa maana twajua kwamba nyumba yetu ya kidunia, hema hili, ikifumuliwa, twapaswa kuwa na jengo kutoka kwa Mungu, nyumba isiyofanyizwa kwa mikono, yenye kudumu milele katika mbingu. 2 Kwa maana katika nyumba hii ya kukaa twapiga kite kwelikweli, tukitamani kwa bidii kuvaa ile yetu kutoka mbinguni, 3 ili kwamba, tukiisha kuivaa kwa kweli, hatutapatikana tukiwa uchi. 4 Kwa kweli, sisi tulio katika hema hili twapiga kite, tukiwa tumelemewa; kwa sababu twataka, si kulivua, bali kuvaa lile jingine, ili kiwezacho kufa kipate kumezwa na uhai. 5 Basi yeye aliyetutokeza kwa ajili ya jambo hilihili ni Mungu, aliyetupa arbuni ya kitakachokuja, yaani, roho.
6 Kwa hiyo sikuzote sisi ni wenye moyo mkuu na twajua kwamba, wakati tungali tuna nyumba yetu katika mwili, hatupo alipo Bwana, 7 kwa maana tunatembea kwa imani, si kwa kuona. 8 Lakini sisi ni wenye moyo mkuu na twapendezwa vema tusiwepo katika mwili na badala ya hivyo tufanye nyumba yetu kuwa pamoja na Bwana. 9 Kwa hiyo pia tunaifanya iwe shabaha yetu kwamba, kama tunakuwa na nyumba yetu pamoja naye au tunakuwa hatupo pamoja naye, tupate kuwa wenye kukubalika kwake. 10 Kwa maana lazima sisi sote tufanywe dhahiri mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mmoja apate thawabu yake kwa mambo yaliyofanywa kuupitia mwili, kulingana na mambo ambayo amezoea, kama ni jambo jema au jambo ovu.
11 Kwa hiyo, kwa kuwa tunaijua hofu ya Bwana, twafuliza kushawishi watu, lakini sisi tumefanywa dhahiri kwa Mungu. Hata hivyo, natumaini kwamba tumefanywa dhahiri pia kwa dhamiri zenu. 12 Hatujipendekezi wenyewe tena kwenu, bali tunawapa nyinyi kichocheo cha kujisifu kwa habari yetu, ili mpate kuwa na jibu la kuwapa wale ambao hujisifu juu ya kuonekana kwa nje lakini si juu ya moyo. 13 Kwa maana ikiwa tulikuwa tumerukwa na akili yetu, ilikuwa kwa ajili ya Mungu; ikiwa tuko timamu katika akili, ni kwa ajili yenu. 14 Kwa maana upendo alio nao Kristo hutushurutisha, kwa sababu hili ndilo tumehukumu, kwamba mtu mmoja alikufa kwa ajili ya wote; kwa hiyo, basi, wote walikuwa wamekufa; 15 naye alikufa kwa ajili ya wote ili wale waishio wapate kuishi si kwa ajili yao wenyewe tena, bali kwa ajili ya yeye aliyekufa kwa ajili yao na alifufuliwa.
16 Kwa sababu hiyo tangu sasa na kuendelea sisi hatujui mtu yeyote kulingana na mwili. Hata ikiwa tumemjua Kristo kulingana na mwili, hakika sasa hatumjui hivyo tena. 17 Kwa sababu hiyo ikiwa yeyote yuko katika muungano na Kristo, yeye ni kiumbe kipya; yale mambo ya zamani yalipitilia mbali, tazameni! mambo mapya yamekuja kuwako. 18 Lakini mambo yote ni kutoka kwa Mungu, aliyetupatanisha sisi kwake mwenyewe kupitia Kristo na kutupa sisi huduma ya upatanisho, 19 yaani, kwamba Mungu kupitia Kristo alikuwa akipatanisha ulimwengu kwake mwenyewe, bila kuwahesabia makosa yao, naye alitukabidhi neno la upatanisho.
20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi walio badala ya Kristo, kama kwamba Mungu alikuwa akisihi sana kupitia sisi. Kama walio badala ya Kristo twaomba: “Iweni wenye kupatanishwa na Mungu.” 21 Yeye ambaye hakujua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa uadilifu wa Mungu kupitia yeye.