2 Wathesalonike
3 Mwishowe, akina ndugu, endelezeni sala kwa ajili yetu, ili neno la Yehova lipate kufuliza kusonga kwa kasi na kutukuzwa kama vile kwa kweli lilivyo kwenu; 2 na ili tupate kukombolewa kutokana na watu wenye madhara na waovu, kwa maana imani si miliki ya watu wote. 3 Lakini Bwana ni mwaminifu, naye atawafanya nyinyi imara na kuwaepusha na mwovu. 4 Zaidi ya hayo, tuna uhakika katika Bwana kuhusu nyinyi, kwamba mnafanya na mtaendelea kufanya mambo tuagizayo. 5 Bwana na aendelee kuelekeza kwa mafanikio mioyo yenu kuingia katika kumpenda Mungu na kuingia katika uvumilivu kwa ajili ya Kristo.
6 Sasa tunawapa nyinyi maagizo, akina ndugu, katika jina la Bwana Yesu Kristo, kujiondoa kutoka kwa kila ndugu anayetembea bila utaratibu na si kulingana na mapokeo mliyopokea kutoka kwetu. 7 Kwa maana nyinyi wenyewe mwajua njia iwapasayo kutuiga, kwa sababu hatukujiendesha bila utaratibu miongoni mwenu 8 wala hatukula chakula kwa yeyote bure. Kinyume cha hilo, kwa kazi ya jasho na kumenyeka usiku na mchana tulikuwa tukifanya kazi ili tusimtwike yeyote kati yenu mzigo ulemeao wenye gharama. 9 Si kwamba hatuna mamlaka, bali ili sisi tupate kujitoa wenyewe kuwa kielelezo kwenu ili mtuige sisi. 10 Kwa kweli, pia, tulipokuwa pamoja nanyi, tulikuwa na kawaida ya kuwapa nyinyi agizo hili: “Ikiwa yeyote hataki kufanya kazi, wala msimwache ale.” 11 Kwa maana twasikia watu fulani wanatembea bila utaratibu miongoni mwenu, wakiwa hawafanyi kazi hata kidogo bali wakijiingiza katika lile lisilowahusu wao. 12 Kwa watu wa namna hiyo twatoa agizo na kutoa himizo lenye bidii katika Bwana Yesu Kristo kwamba kwa kufanya kazi kwa utulivu wale chakula ambacho wao wenyewe wachuma.
13 Kwa upande wenu, akina ndugu, msikate tamaa katika kutenda lililo sawa. 14 Lakini ikiwa yeyote hawi mtiifu kwa neno letu kupitia barua hii, mfulize kumtia mtu huyu alama, komeni kushirikiana naye, ili apate kuaibika. 15 Na bado msiwe mkimwona yeye kuwa adui, bali endeleeni kumwonya kwa upole kama ndugu.
16 Sasa Bwana wa amani mwenyewe awape nyinyi amani daima katika kila njia. Bwana awe pamoja nanyi nyote.
17 Hii ni salamu yangu, ya Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe, ambao ni ishara katika kila barua; hii ndiyo njia ambayo mimi huandika.
18 Fadhili isiyostahiliwa ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nanyi nyote.