2 Timotheo
4 Nakuagiza kwa uzito mbele ya Mungu na Kristo Yesu, ambaye akusudiwa kuhukumu walio hai na wafu, na kwa udhihirisho wake na ufalme wake, 2 lihubiri neno, lifanye kwa hima katika majira yenye kufaa, katika majira yenye taabu, karipia, kemea, himiza kwa bidii, kwa ustahimilivu wote na usanifu wa kufundisha. 3 Kwa maana kutakuwako kipindi cha wakati ambapo hawatachukuliana na fundisho lenye afya, bali, kwa kupatana na tamaa zao wenyewe, watajirundikia walimu kwa ajili yao wenyewe ili wapate kutekenywa masikio yao; 4 nao watageuzia mbali masikio yao kuacha kweli, lakini watageuzwa kando kwenye hadithi zisizo za kweli. 5 Ingawa hivyo, wewe tunza akili zako katika mambo yote, vumilia uovu, fanya kazi ya mweneza-evanjeli, timiza kikamili huduma yako.
6 Kwa maana mimi tayari namwagwa kama toleo la kinywaji, na wakati upasao wa kuachiliwa kwangu wakaribia sana. 7 Nimepigana pigano bora, nimekimbia mwendo hadi mwisho, nimeshika imani. 8 Tangu wakati huu na kuendelea kumewekwa akiba kwa ajili yangu taji la uadilifu, ambalo Bwana, aliye hakimu mwadilifu, atanipa kuwa zawadi katika siku ile, lakini si mimi tu, bali pia wale wote ambao wamependa udhihirisho wake.
9 Fanya yote kabisa uwezayo kunijia mimi upesi. 10 Kwa maana Demasi ameniachilia mbali kwa sababu aliupenda mfumo wa mambo uliopo, naye ameenda Thesalonike; Kresensi hadi Galatia, Tito hadi Dalmatia. 11 Luka peke yake yuko pamoja nami. Umchukue Marko na kumleta pamoja nawe, kwa maana yeye ni mwenye mafaa kwangu kwa ajili ya huduma. 12 Lakini nimemtuma Tikiko aende Efeso. 13 Ujapo, lilete joho nililoachia Karpo katika Troasi, na hati-kunjo, hasa zile hati za ngozi.
14 Aleksanda mfua-shaba alinitenda mabaya mengi— Yehova atamlipa kulingana na vitendo vyake— 15 na wewe pia uwe mwenye kujilinda dhidi yake, kwa maana alikinza maneno yetu kwa kadiri izidiyo mno.
16 Katika teteo langu la kwanza hakuna yeyote aliyekuja upande wangu, bali wao wote waliniachilia mbali —hilo lisipate kuhesabiwa dhidi yao— 17 lakini Bwana alisimama karibu nami na kutia nguvu ndani yangu, ili kupitia mimi kule kuhubiri kupate kutimizwa kikamili na mataifa yote yapate kusikia; nami nilikombolewa kutoka katika kinywa cha simba. 18 Bwana atanikomboa kutoka katika kila kazi mbovu na ataniokoa kwa ajili ya ufalme wake wa kimbingu. Kwake uwe utukufu milele na milele. Ameni.
19 Uwape salamu zangu Priska na Akila na watu wa nyumbani mwa Onesiforo.
20 Erasto alikaa Korintho, lakini nilimwacha Trofimo akiwa mgonjwa Mileto. 21 Fanya yote kabisa uwezayo kuwasili kabla ya majira ya baridi kali.
Eubulo akupelekea salamu zake, na pia Pudensi na Lino na Klaudia na ndugu wote.
22 Bwana awe pamoja na roho ambayo wewe waonyesha. Fadhili yake isiyostahiliwa iwe pamoja na nyinyi watu.