Yakobo
4 Vita vyatokana na chanzo gani na mapigano miongoni mwenu yatokana na chanzo gani? Je, si kutoka katika chanzo hiki, yaani, kutokana na tamaa zenu za kufurahisha hisi za mwili ambazo huendeleza pambano katika viungo vyenu? 2 Mwatamani, na bado hamna kitu. Mwaendelea kuua kimakusudi na kutamani kwa wivu, na bado hamwezi kupata. Mwaendelea kupigana na kufanya vita. Hamna kitu kwa sababu ya kutokuomba kwenu. 3 Mwaomba, na bado hampokei, kwa sababu mnaomba kwa kusudi baya, ili mtumie hicho kwa tamaa zenu za kufurahisha hisi za mwili.
4 Wanawake wazinzi, je, hamjui kwamba urafiki na ulimwengu ni uadui na Mungu? Kwa hiyo, yeyote yule atakaye kuwa rafiki ya ulimwengu anajifanya mwenyewe kuwa adui ya Mungu. 5 Au je, yaonekana kwenu kwamba andiko lasema bila kusudi lolote: “Ni kwa mwelekeo wa kuhusudu kwamba roho ambayo imefanya makao katika sisi hufuliza kuwa na hamu sana”? 6 Hata hivyo, fadhili isiyostahiliwa ambayo yeye hutoa ni kubwa zaidi. Kwa sababu hiyo lasema: “Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu fadhili isiyostahiliwa.”
7 Basi, jitiisheni wenyewe kwa Mungu; lakini mpingeni Ibilisi, naye atawakimbia. 8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia. Safisheni mikono yenu, nyinyi watenda-dhambi, na takaseni mioyo yenu, nyinyi wenye kusitasita kuamua. 9 Jiacheni mwingiwe na taabu na ombolezeni na kutoa machozi. Acheni kicheko chenu kigeuzwe kuwa ombolezo, na shangwe yenu kuwa simanzi. 10 Jinyenyekezeni wenyewe machoni pa Yehova, naye atawakweza.
11 Komeni kusema dhidi ya mtu na mwenzake, akina ndugu. Yeye asemaye dhidi ya ndugu au ahukumuye ndugu yake husema dhidi ya sheria na huhukumu sheria. Basi ikiwa wahukumu sheria, wewe si mtekelezaji wa sheria, bali ni hakimu. 12 Mmoja yuko ambaye ni mpaji-sheria na hakimu, yeye awezaye kuokoa na kuangamiza. Lakini wewe, wewe ni nani uwe ukihukumu jirani yako?
13 Haya, basi, nyinyi msemao: “Leo au kesho hakika sisi tutafunga safari kwenda kwenye jiji hili na hakika tutamaliza mwaka huko, nasi hakika tutajitia katika biashara na kuzipata faida,” 14 kwa kuwa hamjui uhai wenu utakuwa nini kesho. Kwa maana nyinyi ni ukungu unaotokea kwa muda kidogo na kisha kutoweka. 15 Badala ya hivyo, mwapaswa kusema: “Yehova akipenda, tutaishi na pia kufanya hili au lile.” 16 Lakini sasa mwaonea fahari kujigamba kwenu kwa kujitanguliza. Kuona fahari kote kwa namna hiyo ni kuovu. 17 Kwa hiyo, ikiwa mtu ajua jinsi ya kufanya lililo sawa na bado halifanyi, hiyo ni dhambi kwake.