Yakobo
5 Haya! sasa, nyinyi watu matajiri, toeni machozi, mnaopiga kilio juu ya taabu zenu zinazokuja juu yenu. 2 Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu ya nje yamekuwa yenye kuliwa na nondo. 3 Dhahabu na fedha zimefanya kutu kabisa, na kutu yazo itakuwa kama ushahidi dhidi yenu na itakula sehemu zenu zenye nyama. Kitu fulani kama moto ndicho nyinyi mmeweka akiba katika siku za mwisho. 4 Tazameni! Mishahara iliyo haki ya wafanyakazi waliovuna mashamba yenu lakini ambayo yazuiliwa nanyi, yafuliza kupaaza kilio, na vilio vya kutaka msaada kwa upande wa wavunaji vimeingia ndani ya masikio ya Yehova wa majeshi. 5 Nyinyi mmeishi katika anasa juu ya dunia na kuchagua kujitia katika kufurahisha hisi za mwili. Mmenonesha mioyo yenu katika siku ya machinjo. 6 Mmelaumu, mmemuua kimakusudi aliye mwadilifu. Je, yeye hawapingi nyinyi?
7 Kwa hiyo, dhihirisheni subira akina ndugu, hadi kuwapo kwa Bwana. Tazameni! Mkulima hufuliza kungojea matunda yenye bei ya dunia, akidhihirisha subira juu yayo mpaka apatapo mvua ya mapema na mvua ya mwisho-mwisho. 8 Nyinyi pia dhihirisheni subira; fanyeni mioyo yenu kuwa imara, kwa sababu kuwapo kwa Bwana kumekaribia.
9 Msipigiane vite kwa uchungu, akina ndugu, ili msipate kuhukumiwa. Tazameni! Hakimu amesimama mbele ya milango. 10 Akina ndugu, watwaeni kama kiolezo cha kuvumilia uovu na kudhihirisha subira wale manabii, waliosema katika jina la Yehova. 11 Tazameni! Twawatamka kuwa wenye furaha wale ambao wamevumilia. Nyinyi mmesikia juu ya uvumilivu wa Yobu na mmeona tokeo alilotoa Yehova, kwamba Yehova ni mwenye wororo sana katika shauku na mwenye rehema.
12 Juu ya mambo yote, ingawa hivyo, ndugu zangu, komeni kuapa, ndiyo, ama kwa mbingu ama kwa dunia ama kwa kiapo kingine chochote. Bali acheni Ndiyo yenu imaanishe Ndiyo, na La yenu, La, ili msianguke hukumuni.
13 Je, kuna yeyote miongoni mwenu anayevumilia uovu? Acheni aendeleze sala. Je, kuna yeyote mwenye roho changamfu? Acheni aziimbe zaburi. 14 Je, kuna yeyote mgonjwa miongoni mwenu? Acheni awaite kwake wanaume wazee wa kutaniko, na acheni wasali juu yake, wakimpaka mafuta katika jina la Yehova. 15 Na sala ya imani itamfanya huyo asiyejisikia vizuri apone, na Yehova atamwinua. Pia, ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.
16 Kwa hiyo ungamianeni dhambi zenu waziwazi na kusali kwa ajili ya mtu na mwenzake, ili mpate kuponywa. Dua ya mtu mwadilifu, inapofanya kazi, ina kani nyingi. 17 Eliya alikuwa mtu mwenye hisia kama zetu, na bado katika sala alisali mvua isinye; na mvua haikunya juu ya nchi kwa miaka mitatu na miezi sita. 18 Naye akasali tena, na mbingu ikatoa mvua na nchi ikazaa matunda yayo.
19 Ndugu zangu, ikiwa yeyote miongoni mwenu aongozwa vibaya kutoka kwenye kweli na mwingine amrudisha, 20 jueni kwamba yeye arudishaye mtenda-dhambi kutoka kwenye kosa la njia yake ataokoa nafsi yake kutoka kwenye kifo na atafunika wingi wa dhambi.