Yakobo
3 Si wengi kati yenu wapaswao kuwa walimu, ndugu zangu, mkijua kwamba tutapokea hukumu nzito zaidi. 2 Kwa maana sisi sote hujikwaa mara nyingi. Ikiwa yeyote hajikwai katika neno, huyu ni mtu mkamilifu, awezaye kuuongoza kwa hatamu mwili wake wote pia. 3 Ikiwa sisi huziweka hatamu katika vinywa vya farasi ili watutii, sisi huuongoza mwili wao wote pia. 4 Tazameni! Hata mashua, zijapokuwa ni kubwa sana na huendeshwa na pepo kali, huongozwa na mtambo wa usukani ulio mdogo sana kwenda ambako mwelekeo wa mtu aliye kwenye usukani ataka.
5 Hivyo, pia, ulimi ni kiungo kidogo na bado husema makubwa ya kujigamba. Tazameni! Jinsi ichukuavyo moto mdogo kuwasha mwitu mkubwa! 6 Basi, ulimi ni moto. Ulimi umefanywa kuwa ulimwengu wa ukosefu wa uadilifu miongoni mwa viungo vyetu, kwa maana huutia doa mwili wote na kuliwasha miali gurudumu la uhai wa asili na huo huwashwa miali na Gehena. 7 Kwa maana kila namna ya jamii ya hayawani-mwitu na vilevile ndege na kitambaazi na kiumbe cha baharini ni ya kufugwa na imefugwa na jamii ya kibinadamu. 8 Lakini ulimi, hakuna hata mmoja kati ya wanadamu awezaye kuufuga. Ni kitu kisichotawalika chenye ubaya, umejaa sumu yenye kuleta kifo. 9 Kwa huo twabariki Yehova, naam Baba, na bado kwa huo twalaani wanadamu ambao wamekuja kuwako “katika ufanani wa Mungu.” 10 Kutoka katika kinywa kilekile huja kubariki na kulaani.
Haifai, ndugu zangu, mambo haya kuendelea kutukia kwa njia hii. 11 Bubujiko halifanyi yaliyo matamu na machungu kububujika kutoka katika kilango kilekile, je, ni hivyo? 12 Ndugu zangu, mtini hauwezi kutokeza zeituni au mzabibu kutokeza tini, je, waweza? Wala maji ya chumvi hayawezi kutokeza maji matamu.
13 Ni nani aliye mwenye hekima na mwenye kuelewa miongoni mwenu? Acheni aonyeshe kutokana na mwenendo wake bora kazi zake kwa upole ulio wa hekima. 14 Lakini ikiwa nyinyi mna wivu wenye uchungu na ugomvi katika mioyo yenu, msiwe mkijigamba na kusema uwongo dhidi ya kweli. 15 Hii siyo hekima iteremkayo kutoka juu, bali ni ya kidunia, ya kinyama, ya roho waovu. 16 Kwa maana ambako kuna wivu na ugomvi, hapo ukosefu wa utaratibu na kila jambo ovu vipo.
17 Lakini hekima ya kutoka juu kwanza kabisa ni safi kiadili, kisha yenye kufanya amani, yenye kukubali sababu, tayari kutii, yenye kujaa rehema na matunda mema, isiyofanya tofauti zenye ubaguzi, si ya kinafiki. 18 Zaidi ya hayo, tunda la uadilifu hupandwa mbegu yalo chini ya hali zenye amani kwa ajili ya wale wanaofanya amani.