Yakobo
2 Ndugu zangu, nyinyi hamshiki imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, utukufu wetu, kwa matendo ya upendeleo, je, mnafanya hivyo? 2 Kwa maana, ikiwa mwanamume mwenye pete za dhahabu kwenye vidole vyake na aliyevaa mavazi maridadi aingia ndani ya kusanyiko lenu, lakini mtu maskini aliyevaa mavazi yenye uchafu wa kuchukiza aingia pia, 3 lakini mwamtazama kwa upendeleo yule aliyevaa mavazi maridadi na kumwambia: “Wewe kalia kiti hiki hapa mahali bora,” nanyi mwamwambia aliye maskini: “Wewe fuliza kusimama,” au: “Kalia kiti kile pale chini ya kibago cha miguu yangu,” 4 nyinyi mna tofauti za kitabaka miongoni mwenu wenyewe nanyi mmekuwa mahakimu mkitoa maamuzi maovu, je, sivyo ilivyo?
5 Sikilizeni, ndugu zangu wapendwa. Mungu alichagua walio maskini kwa habari ya ulimwengu wawe matajiri katika imani na warithi wa ule ufalme, alioahidi wale wampendao yeye, je, hakufanya hivyo? 6 Ingawa hivyo, nyinyi mmemvunjia heshima mtu maskini. Matajiri huwaonea nyinyi, nao huwakokota mbele ya mahakama za sheria, je, hawafanyi hivyo? 7 Wao hukufuru jina bora ambalo kwalo mliitwa, je, hawafanyi hivyo? 8 Sasa, ikiwa mwazoea kutekeleza sheria ya kifalme kulingana na andiko: “Lazima umpende jirani yako kama wewe mwenyewe,” mnafanya vema kabisa. 9 Lakini ikiwa mwaendelea kuonyesha upendeleo, mnafanya dhambi, kwa maana mwakaripiwa na sheria kuwa wakiukaji-sheria.
10 Kwa maana yeyote yule ashikaye Sheria yote lakini achukua hatua isiyo ya kweli katika jambo moja, amekuwa mkosaji dhidi ya yote. 11 Kwa maana yeye aliyesema: “Lazima usifanye uzinzi,” alisema pia: “Lazima usiue kimakusudi.” Sasa, ikiwa wewe hufanyi uzinzi lakini waua kimakusudi, umekuwa mkiukaji-sheria. 12 Fulizeni kusema katika njia hiyo na kufuliza kufanya katika njia hiyo kama wafanyavyo wale watakaohukumiwa kwa sheria ya watu huru. 13 Kwa maana yeye asiyezoea rehema atapata hukumu yake bila rehema. Rehema huchachawa kwa shangwe ya ushindi juu ya hukumu.
14 Ina manufaa gani, ndugu zangu, ikiwa mtu fulani asema ana imani lakini hana kazi? Imani hiyo haiwezi kumwokoa, je, yaweza? 15 Ikiwa ndugu au dada yumo katika hali ya uchi na anakosa chakula cha kutosha kwa siku, 16 lakini mtu fulani kati yenu awaambia wao: “Nendeni kwa amani, fulizeni kujipasha moto na kulishwa vizuri,” lakini nyinyi hamwapi mahitaji ya lazima ya mwili wao, ina manufaa gani? 17 Hivyo, pia, imani ikiwa haina kazi, imekufa ndani yayo yenyewe.
18 Hata hivyo, mtu fulani atasema: “Wewe una imani, nami nina kazi. Nionyeshe imani yako bila kazi, nami nitakuonyesha imani yangu kwa kazi zangu.” 19 Wewe waamini kuna Mungu mmoja, sivyo? Unafanya vema kabisa. Hata hivyo roho waovu waamini na kutetemeka sana. 20 Lakini je, wewe wajali kujua, Ewe binadamu mtupu, kwamba imani bila kazi haina utendaji? 21 Je, Abrahamu baba yetu hakutangazwa kuwa mwadilifu kwazo kazi akiwa amekwisha kutoa Isaka mwana wake juu ya madhabahu? 22 Nyinyi mwaona kwamba imani yake ilifanya kazi pamoja na kazi zake na kwa kazi zake imani yake ilikamilishwa, 23 na andiko likatimizwa lisemalo: “Abrahamu aliweka imani katika Yehova, na ilihesabiwa kwake kuwa uadilifu,” naye akaja kuitwa “rafiki ya Yehova.”
24 Mwaona kwamba mtu atatangazwa kuwa mwadilifu kwazo kazi, na si kwa imani pekee. 25 Kwa namna ileile je, Rahabu kahaba hakutangazwa pia kuwa mwadilifu kwazo kazi, akiisha kupokea wale wajumbe kwa ukaribishaji-wageni na kuwatoa nje kwa njia nyingine? 26 Kwa kweli, kama vile mwili bila roho umekufa, ndivyo pia imani bila kuwa na kazi imekufa.