Yakobo
Barua ya Yakobo
1 Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo, kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika huku na huku:
Salamu!
2 Fikirieni yote kuwa shangwe, ndugu zangu, mkutanapo na majaribu ya namna mbalimbali, 3 kama mjuavyo kwamba ubora huu uliojaribiwa wa imani yenu hutokeza uvumilivu. 4 Lakini acheni uvumilivu uwe na kazi yao ikiwa kamili, ili nyinyi mpate kuwa kamili na timamu katika mambo yote, bila ukosefu katika kitu chochote.
5 Kwa hiyo, ikiwa yeyote kati yenu anakosa hekima, acheni afulize kumwomba Mungu, kwa maana yeye huwapa wote kwa ukarimu na bila kushutumu; naye atapewa hiyo. 6 Lakini acheni afulize kuomba katika imani, bila kutia shaka hata kidogo, kwa maana yeye atiaye shaka ni kama wimbi la bahari liendeshwalo na upepo na kupeperushwa huku na huku. 7 Kwa kweli, acheni mtu huyo asidhani kwamba atapokea kitu chochote kutoka kwa Yehova; 8 yeye ni mtu wa kusitasita kuamua, asiye imara katika njia zake zote.
9 Lakini acheni ndugu aliye wa hali ya chini achachawe juu ya kukwezwa kwake, 10 na aliye tajiri juu ya kutwezwa kwake, kwa sababu kama ua la mimea atapitilia mbali. 11 Kwa maana jua huchomoza pamoja na joto lalo lenye kuchoma na kunyausha mimea, na ua layo huanguka na ule uzuri wa kuonekana kwalo kwa nje huharibika. Ndivyo, pia, mtu tajiri atakavyonyauka katika njia zake za maisha.
12 Mwenye furaha ni mtu afulizaye kuvumilia jaribu, kwa sababu akiisha kukubaliwa atapokea taji la uhai, ambalo [Yehova] aliahidi wale waendeleao kumpenda. 13 Wakati yuko chini ya jaribu, acheni yeyote asiseme: “Mimi ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na mambo maovu wala yeye mwenyewe hamjaribu yeyote. 14 Lakini kila mmoja hujaribiwa kwa kuvutwa na kutongozwa na tamaa yake mwenyewe. 15 Kisha tamaa, wakati imetungika mimba, huzaa dhambi; nayo, dhambi, wakati imetimilika, hutokeza kifo.
16 Msiongozwe vibaya, ndugu zangu wapendwa. 17 Kila zawadi njema na kila upaji mkamilifu ni kutoka juu, kwa maana huteremka kutoka kwa Baba wa mianga ya kimbingu, na kwake yeye hakuna badiliko-badiliko la kugeuka kwa kivuli. 18 Kwa sababu yeye alipenda hilo, alituzaa sisi kwa njia ya neno la kweli, ili sisi tuwe matunda fulani ya kwanza ya viumbe vyake.
19 Jueni hili, ndugu zangu wapendwa. Kila mtu lazima awe mwepesi sana juu ya kusikia, wa polepole juu ya kusema, wa polepole juu ya hasira ya kisasi; 20 kwa maana hasira ya kisasi ya binadamu haitokezi uadilifu wa Mungu. 21 Kwa sababu hiyo wekeni mbali uchafuko wote wenye kuchukiza na jambo lile lenye kuzidi bure, ubaya, na pokeeni kwa upole kupandwa kwa neno liwezalo kuokoa nafsi zenu.
22 Hata hivyo, iweni watekelezaji wa neno, na si wasikiaji tu, mkijidanganya wenyewe kwa kuwazawaza kusiko kwa kweli. 23 Kwa maana ikiwa yeyote ni msikiaji wa neno, na si mtekelezaji, mtu huyu ni kama mtu ambaye anatazama uso wake wa asili katika kioo. 24 Kwa maana yeye hujitazama mwenyewe, na huyo aenda zake na mara husahau yeye ni mtu wa namna gani. 25 Lakini yeye achunguaye ndani ya sheria kamilifu iliyo ya uhuru na ambaye hudumu katika hiyo, mtu huyu, kwa sababu amekuwa, si msikiaji msahaulifu, bali mtekelezaji wa kazi, atakuwa mwenye furaha katika kutenda hiyo.
26 Ikiwa mtu yeyote ajiona mwenyewe kuwa mwabudu wa kidesturi na bado hauongozi kwa hatamu ulimi wake, bali aendelea kudanganya moyo wake mwenyewe, namna ya ibada ya mtu huyu ni ya ubatili. 27 Namna ya ibada iliyo safi na isiyo na unajisi kwa maoni ya Mungu wetu na Baba ni hii: kutazama mayatima na wajane katika dhiki yao, na kufuliza kujitunza mwenyewe bila doa kutokana na ulimwengu.