Angalia Usidanganywe
KWA VILE udanganyifu umezidi mno katika ulimwengu, ni lazima kila mtu aangalie zaidi sana asije akadanganywa. Haya ni mawazo fulani yanayoweza kuwa yenye kukufaa.
● Watu wengi wanaonunua vitu kwa njia ya kuagiza kwa posta wananung’unika kwamba hawapokei zile bidhaa walizolipia. Hivyo ikiwa unanunua kwa njia ya posta, fanya biashara na kampuni inayosifiwa vizuri kuwa inaaminika. Tunza pia nakala za barua zote na vilevile maandishi ya agizo lako. Lipa kwa njia ya hundi (cheki) au money order, si kwa fedha taslimu.
● Unaponunua vitu madukani, uwe mwangalifu. Kwa mfano, kama unanunua nyama au mazao ambayo ni lazima yapimwe kwa mizani, simama mahali ambapo unaweza kutazama mizani na mikono ya mwuzaji vilevile. Kufanya hivi kutamfanya mtu anayepima asidanganye.
● Ikiwa unalipa fedha kwa bidhaa nyingi ambazo umenunua, mwache yule karani wa kupokea malipo aone ukivihesabu vile vitu ambavyo umenunua. Atakuwa mwangalifu zaidi asikosee. Hesabu fedha za kichele (chenji, au senti unazorudishiwa zikibaki ukiisha kulipa) kabla ya kuondoka mbele ya karani anayepokea malipo. Kurudishiwa senti pungufu ni njia mojawapo ya njia zinazotumiwa na watu wengi zaidi ili kudanganya wanunuzi bila kukusudia au kwa kukusudia.
● Ukitaka kitu fulani kilichoharibika kitengenezwe, inafaa kutafuta kampuni au mtengenezaji anayesifiwa kuwa mwaminifu. Tena, uliza ili upate kujua mapema kadiri ya kiasi kinachohitajiwa na kupata maandishi ya kiasi hicho. Ni lazima kukadiri huku kutie na maneno ya kusema kwamba hutatozwa fedha zaidi ya hizo zilizokadiriwa bila ya idhini yako kwanza.
● Uwe mwangalifu sana unapotia sahihi yako (kusaina). Sahihi yako yaweza kukupeleka kortini au kukufunga. Soma kwa uangalifu sana kabla ya kutia sahihi yako. Ikiwa msemo unaotumiwa katika mapatano si wenye kufahamika sana nawe hujui maana yake, mwulize mtu anayejua akusaidie. Jambo jingine la kuangalia ni zile nafasi wazi zisizo na maandishi katika mapatano, au mwandiko usiosomeka vizuri au tarakimu (namba) zinazoweza kugeuzwa zisomeke vingine baadaye upate kudanganywa. Tunza maandishi yote yaliyotiwa sahihi katika kiweko chako cha maandishi.
● Unaponunua vitu vingi sana, uliza maulizo upate kujua bei zo zote za siri. Chunguza ili ujue kama ni lazima ulipe fedha zaidi kwa ajili ya upelekaji, kazi ambayo unafanyiwa, na kadhalika. Ikiwa unakopeshwa, hakikisha kujua malipo yote yatakuwa kiasi gani. Iwapo unakodi au unapanga nyumba, uliza juu ya kupaka rangi, vitu vilivyoharibika na vinahitaji kutengenezwa na vifaa vingine. Lakini usifanye ahadi zo zote ziwe za maneno tu, bali ziandikwe.
● Mara nyingi watembeza bidhaa (wachuuzi) wanatoa maneno matupu ya kuhakikisha bidhaa kuwa imara, lakini maneno matupu hayakubaliwi kortini hata kidogo. Wengine wanasema “fedha zitarudishwa upesi kama cho chote hakifai.” Lakini mara nyingi watu hawarudishiwi fedha ikiwa bidhaa ni mbaya.
● Ikiwa taarifa za malipo (statements) zinatumiwa, hakikisha kwamba risiti zote unazotia sahihi yako zimeandikwa waziwazi jumla ya malipo na kwamba haiwezi kugeuzwa kwa njia ya kukudanganya. Ukipoteza taarifa, piga ripoti mara hiyo, maana ni lazima ufanye hivyo au sivyo unaweza kupata taabu. Tunza risiti zako zote na kuzilinganisha kwa uangalifu na taarifa au stetimenti za kila mwezi.
● Unapotoa malipo ya kutibiwa hospitalini au mahali pengine, watu wengi wanaona inafaa kuomba risiti iandikwe hivi, “Paid in full” (“Zimelipwa zote”), ili kuepuka matatizo yanayoweza kutokea baadaye, badala ya kuandika tu hivi, “Paid” (“Zimelipwa”).
Ikiwa ungetaka usidanganywe siku hizi wakati bei zinapoendelea kupanda juu na udanganyifu nao unaongezeka, ni lazima uwe mwangalifu, uwe macho.