Sura ya 6
Matatizo ya Kifedha—Kuna Msaada Gani?
“KULA karamu kunakufanya wewe ufurahi na divai inakuchangamsha wewe, lakini huwezi kupata lo lote la mambo hayo usipokuwa na pesa.”—Mhubiri 10:19, Good News Bible.
2 Fedha ni kitu kinachohangaikiwa sana katika nchi zote. Sababu moja ya kuzihangaikia ni infuleshoni. Kila siku gharama za maisha zinapanda. Watu wengi hata hawana pesa za kununua chakula wanachohitaji. Wanaume zaidi na zaidi wanalazimika kuwa na kazi mbili, na wake zaidi na zaidi wanaacha kukaa nyumbani wakafanye kazi. Jamaa zinaumia. Afya inaharibika. Kwa ujumla matatizo hayo ya kifedha yanazidi kuwa magumu wakati watu wanapoanza kukopa vitu wavilipie baadaye. Kwa sababu ya kutegemea ukopaji, watu wengi walio na deni kubwa sana wanazidi kukopa vitu ambavyo kusema kweli hawavihitaji. Inakuwa hivyo katika maeneo ambako watu wana fedha chache, wala si katika nchi zenye maendeleo tu.
3 Biblia inatoa msaada gani wenye mafaa? Je! inaweza kukusaidia wewe upate kazi au udumishe kazi uliyo nayo? Je! inaweza kupunguza wasiwasi wa jamaa yako kuhusu fedha, kisha maisha yawe yenye furaha zaidi?
JE! UNYOFU NA JUHUDI KAZINI VINASAIDIA?
4 “Watu wanaofanya kazi kwa juhudi hawapati pumziko zuri. Je! wewe unakubali?” Katika uchunguzi uliofanywa, asilimia 85 ya watu walikubali. Mara nyingi inaelekea kuwa kwamba kufanikiwa kwa watu kunategemea kudanganya, kuiba, kuhonga au kuhongwa na kujulikana sana. Lakini Maandiko yanatilia mkazo ubora wa unyofu na kufanya kazi kwa juhudi. Kwa mfano, Biblia inasema hivi:
“Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe.”—Waefeso 4:28.
“Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. Je! wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme.”—Mithali 13:4; 22:29.
“Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu.”—1 Wathesalonike 4:11, 12, Habari Njema kwa Watu Wote.
5 Kupita kwa wakati na matukio mengi maishani kumethibitisha kwamba maoni hayo yanasaidia. Ndiyo, ni kweli kwamba wavivu fulani wanaelekea kupata mafanikio zaidi ya watu wengine. Lakini kwa ujumla na pia hatimaye, ukifuata mashauri ya Biblia utafanikiwa zaidi ya wale wanaoyapuza.
6 Mara kwa mara matajiri wa kazi wanalalamika wakisema wafanya kazi wanafika wakiwa wamechelewa, wanalofa (wanakaa tu bila kufanya kazi), ni wachafu-wachafu wala hawawezi kuaminiwa. Kwa hiyo mtu asiyechelewa kazini, aliye mwangalifu, safi, mwenye kuaminika na mwenye bidii kwa sababu ya kufuata kanuni za Biblia, atafutapo kazi ataipata. Na inaelekea ndiye atakayechuma fedha nyingi zaidi, maana mara nyingi matajiri wa kazi wanapenda kutoa fedha kwa ajili ya kazi iliyofanywa vizuri. Habari nyingi zimesimuliwa na Mashahidi wa Yehova kuonyesha hivyo ndivyo ilivyo. 7 Lakini siku hizi ni lazima mtu aseme uongo na kudanganya, au sivyo? Wakristo wamekataa kuiba, kusema uongo au kudanganya kwa sababu ya kutumia kanuni za Biblia, nao wameona kwamba mashauri ya Kimaandiko yanasaidia.
Shirika moja la Johannesburg, Afrika Kusini, lililokuwa na kazi ya kuuza vifaa vya nguvu za umeme lilikuwa likifilisika. Sababu moja ni kwamba wafanya kazi wengi walikuwa wakiiba. Siku moja meneja wa shirika hilo akawakusanya Waafrika wote pamoja na kuwafukuza wote. Lakini asubuhi yake mfanya kazi mmoja akawa akisafiri katika gari-moshi kama kawaida akafanye kazi, akakutana na mfanya kazi mwenzake. Akamwuliza huyo, ‘Imekuwaje unakwenda kazini?’ Yule mfanya kazi mwingine akasema meneja wa shirika alimwambia faraghani kwamba yeye hangefukuzwa kazini kwa sababu alikuwa mtu mnyofu. Naye yule mwanamume wa kwanza akasema aliambiwa ivyo hivyo. Walipofika kazini wakakuta mfanya kazi mwingine wa tatu ambaye pia alikuwa ameambiwa faraghani afike kazini kama kawaida. Wote hao walikuwa ni Wakristo wa kweli.
Robert alikuwa mfanya kazi wa shirika la Kiingereza la ujenzi wa barabara. Siku moja mkurugenzi akasema mtu ye yote akipiga simu, Robert amweleze hayupo. Lakini Robert alipokuwa akijibu simu moja akaeleza kwamba mkurugenzi ana kazi nyingi. Kusikia hivyo, mkurugenzi akamchambua-chambua. Lakini matata yalikwisha wakati Robert alipomweleza kwamba hangeweza kusema uongo kwa manna yeye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. (Waefeso 4:25) Baadaye, Robert alipopangiwa kupandishwa cheo, mfanya kazi mwenzake mwenye pupa alijaribu kutokeza mashaka akisema Robert hakuwa mtu mnyofu. Hapo sasa mkurugenzi akanena kwa uthabiti akitetea unyofu wa Robert. Robert alipandishwa cheo.
8 Je! unaweza kuwa mnyofu ikiwa unajifanyia kazi yako mwenyewe? Katika visa fulani huenda unyofu ukaelekea kutokufaa. Lakini huo ungali ndio mwendo bora zaidi. Unakusaidia uwe na dhamiri safi mbele za Mungu na kupata amani ya akilini. Zaidi ya hilo, watu wengi wanapendelea zaidi kufanya kazi na mtu wanayeamini hatawadanganya. Ni kama vile Biblia inavyosema –‘unajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo.’
MSAADA KUHUSU UKOSEFU WA MAKAO
9 Kupata makao mazuri ni tatizo jingine kubwa. Katika nchi nyingine jamaa nzima-nzima zinalazimika kuishi zikiwa zimesongamana katika chumba kimoja. Au, huenda tatizo likawa ni kupata nyumba safi isiyo ya fedha nyingi mno. Je! Biblia ina msaada wa kutatua matatizo hayo?
10 Wakati unapokodi nyumba kwa muda mfupi au mrefu, unatumia mali ya mtu mwingine. Unastahili kuangalia kwamba Mungu aliwahimiza Waisraeli waheshimu na kutunza mali za wengine. (Kumbukumbu la Torati 22:1-4) Aliwatia moyo pia wawe safi kimwili. (Kumbukumbu la Torati 23:12-14; Kutoka 30:18-21) Kwa hiyo, Wakristo waaminifu wanajaribu kuepuka kuharibu mali, tena wanaiweka nyumba yo yote wanayokodi katika hali safi. Kwa sababu hiyo, na kwa sababu ‘wanaishi kwa utulivu,’ wanathaminiwa mahali pengi kuwa wapangaji wazuri, na imekuwa vyepesi kwao kupata nyumba.
Jamaa moja ya Kikristo ilikodi nyumba ya mtu fulani ambaye hapo zamani alikuwa meya wa mji mkuu wa nchi moja ya Afrika. Wao waliendelea kuliweka jengo lake katika hali safi na kulipa kodi ya nyumba bila kuichelewesha. (Warumi 13:8) Walipokaribia kuhama wakajulisha mwenye nyumba kwa jamaa nyingine ya kundi lao. Mwenye nyumba akasema kwamba mtu anapohama yeye ‘anaongeza’ kodi wakati mtu mwingine anapoingia, kisha kodi inakuwa maradufu. Lakini kwa sababu alijua Wakristo hawa wangekuwa watu wa kutegemeka, watu safi, hakuipandisha kodi, ikabaki ikiwa karibu nusu ya kiasi kilichotozwa nyumba za namna hiyo mahali hapo.
11 Hata wakati hali zenye kulemea mtu zinapomzuia kupata nyumba nzuri zaidi, bado anafaidika. Yeye anatunza usafi wa nyumba yake na kuifanya nadhifu. Basi maisha yanakuwa ya afya bora na ya furaha zaidi.
KUTUMIA FEDHA ZAKO KWA HEKIMA
12 Mfalme Sulemani mwenye utajiri aliandika hivi: “Hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.”—Mhubiri 7:12.
13 Sulemani alijua fedha zinatoa ulinzi wa kujikinga na taabu zinazoweza kutokana na umaskini, na lazima sisi pia tujue hivyo. Kwa hiyo fedha si za kutumiwa ovyo ovyo; zinapasa kutumiwa kwa hekima. Biblia inatutolea mashauri gani yenye mafaa juu ya kutumia vizuri fedha zetu?
14 Yesu aliuliza hivi: “Ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki.”—Luka 14:28-30.
15 Maneno hayo yanaweza kutumiwa kuhusiana na fedha za jamaa. Watu wengi waliooana wameona ni vema kukaa kitako wapange kwa utulivu matumizi ya fedha zao waone kama inawezekana na ni hekima kununua kitu fulani cha bei kubwa. Wamezidi kusaidiwa na kumbusho la Biblia kwamba mambo yasiyotazamiwa yanatukia. (Mhubiri 9:11) Kufanya hivyo kumewasaidia waepuke kushtukia kununua vitu wasivyokuwa wamepanga kununua na hivyo wanaepuka deni za muda mrefu.
16 Pia, angalia maneno haya ya busara: “Akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” (Mithali 22:7) Ingawa Biblia haikatazi kukopa au kukopesha, inatufungua macho tuone kwamba kukopa-kopa bila lazima kunaweza kufanya mtu awe mtumwa wa benki au wa mkopeshaji. Mwenye hekima ni yule anayekumbuka kwamba siku hizi watu wengi wanashawishika wanunue vitu kwa mikopo, kisha wanajikuta wakiwa na deni, wakilipa faida kubwa.
17 Biblia imesaidia jamaa nyingi kupunguza matatizo ya kifedha kwa kuacha kutupa chakula na vitu vingine. Yesu alituwekea mfano mwema. Alipokwisha kulisha kundi kubwa la watu, aliagiza masalio yakusanywe. (Yohana 6:10-13) Wakristo wazee na vijana wanaweza kuepuka sana kutupa chakula na fedha kwa kufuata mfano huo.
18 Ili mtu ajue kufuata mashauri ya Biblia kuhusu fedha huenda akahitaji abadili sana maoni yake, lakini atapata faida nyingi, kama kinavyoonyesha kisa kinachofuata:
Vijana wawili (mvulana na msichana) walianza kupatwa na matatizo ya kifedha muda mfupi baada ya kuoana huko Zimbabwe. Mshahara wa mume huyu ulikuwa mdogo; mke naye alitaka wawe na vitu vingi vipya na wale vyakula bora. Basi mke naye akaanza kufanya kazi, lakini ilikuwa ni kama kazi bure tu. Ndoa yao ilizidi kuharibika sana hata kukawa na mashaka ya kuishi pamoja. Wazee fulani wa Kikristo waliwasaidia. Walitumia Biblia wakazungumza nao umaana wa kupanga matumizi ya fedha zao. (Luka 14:28-30) Vijana hao waliooana waliyaona mafaa ya kupanga orodha ya ununuzi kwa kukadiria bei za vitu na kununua kwa wingi vyakula vya juma nzima ili waokoe kiasi fulani cha fedha kwa njia hiyo. (Mithali 31:14) Wazee wakazungumza nao mashauri ya Kimaandiko juu ya kuridhika na vitu walivyo navyo na uhitaji wa kuepuka tamaa ya vitu vya anasa wasivyokuwa na fedha za kuvinunua. (Luka 12:22-31) Lo! mashauri hayo ya Kimaandiko yalisaidia sana! Vijana hao walipata furaha zaidi kwa sababu ya kutulia zaidi wasitumie fedha zao vyo vyote tu. Hata jirani walisema ndoa yao ilikuwa imepata maendeleo.
19 Wale walio na mapato yasiyoongezeka wamefaidika pia kutokana na maoni ya Biblia yenye mafaa. Ndivyo ilivyokuwa katika Spania kwa wazee-wazee waliooana:
Mapato ya Francisco na Maria ni madogo sana wala hayatoshi. Hata hivyo wanasema wanaishi vizuri kwa kutumia mambo wanayojifunza katika Maandiko. Kwa mfano, Mithali 6:6-8 inasema: ‘Mwendee chungu, zitafakari njia zake ukapate hekima. Hujiwekea akiba ya chakula wakati wa jua; hukusanya chakula chake wakati wa mavuno.’ Maria anasema alijifunza kufanya hivyo, akawa akinunua vitu wakati vilipokuwako kwa wingi vikiwa vya bei ndogo, kama wakati matunda yalipopatikana kwa wingi. Pia yeye anangojea vipindi ambavyo bei za mavazi zinapunguzwa madukani ili anunue mavazi atakayovaa mwaka unaofuata. Wao ‘wanajiwekea chakula wakati wa jua’ kwa kulima kishamba kilichoko umbali wa mwendo wa dakika 45 kutoka nyumbani kwao. Maneno ya 1 Yohana 2:16 yanasaidia pia. Wamejifunza kuridhika na vifaa vya kupambia nyumba yao hata ikiwa ni vya kizamani. Na badala ya kuwa na tafrija za fedha nyingi, wao wanafurahia kusaidia wengine wajue habari za Mungu.
EPUKA KUFAGIA FEDHA ZOTE
20 Kuingilia mazoea kama ya dawa za kulevya au kulewa pombe, kuvuta sigara na kucheza kamari kunaweza kumaliza fedha zako zote. Biblia inatusaidia pande hizi, pia.a
21 Ebu fikiria pombe. Biblia haikatazi kutumia vileo kwa kiasi. Lakini inatoa maoni haya:
“Wapendao anasa huendelea kuwa maskini; hatatajirika yeye anayependa divai na maisha mazuri.”
“Usiwe mmoja wa wale wanaozoea kunywa-kunywa divai daima . . . kwa maana mlevi na mlafi wanajifukarisha, na kichwa chenye kusinzia-sinzia hufanya mtu awe mvaaji wa matambara.”—Mithali 21:17; 23:20, 21, Jerusalem Bible.
22 Kunywa kupindukia kunafagia fedha zote kwa njia mbalimbali. Vileo (pombe) vyenyewe ni vya bei kubwa, kwa maana watu wengine wanatumia hata nusu ya mshahara wao wakinywa pombe. Katika mkoa mmoja tu wa Quebec, Kanada, dola zaidi ya bilioni moja zinatumiwa kila mwaka katika unywaji wa pombe. Bilioni nyingine moja inamalizwa na mambo yanayohusiana na unywaji wa kupita kiasi—kukosa kufika kazini na kupata misiba ya barabarani inayohusiana na ulevi.
Katika kusini mwa Chile mwuza-viatu alifutwa kazi kwa sababu ya ulevi. Ndipo akajaribu kushona viatu vilivyoraruka katika kibanda kilichokuwa karibu na nyumba iliyoharibika-haribika ambamo jamaa yake iliishi kwa kuikodi. Hata hivyo, akawa akitumia kiasi kikubwa cha fedha zake akinunua pombe hata ikawa kawaida ya mkewe kulazimika kwenda kumkomboa gerezani. Mke alilazimika kukaa mpaka usiku sana akitengeneza nywele za bandia ili wapate fedha za chakula. Lakini ndipo mke huyo alipoanza kujifunza Biblia na Mashahidi wa Yehova, na funzo hilo likamfanya amhurumie na kumsaidia zaidi mume wake badala ya kumwonea ubaya. Basi ikawa kwamba mumewe alianza kuhudhuria funzo hilo. Akajifunza kwamba mtu hawezi kuwa mlevi na bado awe Mkristo, basi akaacha kunywa. Jamaa ikawa na chakula kizuri zaidi. Baada ya muda fulani hata wakanunua nyumba ndogo na duka, kisha akawa akitumia duka hilo kuendesha kibiashara cha kutengeneza viatu vilivyoraruka.
23 Namna gani kucheza kamari, kuwe ni kwenye uwanja wa mbio za farasi au kwenye jumba la kamari au kutumia tikiti za bahati-nasibu? Watu wengi wanapatwa na matatizo ya kifedha kwa sababu ni wacheza-kamari wa kupindukia. Wao wanazidi kujikaza tu wakidhani watapata “donge nono,” lakini ng’o! Wanaponda mapesa yao bure, na mara nyingi jamaa zao zinataabika sana.
24 Mwanamume mmoja Mwaustralia anasema kwamba kwa miaka mingi “kucheza kamari kulikuwa tamaa iliyokaa imara akilini mwangu. Nilikuwa nikicheza kamari siku saba kila juma, na kama siku zingaliweza kuongezwa zizidi hapo ningalicheza sana.” Alikopa-kopa rafiki zake mpaka wakaanza kumwepa. “Nyakati nyingine nilipomalizwa fedha zangu nilikuwa nikipiga kichwa ukutani na kumsihi mke wangu nikimwambia, ‘Tafadhali nipe shilingi 5 tu. Hakika nitashinda.’ ”
25 Alipoanza kujifunza Biblia, alivutwa na shauri hili la Yesu: “Jihadharini na kila aina ya tamaa.” (Luka 12:15, HNWW; 1 Wakorintho 6:9, 10) Mwanamume huyo alikata kauli kwamba mchezo wake wa kamari ulimwonyesha kuwa mwenye pupa nyingi sana, basi akajiachisha kamari. Kwa kuwa sasa aliweza kufaidi jamaa kwa mshahara wake, aliweza kuithamini zaidi mithali hii: “Utajiri uliopatikana kwa kutunga hila [“utajiri unaotokana na kucheza kamari,” Living Bible] utapungua; lakini yeye akusanyaye kidogo kidogo ataongeza ghala yake.”—Mithali 13:11, An Ameri-can Translation.
KURIDHIKA KUNASAIDIA
26 Kwa habari ya fedha, maoni ya mtu binafsi ndiyo yanayoweza hasa kurekebishwa na Biblia. Kwenye 1 Timotheo 6:7-10 tunasoma hivi:
“Tulileta kitu gani katika ulimwengu? Hakuna! Tunaweza kuchukua kitu gani katika ulimwengu? Hakuna! Basi, ikiwa tuna chakula na nguo, hivyo vyapasa vitutoshe. Lakini wale wanaotaka kuwa matajiri hutumbukia ndani ya kishawishi na kunaswa katika mtego wa tamaa nyingi za kipumbavu na zenye kuumiza. . . . Wengine wamekuwa na hamu kubwa sana ya kupata [fedha] hata wakatanga-tanga wakiiacha ile imani, na wamevunja mioyo yao kwa huzuni za namna nyingi.”—Good News Bible.
27 Wale wanaopenda fedha hawazishibi kamwe, wawe ni maskini au ni matajiri. Mtu mwenye bidii na mwenye cheo kikubwa katika California alimwambia mkewe hivi: “Mimi nataka kuwa tajiri . . . nami nikiambiwa nichague nitakacho zaidi, kati ya wewe na [shirika la kazi], wewe ndiwe utaumia.” Akawa mkuu wa shirika kubwa la kazi, akawa milionea, naye anaishi katika nyumba ya dola 700,000. Na bado yeye anasema: “Cho chote nilicho nacho hakinitoshi.” Ukweli ni kwamba fedha sizo zinazohakikishia mtu atapata furaha. Miaka miwili kabla ya kifo chake, J. P. Getty, milionea aliyekuwa akiuza mafuta, alisema hivi: “Fedha hazileti furaha. Labda zinaleta huzuni.”
28 Ingawa Biblia haikatazi watu wasiwe na fedha au mali, inaonya vikali juu ya kusitawisha kupenda fedha. Inatukumbusha kwamba uzima hautokani na mali zetu.—Luka 12:16-20.
29 Kwa hiyo badala ya kujaza maisha yako wasiwasi mwingi ukijitahidi kupata utajiri, ridhika na ulicho nacho au kile unachoweza kupata kwa kiasi. Maneno ya Yesu kwenye Luka 12:22-31 yanaweza kutusaidia tuwe na maoni hayo:
“Msisumbukie maisha yenu, mtakula nini; wala miili yenu, mtavaa nini. Kwa kuwa maisha ni zaidi ya chakula, na mwili ni zaidi ya mavazi. Watafakarini kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege! . . . Ninyi, msitafute mtakavyokula wala mtakavyokunywa; wala msifanye wasiwasi, kwa maana, hayo yote ndiyo watafutayo mataifa ya duniani, lakini Baba yenu anajua ya kuwa mna haja na hayo.”
30Kuwa na mavazi ya bei kubwa, chakula kizuri na nyumba yenye vifaa vya kustarehesha huenda kukaleta furaha ya kiasi fulani, lakini vitu hivyo havitakuongeza walau mwaka mmoja kwenye maisha yako—huenda vikapunguza miaka mingi ya maisha hayo. Lakini unaweza kupata furaha nyingi maishani bila mali.
31 Wala si lazima uwe na utajiri ndipo uweze kupata rafiki. Mtu ye yote anayetumia fedha zake ili apate rafiki anakosea. “Rafiki” za namna hiyo wanakula chakula chako na kushiriki mali zako, lakini fedha zinapokwisha, nao wanakwisha.—Mhubiri 5:11; Mithali 19:6.
32 Lakini unapoyakubali maoni ya Biblia yaliyosawazika juu ya kazi, ukifurahia maisha na kutendea wengine mema, utapata “zawadi kutoka kwa Mungu.” Ni kama Mhubiri 3:12, 13, NW, anavyosema: “Hakuna lililo bora kwao kuliko mtu kushangilia na kufanya mema wakati wa maisha yake; na pia kwamba kila mtu amepaswa kweli kula na kunywa na kuona mema kwa kazi yake yote ya juhudi. Hiyo ndiyo zawadi kutoka kwa Mungu.”
33 Mashauri ya Mungu juu ya mambo hayo yanafaa sana hivi kwamba yanaweza kufanya mtu aulize hivi: Je! siku moja Mungu atakomesha umaskini kabisa kabisa, akomeshe ukosefu wa chakula cha kutosha na upewaji wa makao yasiyofaa, hayo yakiwa ni mambo ambayo mara nyingi yanahusiana na matatizo ya kifedha? Barabara! Na baadaye tutauzungumza ushuhuda unaoonyesha kuna msingi wa kusadiki hivyo. Lakini, kwanza, na tuangalie matatizo mengine yanayoharibu sana maisha za watu siku hizi.
[Maelezo ya Chini]
a Angalia pia Sura ya 10, “Afya Bora na Maisha Marefu Zaidi—Vipi?”
[Study Questions]
[Mambo ya Kuzungumziwa]
Sababu gani kuna uhitaji wa kupata msaada ili kutatua matatizo ya kifedha? (1-3)
Ni maoni gani tofauti, yenye mafaa, ambayo Biblia inatoa juu ya kazi? (Mhubiri 8:12, 13) (4-6)
Unyofu una ubora gani? (Warumi 2:14, 15) (7, 8)
Kuna shauri gani lenye mafaa kuhusu fedha? (12-16)
Watu wametumiaje maoni ya Biblia wakajifaidi? (17-19)
Kwa sababu gani mashauri ya Biblia juu ya kunywa pombe yanasaidia? (20-22)
Kucheza kamari kumeongezaje matatizo? (23-25)
Kwa sababu gani maoni ya Kibiblia juu ya kuridhika yana mafaa? (26, 27)
Ni shauri gani lenye kufaa alilotoa Yesu juu ya utajiri? (28-30)
Mashauri ya Kimaandiko yanaweza kukusaidiaje uwe na maisha bora? (31-33)
[Sanduku katika ukurasa wa 53]
MWANAMKE MFANYA-BIASHARA WA AMERIKA YA KUSINI
Katika Georgetown, Guyana, Norma mwenye umri wa miaka 48 alikuwa na vibanda vya mboga na matunda kwenye mojalapo la masoko yaliyo makubwa zaidi. Alikuwa akipunja watu kwa kutumia vipimo vya uongo. Ikiwa mtu anaagiza gramu 114 za samaki wa chumvi, alikuwa akimpimia gramu 85, na vivyo hivyo. Pia, yale mawe ya mizani hayakuwa na uzito uliotakwa. Basi, hakuna siku ambayo wanunuzi walipata kiasi kamili cha vitu vyao.
Jumapili moja mtu wa ukoo wake alimpa nakala ya “Mnara wa Mlinzi” uliozungumza juu ya matumizi ya kanuni za Biblia katika biashara. Maneno ya gazeti hilo yaliyohusu mazoea ya udanganyifu yalimlenga yeye barabara. (Mithali 20:23; Mambo ya Walawi 19:35, 36) Jumatatu Norma aliyatupa mawe ya uongo ya kupimia akanunua yenye vipimo vya kweli. Akaanza kuhudhuria mikutano kwenye Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova na kufunzwa Biblia. Ajapofanyiwa dhihaka na watu wa jamaa yake, yeye alizidi kusadiki kwamba alitenda jambo linalofaa.
Biashara yake iliendeleaje? Hangeweza kupata faida kutokana na bidhaa fulani bila kutumia udanganyifu, basi akaacha kuziuza. Lakini wanunuzi waliona yeye hawadanganyi kwa bidhaa zilizobaki, wakasema, ‘Tangu uwe Mkristo unatupatia bidhaa zinazopita fedha tunazokupa.’ Basi ikawa kwamba biashara yake ilisitawi zaidi. Kwa sababu ya kupata faida kwa njia nyofu, Norma alimaliza kulipia nyumba yake aliyokuwa ameiwekea rehani, akaweka kiasi fulani cha fedha katika benki na kutoa michango ya kusaidia wenye shida. Afya yake imekuwa bora, kwa maana sasa hapatwi tena na wasiwasi kama wakati alipokuwa akiogopa kupatikana akipunja watu.
[Sanduku katika ukurasa wa 59]
“Asilimia 87 ya watu wa Australia wameshiriki namna fulani ya kucheza kamari kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu iliyopita.”—“The Sunday Mail” (Brisbane)
“Afadhali Tucheze Kamari Kuliko Kula! Wakaaji wa Queensland wanatumia dola zinazokadiriwa kuwa milioni 12 kila juma wakicheza kamari—kiasi ambacho kinakaribia kile wanachotumia kununua vyakula na vitu vingine kama nyama.”—“The Sunday Mail” (Brisbane).
[Picha katika ukurasa wa 57]
Mashauri ya Biblia yamesaidia jamaa kupanga matumizi ya fedha zao
[Picha katika ukurasa wa 60]
Kanuni za Biblia zina mafaa gani juu ya ulevi, uvutaji wa sigara na uchezaji wa kamari?