Kategemezwa na Tumaini la Ufalme
KATIKA Aprili 1987 Lila, mwanamke aliye katika miaka yake ya 80, alimtazama mume wake akifa katika hospitali moja karibu na Portland, Oregon. Wauguzi walimkazia macho kwa huruma. Yeye alitazama maiti hiyo kisha akapiga hatua na kuipapasa.
“Wewe umekuwa mume mwema,” akasema. “Nitakuona katika ufufuo!” Halafu akageuka na kusema: “Nimesema hivyo kwa sababu mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Acheni niwaeleze.” Akaendelea na kusimulia juu ya ufufuo na ulimwengu mpya wa Mungu.
Baadaye, alipokuwa akiondoka hospitali, mtaalamu wa moyo aliyekuwa ametibu mume wake akamfikia katika kijia cha kupita ukumbini. Alitua akaeleza huruma zake. Lila naye akaanza papo hapo kueleza kwamba karibuni angemwona mume wake katika ulimwengu mpya kupitia ufufuo. Akatoa ushahidi mwingi kabla daktari hajaweza kuondoka hapo, huku akisema: “Lila, mimi natumaini itakuwa hivyo kwako.” Daktari alipokuwa akigeuka aende zake, Lila akasema: “Itakuwa hivyo hasa, nami nataka kukuona wewe pia huko!”
Bila Lila kujua, daktari huyo alikuwa ametembelewa na Mashahidi wa Yehova. Sasa, kwa kutazama jinsi imani ya Lila ilivyomwimarisha wakati wa mkazo wa kifo cha mume wake na kusikia tumaini lake chanya kwa wakati ujao, daktari huyo alitiwa moyo. Yeye na mke wake waliendelea na mazungumzo yao na Mashahidi wa Yehova.
Miezi michache baadaye, katika Januari 1988, Lila alianza kuwa mgonjwa na kujikuta hospitali. Utibabu ulikuwa haufanyi kazi na alionekana akiendelea kwisha. Yule mtaalamu wa moyo akapata habari hizo na mara hiyo akaenda kumzuru katika sehemu ya wagonjwa mahututi. Aliuliza hivi: “Sasa, Lila, unaendeleaje?”
“Yaonekana siendelei vizuri sana.”
“Unamkosa Erick, sivyo?”
“Ndiyo, nadhani namkosa, zaidi ya nyakati zote.”
Halafu akanena naye juu ya ahadi ya Biblia ya kumwona Erick tena katika ufufuo, na pia tumaini la uhai wa milele katika ukamilifu katika ulimwengu mpya. Kwa kweli, mambo haya haya ndiyo yale Lila aliyokuwa amemwambia mapema kidogo wakati mume wake alipokuwa amekufa! Ilikuwa ndiyo dawa bora zaidi ambayo daktari angeweza kumpa Lila. Lila alichangamka mara hiyo, akatoka hospitali mnamo juma hilo, na akarudia huduma ya Kikristo kwa nguvu zilizofanywa upya.
Na namna gani juu ya huyo mtaalamu wa moyo? Yeye na mke wake waliweka maisha zao wakfu kwa Mungu wakabatizwa kwenye mkusanyiko wa wilaya wa Mashahidi wa Yehova katika Corvallis, Oregon, katika Juni 1988.—Imechangwa.