Mazingira Yanayozorota
‘Jambo fulani lisipofanywa karibuni, twaweza kutarajia mzoroto wa kiuchumi wenye kuenea pote na msukosuko wa kijamii’
HUO ndio uliokuwa ujumbe wa Lester Brown, msimamizi wa Taasisi ya Worldwatch, kikundi cha utafiti wa kimazingira. Maelezo yake yalitokea katika ripoti ya kila mwaka ya “hali ya ulimwengu.”
Mazingira ya dunia, akasema Brown, yaendelea kuzorota. Matisho yahusuyo kupungua sana kwa gesi ya ozoni, ukavu, kumalizika kwa misitu, mmomonyoko wa udongo, na ongezeko la idadi ya watu yasipodhibitiwa, “mzoroto wa kiuchumi huenda usiepukike.” Aliandika kwamba mazao ya chakula ulimwenguni yamepungua kwa asilimia 14 kwa kila mtu tangu 1984 na kwamba akiba za nafaka zimeshuka kwa kadiri ambayo ndiyo ya chini zaidi katika muda wa miaka 15.
Brown alitaarifu hivi pia: “Wakati unatuishia. . . . Ni lazima tufanye jambo hilo katika miaka ya 1990. Baada ya hapo itakuwa kuchelewa mno. . . . Jambo ambalo litatuamsha kwa kishindo ni kama tuna mavuno mengine yenye kuhusiana na ukavu. Hapo ndipo tutajikuta bila nafaka ya kupeleka nje, na bei za nafaka ziongezeke mara mbili au mara tatu. Mkumbo huo wa hali ya kiuchumi utafanya upungufu wa mafuta uonekane kama si kitu kwa kulinganishwa.” Pia alionelea hivi: “Tayari imekuwa kuchelewa mno kwa sehemu fulani ya Afrika. Hakuna njia ya kubadili mambo huko. . . . Labda itakayofuata ni Amerika ya Kilatini.”
Mielekeo hiyo yapatana na unabii wa Biblia usemao juu ya njaa, magonjwa, vita, na kifo, huku binadamu ‘akiangamiza dunia’ katika wakati wetu. Yesu alitabiri kwamba jambo hili lingefikia upeo katika “dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu.” Hiyo itamaanisha mwisho wa huu mfumo wa mambo uliopo, kutayarisha njia kwa ajili ya ulimwengu mpya wenye kufanyizwa na Mungu.—Ufunuo 6:1-8; 11:18, HNWW; Mathayo 24:21; 2 Petro 3:10-13.