Fisi Mkosa Kueleweka
Ni wanyama wachache ambao wanaharibiwa sifa kuliko fisi. Na ni kweli kwamba wao si viumbe wa kupendeka sana. Yale macho madogo maangavu, ule mgongo wenye kuteremka chini, na ile hali ya ubaridi wa kutojali sana, yote hayo yanafanya wanadamu wanaotazama wawe na maoni ya kwamba yeye ana sura mbaya na ni mkorofi. Zaidi ya hilo, fisi anacheka na kuchekacheka kama mkichaa. Mara nyingi kilio chake chenye kutia huzuni na hofu kinapenya usiku wa Kiafrika kwa wembamba mkali unaoharibu utulivu. Sifa zote hizi zikiunganishwa pamoja huenda zikatosha kukutetemesha!
Lakini fisi wamenenewa vibaya mbele ya watu kuliko vile wanavyostahili. Hivyo basi acheni turekebishe mashtaka machache. Kwanza kabisa, mara nyingi fisi anafikiriwa kuwa mbwa wa namna fulani. Sivyo alivyo kamwe. Kwa kuwa yeye ni wa jamii tofauti, ufanano wake na mbwa ni wa juujuu tu.
Kwa kawaida fisi wanafikiriwa kuwa waoga pia. Lakini ni vigumu kwa waoga kuwa wawindaji wenye mafanikio. Eti wawindaji? Ndiyo, fisi si wala mizoga tu. Wakiwa na mabega yenye nguvu isivyo kawaida na taya zilizo imara kuliko za wanyama wote wa Kiafrika walio wala nyama, wao wanafanikiwa sana kuwinda windo lao wenyewe—hata wanyama wakubwa kama nyati. Kwa uhakika, wanahesabiwa kati ya wanyemeleaji hodari wa Afrika.
Alipokuwa akichunguza wanyama wala nyama wa kusini mwa Afrika, mara nyingi mtungaji Chris McBride aliwaona fisi kwa kweli wakifukuza simba majike kutoka kwenye windo lao wenyewe walipokuwa wakilila. Ni simba ndume peke yake ambaye angeweza kukinza shambulio la kikundi cha fisi. Kama fisi angekuwa mwoga kikweli, je! angekabiliana na adui wa kuogopesha jinsi hiyo? Haielekei hivyo.
Kwa Nini Yeye Anacheka?
Huenda mchekocheko wa fisi wa ukichaa ukasikika kuwa usiokupendeza. Lakini yeye anakuwa akiwasiliana tu na washiriki wenzake katika mbari yake. “Kila fisi mwenye madoa ana kilio chake mwenyewe kinachoweza kutambuliwa na fisi wengine,” anaeleza mstadi mmoja wa Afrika Kusini, Dakt. G. Mills. Kwa njia hii, washiriki wenye kutapakaa sana wa mbari hii wanajulishana wako wapi ili waweze kujumlika kwa haraka kuwa kikundi kimoja tena kukitokea uhitaji, kama vile wakilazimika kutetea eneo lao au kujumlika kuwa kikundi cha uwindaji. Msisimuko wao katika kuua windo au kugundua mzoga unatangazwa kwa “vichekocheko” vya sauti ya juu.
Lakini si fisi wote wanaocheka. Fisi wa rangi kahawia wa kusini mwa Afrika ni mdogo zaidi na mnyamavu kuliko fisi aliye wa kawaida zaidi mwenye madoa na anapendelea kujitafutia chakula peke yake badala ya kuwa katika vikundi-vikundi. Yeye anategemea zaidi kuwasiliana kwa harufu.
Kila mmoja anahamisha harufu yake iliyo tofauti kabisa iende kwenye vishina vya nyasi, vichaka, au miamba kwa kutokeza unga majimaji kutokana na vifuko maalumu vya mkundu. Hisia ya fisi ya kunusa ni kali sana hivi kwamba kutokana na huo unga wa majimaji inaonekana anaweza kufahamu jinsia, cheo cha kijamii, na hata utambulisho wa washiriki wenzake katika mbari.
Je! wewe unakosa kupendezwa na fisi? Ni kweli kwamba yeye si kipenzi wa kupapaswa wala mwenye kuvutia. Lakini si wanyama wote walio hivyo. Viumbe wengi wanatuvutia kwa sifa nyinginezo, kama vile nguvu na ujanja. Kwa kufikiria hilo, kuna mengi juu ya fisi ya kutuvutia na kutusisimua.