Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 8/22 kur. 23-27
  • Nyalaland—Paradiso Ambayo Haijaharibiwa na Binadamu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nyalaland—Paradiso Ambayo Haijaharibiwa na Binadamu
  • Amkeni!—1993
  • Habari Zinazolingana
  • Safarini Huko Ghana
    Amkeni!—2001
  • Je! Binadamu na Mnyama Waweza Kuishi kwa Amani?
    Amkeni!—1991
  • Simba—“Paka” Wenye Manyoya na Wenye Fahari wa Afrika
    Amkeni!—1999
  • Mbuga ya Kitaifa ya Nairobi Ambapo Wanyama Wako Huru
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 8/22 kur. 23-27

Nyalaland—Paradiso Ambayo Haijaharibiwa na Binadamu

Na mleta habari za Amkeni! katika Afrika Kusini

NI BADILIKO lenye kuburudisha kama nini kwa sisi wakaa-jijini wanane!

Tuko Nyalaland—eneo kubwa la kutembelea kwa miguu katika sehemu ya kaskazini ya Mbuga ya Kitaifa ya Kruger katika Afrika Kusini. Jina hilo latokana na aina ya swala mzuri unayeona picha yake katika ukurasa huu. Huyu ni nyala wa kiume.

Ni wakati wa usiku, nasi tumeketi nje tukiwa tumezunguka moto wa kuni tukila mtokoso wa nyama ya nyati. Kuna simba, chui, nyati, na wanyama wengine wenye fahari katika kichaka kilichotuzunguka. Lakini twahisi salama chini ya usimamizi wa walinzi wawili wa mbuga. Kwa kweli, tunajikumbusha kwamba ni salama zaidi hapa kuliko kuishi katika jiji lenye kujaa uhalifu au kusafiri katika barabara kuu yenye magari mengi.

“Mlimsikia bundi-skopi huyo?” auliza Kobus Wentzel, ambaye ndiye mlinzi mkuu wa mbuga. Arudia kwa ustadi mlio huo, prrrrup. “Huo,” aongezea, “ni mlio wa kawaida unaosikika katika eneo hili. Katika matembezi yetu ya kesho, nitawaonyesha baadhi ya ndege, kwa hiyo chukueni kitabu chenye habari za ndege.”

Nyalaland ni paradiso pia kwa wanabotania. Ni sehemu chache katika dunia zinazoweza kulingana nayo kwa unamna-namna wayo wa mimea. Sababu ya hilo, kulingana na Illustrated Guide to the Game Parks and Nature Reserves of Southern Africa, cha Reader’s Digest ni kwamba “tisa kati ya kanda za mazingira ya wanyama zilizo kubwa katika Afrika” hukutanika katika sehemu ya kaskazini mwa Mbuga ya Kruger. “Hapa,” kitabu hicho chaendelea kusema, “sehemu zenye maji-maji zakutana na vichaka vya nchi kame, misitu yakutana na nyanda tambarare, miamba yakutana na mchanga wenye kina kirefu.” Karibu kilometa za mraba 400 za eneo hili la pekee zimetengwa kando ziwe eneo la kutembelea la Nyalaland. Hakuna wanadamu wengine wowote wanaoishi hapo, ila tu wafanyakazi wachache wa kambi, na hakuna barabara za watalii.

Kobus anajaribu kula chakula chake cha jioni huku akijibu maswali yetu mengi. Ana digri ya elimu ya Sayansi kutoka Chuo Kikuu cha Pretoria, alikosomea usimamizi wa mambo ya wanyama wa porini, zuolojia, na botania. Upesi tunaona kwamba ujuzi wake si wa kimasomo tu.

“Je! umepata kukutana na wanyama wakali katika hali za kuhatarisha?”

“Wamejaribu kunishambulia mara kadhaa,” ajibu Kobus, “lakini si na mnyama aliyetaka kweli kuniua.”

“Simba anaposhambulia, unajuaje kwamba anajaribu tu?”

“Anapotua karibu meta nne au tano kutoka mahali ulipo na kuacha kukimbia,” yeye ajibu.

Walinzi wa mbuga kama Kobus wamezoezwa kubaki wakiwa watulivu wakati mnyama anaposhambulia. Yeye aeleza hivi: “Wanakuambia uthubutu, nawe ujaribu mnyama huyo. Hali halisi inaweza kuwa simba-jike mwenye watoto au wa kiume anayejamiiana. Kwa kuja kukushambulia, mnyama huyo anakuambia, ‘Unavuka mpaka—unaingilia faragha yangu, na ni afadhali uende zako.’ Wakati uo huo, nimetayarisha bunduki yangu na niko tayari kumkabili. Nyakati zote mimi huchora mstari wa kuwazia. Akivuka mstari huo, basi ni lazima nifyatue risasi. Lakini kwa yale niliyojionea, wao husimama kabla ya hapo, na sijalazimika kumwua mnyama yeyote katika sehemu hii ya kutembea.”

Kwa wazi, Kobus hawindi ili ahifadhi sehemu fulani za wanyama kuwa kiku-mbusho. Twachangamshwa na staha yake kwa wanyama wa pori. Lakini kunakuwa usiku mno, na ni lazima tuamke asubuhi kesho. Baada ya kuagana, twaenda kulala katika nyumba ndogo nne zenye kuezekwa nyasi zenye umbo-A na zilizojengwa juu ya milonjo.

Kufikia 10:45 alfajiri, Wilson, mpishi wa kambi, atuamsha. Baada ya kufurahia kiamsha-kinywa twaenda kwa gari hadi mahali ambapo matembezi yetu yataanzia. Kwa shukrani twaangalia anga lenye mawingu yaliyotanda. Katika siku za kiangazi zisizo na mawingu, halijoto yaweza kufikia sentigredi 40.

Kwa baadhi yetu, hili ni ono jipya kabisa kwetu. Kwanza twawa na hisi ya wasiwasi kidogo wa labda kukanyaga nyoka au kushambuliwa na mnyama mkali. Lakini upesi badala ya woga huo twawa na hisia ya kustaajabia sehemu tambarare kubwa-kubwa zilizofunikwa miti mibichi hadi upeo wa macho. Vichaka vimejaa nyimbo za ndege na kelele za wadudu. Ah, inafurahisha kama nini kupumua hewa safi, isiyochafuliwa!

Pindi kwa pindi, Kobus na msaidizi wake, Ellion Nkuna, wasimama kutuonyesha kitu chenye kupendeza, kama vile msafara wa siafu au nyayo za mnyama. Tunafikia mti ambao umezingirwa katika shina na kichuguu. “Huu,” aeleza Kobus, “ni mnyala-beri. Mara nyingi unaiona miti hiyo ikiota kwenye vichuguu. Vitendo vya mchwa hurutubisha udongo na kunufaisha mti huu.”

Baada ya kutembea kwa muda wa saa moja, twapita mti ulioangushwa na ndovu. “Ingawa huu ni mti mgumu,” aeleza Kobus, “sio kitu mbele ya ndovu. Yeye huuangusha chini kirahisi. Wao hufanya hivyo mara kwa mara. Huenda ikaonekana kuwa wanafanya vibaya, lakini kuna mafaa vilevile. Katika miezi michache, mti huu labda utakuwa umekufa. Na unapooza, unaandaa chakula kwa vijidudu vidogo na kuingiza madini katika udongo.”

“Nafikiri,” aongeza mshiriki mmoja wa msafara wetu, “idadi ya ndovu isipodhibitiwa, eneo kama hili lingegeuka na kuwa sehemu ya majani pekee.”

“Hiyo ni kweli,” ajibu Kobus. “Hakungebaki hata mti mmoja. Katika Mbuga ya Kruger, tunajaribu kudumisha idadi ya ndovu kuwa karibu 7,500, ambayo, kulingana na ujuzi wetu wa sasa, ndiyo idadi ambayo Kruger inaweza kutegemeza.”

Kisha mtu fulani aona nyayo zilizo wazi za mnyama katika mchanga. Bila kufikiri nikapaaza sauti: “Ni lazima ziwe za chui!”

“La,” asema Kobus, “ni za fisi. Ona kwamba ni nyayo ambazo hazina umbo lenye ulingano, au urefu ni mkubwa kuliko upana. Vilevile unaweza kuona alama za makucha kwa sababu fisi ni mnyama kama mbwa. Hawezi kurudisha makucha yake ndani. Sasa ukilinganisha hizi na nyayo za jamii ya paka, kama chui au simba, ni rahisi sana kutofautisha. Nyayo za jamii ya paka zina umbo lenye ulingano mzuri, yaani ni duara na hazina alama za makucha kwa sababu wanyama hao hurudisha makucha yao ndani. Pia, ukiangalia kisigino, kuna migawanyiko miwili katika nyayo za fisi, ilhali jamii ya paka wana kisigino kikubwa chenye migawanyiko mitatu.”

Kufikia sasa tunaanza kuhisi njaa. Kwa hiyo tunaketi katika kichuguu kikubwa na kufurahia chakula chepesi ambacho sisi wanaume tulikuwa tumebeba katika mifuko ya migongoni. Baadaye, twatembea kuelekea kilima ambacho Kobus atuhimiza tupande. Tukiwa tumepanda nusu, twapumzika katika miamba fulani na kufurahia mwono mzuri ajabu wa vichaka na miti yenye kusongamana sana iliyosambaa kuvuka tambarare hiyo kubwa sana kufikia mpangilio wa milima katika upeo wa macho ulio mbali. Kobus atukumbusha kwamba yale tunayoona sasa ni asili kabisa, hayajaguswa na binadamu wa karne ya 20. Lakini kwenye upeo wa kilima hicho, tunashangaa kupata njia inayoonekana kuwa imetembelewa sana na binadamu.

“Hiyo ni njia ya ndovu,” aonelea Kobus.

Lakini, ninajiuliza kwamba anawezaje kuwa na hakika hivyo kwamba ni wanyama, wala si wanadamu, ndio walioifanya njia hiyo. Mawazo hayo yanapokuwa yakipitia akilini mwangu, Ellion mwenye macho ya kuona vitu haraka apata uthibitisho. Ainua pembe ya ndovu iliyochakaa.

“Labda hii imekaa miongo mingi ya miaka,” asema Kobus.

“Naam,” nikakiri, “hiyo inaonekana kuwa uthibitisho kwamba muda mrefu umepita tangu binadamu yeyote apitie hapa, kwa sababu mwanadamu hawezi kuacha kitu chenye thamani kama hiki.” Ellion aweka pembe hiyo kwenye mfuko wake wa mgongoni ili aipeleke kwa wenye mamlaka wa Mbuga ya Kruger.

Wakati umepita haraka sana, na ni karibu adhuhuri tunapoona gari aina ya Land-Rover. Tumetembea kwa mzingo kwa karibu kilometa kumi na moja. Tunaporudi kwenye kambi, twakuta kwamba Wilson ametayarisha chakula cha mchana, ambacho twakila kwa shukrani. Baada ya usingizi mfupi wa mchana twaondoka kwenda matembezi ya jioni kandokando ya Mto Luvuvhu.

Mandhari ni nzuri sana hapa, kukiwa na vichaka vifupi vya kijani-kibichi vilivyosongamana na miti mikubwa, kama mforsadi-tini ukiwa na maumbo yao yenye kustaajabisha yaliyopinda-pinda. Baada ya kujifunza majina na tabia za miti mbalimbali, twapita kikundi cha nyani kinachotutazama kwa hadhari kutoka nyuma ya vichaka. Kisha twaketi chini kwenye mwamba unaoelekea huo mto.

Tunaposikiliza maji yanayopita kwa kasi, Ellion atuonyesha nyala wanne wa kike wanaokaribia mto nyuma yetu. Kwa uzuri, upepo unavuma kuelekea nyuma yetu, kwa hiyo hawanusi harufu yetu. Tunatazama swala hao wazuri wanapotua kila mara ili wale majani ya kichaka. Baada ya karibu dakika kumi, mmoja wao atuona na kutoa mbweko wa kuonya. Wote watoroka mara hiyo.

Wakati uo huo, baadhi ya nyani hao wenye udadisi wamesogelea karibu, nasi tunasikia kilio kinachofanana na kiyowe chenye kutiwa chumvi cha mtoto. Labda mama yake anamchapa kwa ajili ya kutukaribia mno. Tunawazia kuwa anasema hivi: ‘Usijaribu kwenda karibu na wanadamu hao tena!’

Giza laingia, kwa hiyo ni lazima turudi kambini. Baada ya kurudi, mvua yaanza kunyea, kwa hiyo twala chakula cha jioni katika kibanda chenye kupendeza kilichoezekwa nyasi na chenye pande zilizo wazi. Tunasikiliza pata-pata yenye upole ya mvua ikikatishwa na sauti za vichaka. Wanyama-mwitu wako karibu, na mazungumzo yarudia tena simba. Tunauliza Kobus ni mara ngapi amekabiliana uso kwa uso na simba akiwa anatembea katika sehemu hiyo.

“Karibu mara 70,” yeye ajibu.

“Mnapokutana, kwa kawaida nini hutokea?”

“Jambo ambalo hutokea,” ajibu Kobus, “ni kwamba sisi sote hushtuka. Unatembea mahali fulani, kama tulivyofanya leo, ukitarajia kuona wanyama wa kawaida, wakati kwa ghafula, meta chache mbele yako, kuna kikundi cha simba wanaopumzika katika kivuli. Wanakutazama, na unaona macho yao yakipanuka kana kwamba hawawezi kuamini wanachoona. Macho yangu,” acheka Kobus, “labda yanapanuka pia. Kisha mimi huwaambia watembeaji: ‘Kujeni haraka! mwone!’ Kisha, unasikia mingurumo miwili au mitatu, na kisha wanaenda zao. Wao wanatuogopa zaidi ya jinsi tunavyowaogopa.

“Nyakati nyingine, unakutana na simba-majike wakiwa na watoto, na hali inakuwa tofauti kabisa. Badala ya mngurumo, unapewa mguno mrefu wenye kutisha, na unaona mkia wake ukicheza-cheza huku na huku. Ninakuwa nimetayarisha bunduki yangu na kuambia watembeaji wasimame tuli. Kisha tunarudi nyuma kwa utaratibu, tukiwa tumekaza macho yetu juu ya mnyama huyo na bila kugeuza migongo yetu.”

Asubuhi inayofuata, twatembea kupitia Mashikiripoort zuri—genge jembamba lenye miamba yenye kuinuka juu kwenye kila upande. Hatimaye twafikia mlima wenye pango. Kabla ya kupanda juu, Ellion arusha jiwe kubwa, linalotokeza kelele nyingi. “Nilirusha jiwe hilo,” akaeleza baadaye, “ikitukia kulikuwa kuna simba au wanyama wengine hatari. Hilo huwapa nafasi ya kutoroka.”

“Kama sivyo,” aongezea Kobus, “ungeweza kuzuia mnyama hatari, na basi utakuwa na matatizo.” Tunapofikia pango, hapo kwenye mmoja wa kuta za miamba kuna mchoro uliochorwa na kabila la Bushman. Ni twiga ambaye Kobus asema yeweza kuwa alichorwa zaidi ya miaka mia mbili iliyopita.

Wakati wa matembezi hayo, twaona pia vikundi vya twiga, nyumbu, na pundamilia. Ukiwa katika gari, mara nyingi unaweza kusogea karibu na wanyama hao, lakini ukiwa kwa miguu, wakati upepo unavuma kuwaelekea, wao kwa kawaida hunusa harufu yako na kukimbia kabla hujafika karibu. Twasikiliza kundi ambalo liko mbali la pundamilia likikimbilia mbali, nami nakumbuka maneno yaliyo kweli ambayo yamo katika Biblia: “Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu.”—Mwanzo 9:2.

Kufikia wakati huu tunastahi uwezo wa Ellion wa kuwaona haraka wanyama na kutambua nyayo zao. Yeye ni wa taifa la Tsonga—watu wanaojulikana kwa ustadi wao wa kufuata wanyama kwa nyayo zao. Tunamwuliza juu ya jambo hilo.

“Nilianza kujifunza nilipokuwa mvulana mdogo nikichunga ng’ombe,” yeye aelezea.

Baadaye, wakati wa matembezi yetu ya alasiri, ni Ellion anayetutahadharisha tusikie sauti ya viboko. Upesi twafikia mahali juu ya mto. Na kwa kweli, mle katika maji mna kundi la viboko. Wengi huona kiboko kuwa mnyama aliye hatari zaidi katika Afrika. Lakini tumejifunza kutumaini walinzi wetu wa mbuga waliozoezwa vizuri. Twaketi kimya katika ukingo wa mto na kutazama. Pindi kwa pindi, kichwa cha kiboko chapotea ndani ya maji. Na wakati tu tunapofikiria kwamba ameenda, ainuka kwa ghafula, akitoa pumzi na kupuliza maji kutoka kwenye mianzi yake ya pua iliyo mikubwa. Kisha, kwa pamoja watoa mikoromo yao isiyoweza kusahaulika yenye sauti kubwa na kufungua vinywa vyao vikubwa sana.

Baada ya kuvutiwa na michezo hiyo kwa karibu muda wa nusu saa, twaondoka bila kutaka kwa sababu giza linaanza kuingia. Jioni hiyo, tukiwa tumeketi kuzunguka moto wa kambi, twarudia maono yenye kujenga ya siku mbili zilizopita. Twafurahia kujua kwamba dunia ingali ina sehemu nzuri kama hii ambazo hazijaharibiwa. Kwa habari ya wakati ujao, twafarijika na ahadi ya Biblia kwamba, kabla ya kuchelewa mno, Mungu ataingilia mambo na kuokoa dunia isiharibiwe. Kisha, si Nyalaland tu bali dunia nzima itanufaika na ahadi hakika ya Mungu: “Tazama, nayafanya yote kuwa mapya.”—Ufunuo 11:18; 21:3-5; Isaya 35:5-7.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki