Mitio ya Damu Mishipani na Msongo wa Madaktari
Watu wengi leo, pamoja na baadhi ya madaktari, wanakataa mitio ya damu mishipani. Kwa sababu zipi? Siyo kwa sababu za kidini, kama Mashahidi wa Yehova, lakini kwa sababu za kitiba. Kwa nini iko hivyo? Kwa sababu ya hatari zinazohusika (kama vile kuwasha kwa ini, UKIMWI, na kinga ya mwili iliyodhoofika) ambazo hupatikana daima katika damu ya mtu mwingine. Walakini, katika visa vingi ambapo damu imependekezwa, marafiki na wafanyakazi wa hospitali husonga mgonjwa ili akubali kutiwa damu. Lakini mara nyingi kuna aina nyingine ya msongo inayotenda—msongo wa madaktari kwa madaktari wenzao wanaohudumia.
Katika toleo lalo la Julai 25, 1990, The Journal of the American Medical Association liliripoti hivi: “Ithibati inaonyesha kwamba bidhaa za damu, kama na vifaa vingine vya kitiba, mara nyingi hutumiwa isivyofaa. . . Sisi tulifanya uchunguzi wa ana kwa ana na madaktari wa upasuaji, madaktari wa kurekebisha mifupa, na madaktari nusukaputi wapatao 122 katika hospitali tatu ili kufahamu uvutano wa mambo kadha ya kitiba na yasiyo ya kitiba juu ya uamuzi wa kutia damu mishipani. Tulipata upungufu mkubwa wa maarifa ya madaktari juu ya hatari za kutia damu mishipani na dalili zayo.”
Ni nini kinachomaanishwa na “mambo yasiyo ya kitiba”? Ripoti hiyo inajibu kwa sehemu: “Maamuzi ya madaktari huathiriwa na madaktari wenzao kupitia njia za kiufundi na kijamii. Uvutano wa madaktari huhisiwa zaidi wakati madaktari wanapofanya kazi pamoja. . . Katika hali kama hizo, matendo nyakati nyingine huchochewa na matazamio ya madaktari wa cheo cha juu au wenye uvutano, tamaa ya kutaka kufuatana na kawaida za kikundi, au ya kutaka kuepuka uchambuzi.”
Makala hiyo ilieleza kwamba “hata hivyo, ni asilimia 10 peke yao, waliosema kwamba walikuwa wametia damu mishipani ambayo haikuhitajika ili kuridhisha wenzao mara moja kwa mwezi au zaidi. . . Asilimia 61 kamili ya wakazi walieleza kwamba kwa sababu daktari mwenye cheo kikubwa kuliko wao alikuwa amedokeza kwamba wafanye hivyo, angalau mara moja kwa mwezi, walitia damu mishipani ambayo wao walifikiri haikuhitajika.” Mbali na aina hii ya kusongwa na wafanyakazi wenzi, ni jambo gani jingine linaloweza kumwongoza daktari kuagiza mtio wa damu mishipani?
“Baadhi ya madaktari huelekea kutoa matibabu kwa sababu ya kupendelea kufanya makosa ya kutenda kuliko kufanya makosa ya kutotenda.” Mtaalamu mmoja wa kitiba “alidokeza kwamba lile agizo la kawaida Primum non nocere (‘Kwanza usidhuru’) mara nyingi huenda likasukumwa kando kwa kupendelea agizo la ‘Kwanza fanya jambo.’ Shauku kama hiyo ya kutenda huenda ikawa ni jambo moja katika kueleza zoea lisilofaa la kutia damu mishipani.”
Je, wagonjwa huwa wanafahamu hatari za kutiwa damu mishipani? “Kwa wastani, madaktari walisema kwamba kati ya wagonjwa ambao wao huwaagizia kutiwa mishipani damu ya chembe nyekundu, nusu yao husema wanahangaikia hatari za kutiwa damu mishipani.”
Kwa kweli, hilo laonyesha kwamba kwa mambo yanayohusiana na kutiwa damu mishipani, daktari mwenye elimu na mgonjwa mwenye elimu wamo katika hali njema zaidi kuepuka hatari zisizohitajiwa. Mkristo mwenye elimu ana ulinzi ulio bora hata zaidi—amri za Yehova dhidi ya utumizi mbaya wa damu.—Mwanzo 9:3, 4; Mambo ya Walawi 17:13-16; Matendo 15:19, 20, 28, 29.