Kuutazama Ulimwengu
Matangazo ya Sigareti Yapigwa Marufuku
Kampuni za tumbaku katika Ufaransa zimekuwa zikiepa sheria ya kutotangaza sigareti kwa kutumia majina na mitajo ya kampuni zao kwa kutangaza vitu visivyo vya tumbako. Matangazo hayo yanashirikisha uvutaji pamoja na visa vinavyoonyesha vituko vya ujasiri, michezo, na starehe. Serikali ya Ufaransa imeweka sheria mpya ambayo itapiga marufuku utangazaji wa aina yoyote ya sigareti kuanzia Januari 1, 1993. Sheria hiyo mpya itakataza aina zote za ujulisho wa njia isiyo waziwazi, hata pia udhamini wa michezo kutoka kwa kampuni za sigareti. Maofisa wa serikali wananukuu tarakimu zinazoonyesha kwamba uvutaji unasababisha vifo vya mapema zaidi ya 60,000 kila mwaka katika Ufaransa. Ulimwenguni pote, karibu watu milioni tatu hufa kila mwaka kutokana na ugonjwa unaoletwa na uvutaji.
Kileo na Kazi
Chama mashuhuri cha kutetea wafanyakazi Ujerumani chakadiria kwamba “mmoja kati ya wafanyakazi saba katika Jamhuri ya Muungano ya Ujeruamni ana shida na kileo,” laripoti Süddeutsche Zeitung. Hii hugharimu jamii ya Ujerumani kati ya marki (pesa za Ujerumani) milioni elfu 50 na milioni elfu 120 kila mwaka. Kwa wastani, katika 1990 Wajerumani walikunywa kileo mara nne ya kile walichokunywa katika 1950. Mwanachama wa halmashauri ya chama cha waanya kazi alitambua kwamba kileo kimekuwa kama dawa ya kulevya “ambayo kwayo watu hujitia ganzi ili waweze kukabili kazi yao na mazingira ya kazi.”
“Pafu la Wanadamu”
Shirika jipya la kitaifa linalojulikana kuwa Parlamento Amazónico (Bunge la Amazon) limeundwa karibuni katika Amerika Kusini. Wanachama ni maofisa wa serikali na wanasayansi kutoka Bolivia, Brazili, Kolombia, Ekwedori, Guyana, Peru, Suriname, na Venezuela. Kusudi la shirika hili ni kutia moyo usitawishaji wa kiakili zaidi wa eneo la Amazon, ambayo ina ukubwa wa kilometa za mraba milioni 4.4 na ndiyo makao ya watu milioni 150 katika nchi nane. Gazeti la Argentina La Nación liliripoti kwamba Bunge la Amazon liliita eneo la Amazon “pafu la wanadamu.” Kuhusu kilometa za mraba 240,000 wa msitu ulioharibiwa miaka ya karibuni, wasemaji wa shirika walionyesha kwamba “ingawa huenda ikawa ni biashara nzuri, pesa hizo zitakuwa hazina maana ikiwa sayari haitakaliwa, ambalo litatukia karibuni ikiwa uharibifu huu hautakomeshwa.”