Dondoro Aliyetoroka
Na mleta habari za Amkeni! katika Afrika Kusini.
KWA silika, dondoro, paa mdogo wa Afrika, huweka mfano wa ajabu katika usafi. “Tabia moja ya dondoro,” aeleza Profesa John Skinner katika kitabu South African Animals in the Wild, “ni kwamba kabla ya kwenda choo au kukojoa, kwanza yeye huweka mahali pawe wazi kwa kwato zake za mbele kisha, baadaye, hufunika choo kwa kukwaruza udongo na kufunika mahali hapo.” Naam, kiumbe huyo mdogo hufanya zaidi ya ile sheria waliyopewa askari Waisraeli. (Kumbukumbu la Torati 5:1; 23:13, 14) Yeye hata hufunika mkojo wake.
Tabia za hali ya juu za kwenda choo za dondoro hufanana na sura yake ya kupendeza. “Kwangu mimi dondoro sikuzote amekuwa mmojawapo paa wa Afrika mwenye uzuri na mwenye kupendeka zaidi,” akaandika Laurens van der Post. Katika kitabu chake The Heart of the Hunter, van der Post asimulia jinsi alivyojaribu kupiga risasi dondoro mmoja kwa ajili ya kikundi cha Bushmen wenye njaa katika Jangwa la Kalahari. “Masikio yake mororo,” akaandika mvumbuzi huyo, “yalielekea upande wangu, macho yake makubwa ya zambarau yakiwa wazi kabisa, bila hofu yoyote na kung’aa kwa mshangao tu wa kuona kitu kigeni hivyo katika sehemu hiyo ya mbali. . . . Nilipiga risasi upesi kabla hajashtuliwa au kabla sijashawishiwa nisimuue kwa uanana wake. Nisingefikiria kuwa yawezekana kukosa shabaha kwa ukaribu hivyo. Na bado, niliikosa. Mfyatuko huo ulifanya tu paa huyo mdogo atikise kwa nguvu kichwa chake chenye kupendeza ili kuondoa mlio wa mfyatuko wa bunduki yangu nzito masikioni mwake.”
Baada ya mifyatuo mingine michache, paa huyo mdogo aliamua kwamba ushirika wa mwanadamu ni hatari na akatoroka. Ingawa hawakupata mlo waliohitaji, wale Bushmen wenye njaa wenzi wa van der Post walifurahi. Kwa nini? Bushmen hustahi sana tabia za dondoro, na paa huyo alitenda vile walivyotazamia atende. “Muda wote wa siku hiyo ndefu yenye joto,” aongeza van der Post, “akilini mwangu niliona yule paa mdogo mwanana akisimama bila wasiwasi kujapokuwa mfyatuo baada ya mfyatuo wa bunduki yangu.”