Bunduki—Njia ya Kifo
“WAO huwa na wazo hili lenye makosa,” akasema ofisa mmoja mashuhuri wa polisi, “kwamba wataelekezea mtu bunduki na kudhibiti hali vizuri na mambo yasipoenda jinsi hiyo, wao husita, kama vile maofisa wengi wa polisi husita kwa kipande cha sekunde, nao hulipia hayo kwa maisha zao.” Pia kuna maoni haya kutoka kwa kamishna mwenye sifa wa usalama wa umma katika United States: “Watu wengi hawaelewi uhakika wa kwamba kuwa na bunduki ya mkononi humaanisha kuwa tayari kuishi na madhara ya kuua binadamu mwingine. Usipofyatua risasi kikweli na mhalifu akufyatulie wewe, huwa ni hatari zaidi kuwa na silaha kuliko kutokuwa nayo kamwe.”
Mwisho, kuna jambo hili: “Hata uwazio mdogo tu wapasa kutuambia kwamba silaha hii ya mwundaji maarufu itaongoza kwenye matata mengi zaidi, si machache zaidi,” akaandika ripota mmoja mwanamke—mshiriki wa familia ya polisi, yeye mwenyewe akiwa ni mlenga shabaha stadi. “Je! wanawake wanaonunua bunduki za ‘kuvutia’ wamewahi kukabili wazo la kama ni jambo maridadi bongo za watu kulipushwa? Hilo si tokeo lenye kuvutia. Je! wamepata kuona mwanamume mwenye uso uliofyatuliwa ukang’oka?” Au, mwanamke huyo auliza, “je! ungeweza kulenga shabaha moyoni?”
Wewe ungeweza kuchomoa bunduki yako kwa haraka kadiri gani ukikabiliwa ghafula na mshambulizi? Fikiria yaliyompata mwanamke huyo mwenyewe: “Nilipoviziwa nyuma—na mzoelevu mkichaa mwenye kisu cha machinjo—kabla sijaweza kumwona au kumsikia mshambulizi wangu chuma hicho kilikuwa tayari kooni pangu. Kama ningalikuwa nimetafuta bunduki, nani angalimaliza mambo kabla ya mwingine?” Halafu mwanamke huyo aongezea hivi: “Mimi singeota juu ya kuweka bunduki kwa ulinzi wa kibinafsi. Hili si jambo la adili; ni la kutenda mambo kihalisi.”
Sasa fikiria mambo mengi ya hakika. Katika “mitupiano risasi ambayo kwa kawaida hutukia mara chache kati ya wenye nyumba na wavunja nyumba, ingeweza kwa urahisi kuwa kwamba mvunja nyumba ndiye huthibitika kuwa mstadi zaidi katika kutumia bunduki yake na mwenye nyumba ndiye mwishowe hujikuta katika nyumba ya maiti,” likaripoti gazeti Time la Februari 6, 1989. Hata bunduki iwe ni kipingamizi cha jinsi gani katika kuzuia kitendo cha uhalifu, uzuizi wayo huwa si kitu ukilinganishwa na madhara mengine. Kwa kielelezo, fikiria visa vya kujiua. Katika United States pekee, katika kipindi kimoja cha miezi 12, watu zaidi ya 18,000 walijipiga risasi wakafa.
Haiwezi kujulikana ni vingapi vya vitendo hivyo vya kushtukia tu ambavyo huenda ikawa visingalifanyika kama kusingalikuwa na bunduki katika kibeti au kabati la mavazi. Hata hivyo, kwa uhakika kule kupatikana kwa utayari kulizuia mihanga fulani wasiwe na wakati wa kutosha kufikiri kiakili na labda waokoe maisha zao. Ongeza hesabu ya visa vya kujiua kwa bunduki katika United States kwenye visa vya sehemu nyinginezo za ulimwengu na bila shaka jumla ingekuwa ya kushtusha kweli kweli.
Gazeti Time la Julai 17, 1989, liliripoti kwamba katika juma la kwanza la Mei 1989, watu 464 walipigwa risasi wakafa katika United States pekee. “Mwaka huu wengine zaidi ya 30,000 watashiriki balaa lao,” likasema Time. Gazeti hilo liliripoti kwamba “Waamerika zaidi hufa kutokana na risasi za bunduki kila miaka miwili kuliko wale ambao wameuawa na UKIMWI kufikia sasa. Vivyo hivyo, bunduki huua uhai mwingi zaidi wa Waamerika katika miaka miwili kuliko ule uliouawa na Vita yote ya Viet Nam.”
Wazazi walio na bunduki ni lazima wahimili daraka la watoto wao ambao huzitumia kukomesha uhai wao wenyewe au uhai wa wengine. “Ongezeko la visa vya kujiua kwa vijana katika 1988,” ikaandika karatasi-habari moja, “kwa sehemu laweza kuhusianishwa na upatikanaji rahisi zaidi wa bunduki kwa kadiri wenye nyumba wengi zaidi warundikavyo silaha ili kulinda makao yao, polisi wakasema. . . . Ikiwa wewe una silaha nyumbani, kuna uwezekano wa kwamba mtoto ataifikia siku moja.” “Mwaka uliopita [1988], watoto zaidi ya 3,000 waliwapiga risasi watoto wengine,” ndivyo ilivyoripoti habari moja ya televisheni ya United States katika Juni 1989.
Wazazi, je! mwajua zilipo bunduki zenu? Mzazi mmoja alijua, lakini mwanaye wa miaka kumi alijua pia. “Alitia risasi katika bunduki yenye nguvu nyingi ya mawindo ya baba yake,” likaripoti New York Times la Agosti 26, 1989, “na kumfyatua hadi kifo msichana aliyekuwa amejigamba kuwa bora kuliko yeye kwenye michezo ya vidio.” Je! wewe wajua kilichomo katika sanduku la chakula la mtoto wako zaidi ya sandwichi (mikate) na biskuti wakati umwachapo aende shuleni? Je! ungeamini kwamba ingeweza kuwa ni bunduki yako? Wazazi wa mtoto wa shule ya nasari mwenye umri wa miaka mitano walikuwa na fikira gani wakati maofisa wa shule walipowajulisha kwamba walikuwa wamemnyang’anya mwana wao bastola yenye risasi ya ukubwa wa .25 katika sebule la chakula lililosongamana wanafunzi, huku mamia ya wanafunzi hao wakila sandwichi, maziwa, na biskuti zao?
Baadaye katika 1989, mwanafunzi wa darasa la kwanza mwenye umri wa miaka sita alishikwa akionyesha bastola yenye risasi. Mwezi uo huo mtoto wa miaka 12 alikamatwa kwa kwenda shuleni na bastola yenye risasi. Yote hayo katika wilaya ile ile ya shule. Katika Florida, mwanafunzi mmoja hakuwa na njia ya kuponyoka msiba wa bunduki yenye risasi iliyokuwa mikononi mwa mtoto. Alipigwa risasi mgongoni wakati msichana wa miaka 11 alipoifyatua kiaksidenti bunduki aliyokuwa ameleta shuleni kuonyesha rafiki zake.
“Watoto wetu wenye miaka sita huenda nyumbani na karibu wote wajua kwamba nyumbani mwao mna bunduki,” akasema mkuu mmoja wa shule. “Wengi wao wameona tokeo la bunduki,” akasema mwalimu mmoja wa darasa la tatu. “Labda baba, mjomba au ndugu hayumo tena nyumbani mwao kwa sababu ya bunduki,” akasema. Mifumo fulani ya shule hata imeuona uhitaji wa kuweka vinasa metali ili kugundua bunduki ziletwazo na wanafunzi walio wachanga sana, achia mbali wale wenye umri mkubwa zaidi! Je! wazazi hawapaswi kuhimili daraka kwa vitendo vya watoto wao, hasa wazazi ambao huona yafaa kuwa na bunduki katika nyumba zao ambamo watoto waweza kuzipata?
Huenda wazazi wakajifariji ya kwamba bunduki zao zimefichwa mahali ambapo watoto wao au wengine hawawezi kuzipata. Hata hivyo, kwa tokeo baya watoto ambao wamekufa wamethibitisha kwamba wazazi wao hawakuzificha. Pia, yafikirie mambo ya wazi. “Huwezi kufaulu njia zote mbili,” akasema mkuu mmoja wa polisi. “Ukiilinda salama kweli kweli bunduki yako ili watu wasio na hatia katika nyumba yako, watoto wako au wageni au mtu mwingineye, wasiweze kuumizwa nayo, basi [wewe] hutaweza kuifikia bunduki hiyo kwa ajili ya dharura ile ambayo ndiyo kwanza ilikufanya uinunue.”
Polisi wakadiria kwamba bunduki ya nyumbani ikipata kuja kutumiwa wakati wowote, “itaelekea mara sita zaidi kufyatushwa kwenye mshiriki wa familia au rafiki kuliko kwenye mvamizi,” likaripoti gazeti Time. “Mke au mama hufikiri amemsikia mvunja nyumba na kuishia akimfyatua risasi mume au mwana anayekuja nyumbani kwa kuchelewa,” akasema kamishna mmoja wa usalama wa umma. ‘Basi, je! watu wapaswa kulindaje nyumba zao?’ aliulizwa. “Labda njia bora kabisa ya kujilinda ni kujasiria kupoteza mali yako badala ya uhai wako. Wanyang’anyi na wavunja nyumba walio wengi huwa pale kuiba, si kuua. Vifo vilivyo vingi vya kutumia bunduki au bastola katika nyumba za watu hufanywa kwa kutumia bunduki ya mwenye nyumba. Vyovyote ilivyo, wakaaji wa mjini wapaswa kujaribu kuongezea ulinzi kwa kufanyiza vikundi vya ‘ulinzi’ dhidi ya uhalifu.” Na, mwisho, ni lazima wenye bunduki wajiulize kama wana nia ya kukomesha uhai wa binadamu mwingine ili walinde vilivyomo katika kibeti au pochi au vitu vichache vyenye thamani nyumbani.
Ikiwa wewe ni mwenye hekima, hutamkinza mtu atishaye uhai wako kwa vitu vyako vyenye thamani. Uhai wako una bei kuliko vitu hivyo.