Bunduki—Si za Wanaume Tu
KATIKA ulimwengu wa utangazaji bidhaa, umbo la mwanamume mbabe aliyesimama kwa kushika bunduki limetumiwa kuuza vitu vingi. Ni vitu vya aina zote—tumbako, motakaa, nguo, bunduki na bastola na kadhaa wa kadhaa, ambavyo ni akili ya mtangaza-bidhaa tu iwezayo kuviwekea kikomo.
Katika United States hasa, wanaume wameonyeshwa kuwa wasioweza kutenganishwa na bunduki zao. Katika nyanja za mji, sanamu zimesimamishwa za mashujaa washindi walio na bunduki mikononi mwao ama kiunoni. Hata bila maneno ya kueleza, picha zinazoonyesha ile enzi ya uhayawani wa Magharibi hutambulishwa upesi na ile bunduki ya mitutu sita yenye kuning’inia chini kwenye ukanda ulioangikwa kando ya kiuno cha mwanamume. Sinema nyingi zimefanywa zikiwa na neno “bunduki” katika vichwa vyazo. Maonyesho ya televisheni na vitamasha katika vyumba vya maonyesho ya sinema huwa na mvumo wa risasi zenye kupigwa haraka-haraka—jamaa wazuri na jamaa wabaya wakitupiana risasi katika kila hali na mahali panapowazika. Wanaume wanyonge wakifanywa mibabe kwa kushika bunduki ya mkononi au ya kawaida, kukiwa na tamasha za watu waliolala kwenye nyayo zao wakiwa wafu ili kuonyesha jinsi mambo huwa kihalisi.
Lakini sasa wanawake zaidi wanahusika na bunduki. Muda wa miaka 20 iliyopita, televisheni zimevuvumuka majasusi wanawake na wapelelezi waliojibanza wakitupiana risasi na watu wabaya wakiwashinda kwa kuwapiga shabaha kwa njia hatari zaidi na bunduki zenye nguvu zaidi.
Wao wanamiminika kwa wingi kwenye sehemu za kulenga shabaha za bastola na bunduki, wakifyatua-fyatua risasi katika shabaha zinazofanana na wanaume halisi, wakitoboa matundu katikati ya macho yao kwa risasi.
Kwa hiyo haipasi kukushangaza kujifunza kwamba bunduki za mkononi zilizoundwa kwa ajili ya wanawake hasa ziko tayari sokoni na zinanunuliwa sana. “Mabibi, nyinyi hamngetumia marashi ya mwanamume,” akaandika mwanamke ripota mmoja, “hivyo basi mbona mtumie bastola ya mwanamume? Mwataka bastola nyepesi, isiyo na ncha za kushika kucha zenu, bastola maridadi ambayo bado itafyatuka kwa kishindo. Labda mwataka aina ya ‘LadySmith yenye ukubwa wa .38’ . . . iliyo ya rangi nyangavu ya buluu, au rangi asilia isiyong’ara, pamoja na chaguo lenu la marefu ya mitutu.” Mstadi mmoja alitamka maoni yake juu ya bunduki ambazo wanawake hutaka: “Mwanamke hutaka bunduki ionekane ya kuvutia. Hutaka iwe kitu chenye sura nzuri ambacho yeye hukitia katika kibeti chake. Hataki igongane na kikasha chake cha kuwekea wanja au kioo . . . Wanawake wengi hupenda kufanya rangi za vitu vyao ziratibike vizuri na kupatana. Hawataki vionekane viovu au vya ukorofi . . . Mwanamke anainunua kwa ulinzi, lakini, wakati ule ule, hataki iwe na sura mbaya.”
Baadhi ya bunduki za mkononi ambazo zimekusudiwa kwa ajili ya bibi mwenye madaha ni zile zenye nafasi ya marisau matano ya mtutu wenye ukubwa wa .38 nazo hutolewa kwa chaguo la mitutu ya marefu mawili—inchi mbili na inchi tatu—ili zitoshee vizuri katika kibeti. Baadhi yazo huja zikiwa na vishikio vya mbao laini zenye vistari-stari vya kuvutia, na nyingine huenda zikatiliwa vishikio vya rangi nyepesi za kuvutia. “Huwa na sura nzuri sana,” akasema mwanamke mmoja, “tena ningefikiri huwa za kiasi cha kushikika kwa urahisi.” Halafu, pia, kuna mavumbuo mapya ya vibeti vyenye sehemu za ndani zilizofanyizwa hasa kwa ajili ya bunduki ya mkononi ya mabibi. “Mwanamke mwenye bunduki ya mkononi isiyo na kibeti maalumu anajitafutia matata tu,” akasema mwanamke mmoja. “Mwishowe utajikuta ukiwa na vipande vya biskuti na peremende katika mtutu wa bunduki, au tumbako, ikiwa wewe ni mvutaji, au chochote kile ambacho hujazana chini ya mfuko wa bibi.” Watu fulani watangulia kuuona wakati ambao itakuwa kawaida kumwona mwanamke akitembea na bunduki mkononi kama vile ilivyo kawaida kutembea na mwavuli.
Idadi Zao Zinaongezeka
Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi majuzi umeonyesha kwamba kati ya 1983 na 1986, kuwako kwa bunduki miongoni mwa wanawake katika United States “kuliongezeka kama asilimia 53 na kuwa zaidi ya milioni 12.” Pia uchunguzi huo ulionyesha kwamba wakati wa miaka mitatu hiyo, “wanawake zaidi kama milioni 2 walikuwa wakifikiria kununua bunduki [au bastola].” Katika magazeti fulani ya wanawake, uangalifu huelekezwa kwa ujanja kwenye uhitaji wa mwanamke kupata ulinzi kwa kuonyesha mwanamke akirudi nyumbani na kukuta dirisha limevunjwa katika mlango wake wa mbele. Je! yeye huishi peke yake? Je! ana bunduki ya kujilinda akikutwa na mvamizi? Nambari ambayo huwekwa chini ya tangazo hilo la bidhaa kuonyesha kwamba kodi haitatozwa kumbe huwa ni ya watengenezaji wa bunduki hizo, sasa wakifanya toleo jipya la bunduki nzuri kwa ajili ya wanawake.
“Matangazo hayo ya bidhaa ni kama kumwaga chumvi katika kidonda,” akasema mwanamke mmoja. Sababu ni kwamba kwa kuwa wanawake wengi sana huishi peke yao au ni wazazi waseja, wao huhisi wakiwa ndio wenye kuelekea zaidi kupatwa na uhalifu wa kijeuri, mara nyingi wakiwa na sababu nzuri. Katika majiji mengi yaliyo makubwa, kulala wanawake kinguvu kumeongezeka. Wanawake hunyang’anywa vibeti vyao—wengi kwa kutishwa kudungwa kisu. Kuna mashambulio juu ya wanawake barabarani, katika sehemu za kuegesha magari, na katika majengo ya ofisi saa za mchana. Nyumba za ghorofa na nyumba za watu peke yao, makao ya wanawake waishio peke yao, huvunjwa hali mkaaji amelala. “Ingekuwa afadhali tujifunze kujilinda wenyewe,” akasema mwanamke mmoja, “kwa sababu kadiri tuzidivyo kuwa wenye kutembea sana katika jamii yenye ongezeko la jeuri, itakuwa lazima tujilinde wenyewe.”
“Nilikuwa nikitembea kwenda nyumbani kutoka kazini,” akasema mwanamke mmoja aliyehojiwa katika televisheni ya United States. “Mtu fulani alinishika ghafula kwa nyuma. Alikuwa na kisu naye akanisukuma chini na kunyakua kibeti changu. Papo hapo, nilisema ni lazima nichukue hatua.” Baada ya mwanamke huyo kupeleka ombi la kupata ruhusa ya kutembea na bunduki na kufanya mazoezi ya kulenga shabaha katika uwanja wa kufyatulia, alikuwa na maoni gani? “Niliipoteza kabisa hisi ya kushambuliwa kwa urahisi. Nilijiwazia kwamba, mimi nina bunduki, ninaitumia kufyatua na inafanya kazi vizuri sana, nami siogopi. Nikiwa na kipande hiki cha chuma mikononi mwangu, kwa kweli ningeweza kujilinda.”
Ni wazi kwamba huko ndiko kuwaza kwa wanawake zaidi ya milioni 12 katika United States, na ni nani ajuaye ni wangapi zaidi walio na silaha za haramu? Tarakimu za ulimwenguni pote zingeweza kuwa kubwa ajabu. Hata hivyo, je! kuwaza huko kumetokana na utafiti mwingi juu ya jinsi mambo ya uhakika yaonyeshavyo? Kabla wewe hujaenda ukanunue silaha ya kujikinga, fikiria vile maofisa wa polisi na takwimu zaonyesha.