Bunduki—Njia ya Maisha
ULE mlolongo mrefu wa nyumba nyekundu za kukodi zenye umayamaya wa viumbe hai umerudia kawaida. Mlio wa risasi zinazotoka katika bunduki otomatiki na nusu-otomatiki hauharibu tena utulivu. Mimweko ya moto inayotokana na kila mlipusho wa silaha hizo imeacha kutia vivuli vya kuogofya wakati wa usiku, na imeacha kusaidia kuzimulika barabara zenye nuru hafifu. Kuna mashimo katika sehemu za mbele za majengo ya matufali ya kale ambamo risasi zimepenya kwa kina kirefu katika mapigano ya kutumia bunduki zamani na sasa.
Polisi na wachunguzi wa kitiba wajua sana barabara hizo. Bohari la kuwekea silaha nyingi za kutosha kikosi kidogo cha polisi limetwaliwa—matokeo ya visa vya kuua watu, visa vya watu kujiua wenyewe, mifyatuo ya kiaksidenti, na visa vya unyang’anyi. Wasafirisha-barua na wachukua takataka wakataa kuhudumia jumuiya hiyo kwa kuhofu kunaswa kati ya miminiano la risasi. Watoto watunzwa ndani ya nyumba zao, lakini bado baadhi yao wauawa kwa bunduki wakati risasi zitupwazo kutoka bunduki zilizolengwa shabaha kimakusudi au kimakosa zipenyapo madirisha na kuta na kuzunguka vururu-vururu katika vyumba.
Ikiwa wewe waishi katika jiji kubwa, kuna mawezekano ya kwamba wazielewa sana tamasha zilizosimuliwa hapa, na ikiwa si kwa kushuhudia kwa macho yako mwenyewe, basi ni kwa kuziona ukiwa mtazamaji wa habari za jioni katika TV. Katika majiji mengi mifyatuo ya risasi ni ya kawaida sana hivi kwamba huwa hairipotiwi katika magazeti ya huko. Mara nyingi, hiyo huwa si kitu ikilinganishwa na mauaji mengine ya kufyeka umati wa watu ambayo huvuta uangalifu wa habari za kila siku katika majiji mengine au sehemu nyingine za ulimwengu.
Kwa kielelezo, tamasha fulani ya mauaji ya kufyeka umati wa watu Kalifornia ilitangazwa katika sehemu nyingi za ulimwengu wakati mtumia bunduki aliponyunyiza risasi mia moja kutokana na bunduki ya ushambulizi ya kumimina risasi haraka kwa umati wa watoto wa shule ya msingi, akiua wanafunzi 5 na kujeruhi 29 wengine kabla ya kujiua mwenyewe kwa bunduki ya mkononi. Ulaya na United States pia zilisoma habari za kushtusha juu ya mwanamume kichaa aliyeua kinyama watu 16 katika Uingereza kwa bunduki ya ushambulizi ya aina ya AK-47. Katika Kanada mwanamume aliyechukia wanawake alienda Chuo Kikuu cha Montreal na kufyatua risasi na kuua wanawake 14. Hata hivyo, vingi vya visa hivyo vya kuua kimakusudi au kiaksidenti huwa haviripotiwi nje ya jiji ambamo vimetukia, isipokuwa kama hesabu ya waliokufa ni kubwa sana.
Uvutio wa Ajabu Kuhusiana na Bunduki
Wawakilishi na viongozi wenye kutekeleza sheria ya kieneo, ya kimkoa, ya kitaifa, na ya kimataifa wanatatanishwa na wimbi linaloongezeka la vifo visemwavyo kuwa hutokana na bunduki za mkononi na silaha otomatiki na nusu-otomatiki zilizo kubwa ambazo tayari zimo mikononi mwa wahalifu na watu wenye kasoro za akili. Shirika la Kimataifa la Wakuu wa Polisi lakadiria kwamba kuanzia silaha otomatiki na nusu-otomatiki kama 650,000 hadi 2,000,000 “huenda zikawa zimo mikononi mwa wahalifu kotekote taifani [U.S.A.]—kikosi cha watu wabaya ambao karibu sikuzote ndicho hufanikiwa kulenga shabaha zao,” laripoti U.S. News & World Report.
Yakadiriwa kwamba katika United States pekee, karibu kila nyumba ya pili ina bunduki. Ingawa hesabu kamili ya bunduki zilizo na Waamerika haiwezi kujulikana wazi, makadirio ya hivi majuzi yaonyesha kwamba Waamerika milioni 70 wana bunduki milioni 140 hivi na bunduki za mkononi milioni 60. “Bohari la matumizi ya faragha la kuwekea silaha za taifa latosha kugawia kila mwanamume, mwanamke na mtoto nchini bunduki moja-moja,” likaandika U.S. News & World Report. Je! wewe waona hilo kuwa jambo la kushtusha?
Katika Ulaya pia raia wamekuwa kama kambi yenye silaha. Uingereza inajaribu kuliweza tatizo layo la silaha kwa kadiri watu wabaya wajitwaliavyo silaha chungu nzima. Katika Ujeremani ya Magharibi rundiko haramu la bunduki na bastola lakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya silaha zote zinazoenezwa. Kulingana na ripoti mbalimbali, hesabu fulani ya silaha hizo zimeibwa kutoka “ghala la silaha za polisi Wajeremani, za polisi wa mipakani, za jeshi la Ujeremani na za NATO.” Uswisi yaripotiwa kuwa na kadiri ya juu zaidi ulimwenguni ya bunduki na bastola za matumizi ya faragha. “Mswisi yeyote mwenye kufuata sheria aweza kuwa na bunduki [zake], na kila mtu mume mwenye umri wa kwenda jeshini ni lazima aweke nyumbani bunduki ya ushambulizi iliyo na nguvu kuliko ile iliyotumiwa katika mauaji ya umati wa watu ya Stockton [Kalifornia],” likaripoti The New York Times la Februari 4, 1989.
Siku chache mapema kidogo, The New York Times liliripoti kwamba katika San Salvador, “bunduki hupatikana kwa wingi kama vibeti kwenye viuno vya wanaume. Masokomakuu, ambayo walinzi wayo huzunguka-zunguka vijia wakiwa na bunduki aina ya shotigani, hutaka wanunuzi waache silaha zao katika viweko vya bidhaa kwenye milango ya mbele.” Kulingana na gazeti Asiaweek la Februari 1989, serikali ya Ufilipino “yakubali kwamba nchi imefurikwa na angalau bunduki na bastola 189,000 zisizo na leseni. Hizo, kuongezea zile 439,000 zenye leseni, zamaanisha kwamba silaha zilizo mikononi mwa watu mmoja mmoja faraghani zapita kwa mbali zile zilizo na majeshi, ambayo yana silaha kama 165,000 za kawaida. Na silaha haramu hutwaliwa kila juma kwenye uwanja-ndege wa kimataifa na kwenye ufuo wa Manila.”
Kanada yenye amani, ambako Sheria za Uhalifu huzuia vikali kumiliki na kutumia bunduki na bastola, inapatwa na ongezeko la polepole la makosa ya kutumia bunduki na bastola. Mwishoni mwa 1986, kulikuwako bunduki na bastola karibu 860,000 zilizosajiliwa (zilizoandikishwa) na kuwekewa vizuizi katika Kanada. Hiyo haikutia ndani silaha otomatiki ambazo watu walijiwekea faraghani kabla ya 1978. Ofisa wa polisi Mkanada ambaye amefanya kazi muda mrefu alisema: “Jambo ambalo ningependa kujua ni kwa nini watu wa Kanada huhisi uhitaji wa kuwa na bunduki ya mkononi, bunduki ya kawaida au bunduki aina ya shotigani.”
Serikali ya United States ilipopiga marufuku ya muda hivi majuzi ili silaha nusu-otomatiki zisiingizwe kutoka nchi za nje, kulikuwa na matokeo yasiyotarajiwa. Wanunuzi wenye hamu nyingi walingoja muda mrefu katika milolongo ili wanunue zile ambazo tayari zilikuwa katika maduka ya bunduki kila mahali nchini. “Ni kama lile vumaiko la kukimbilia mashamba kule Oklahoma,” akasema mnunuzi mmoja aliyesimama katika mlolongo ili anunue moja ya zile za mwisho-mwisho akibani. Hizi zingeweza kununuliwa kwa karibu dola 100 kabla ya marufuku hiyo. Siku hiyo zilikuwa zikinunuliwa kwa kiasi cha kufikia dola 1,000 kila moja. “Bunduki hizi zinaingia na kutoka 30 kwa siku,” akasema mwenye duka mmoja mwenye furaha. “Wanazinunua zote, ki-i-la kitu wawezacho kupata,” akasema. “Wamefanya nyumba ya kila mtu iwe na moja,” akasema mwingine mwenye duka la bunduki.
Sheria fulani katika mkoa wa Florida, United States, imeruhusu wenye bunduki watembee peupe wakiwa na bunduki iliyofungwa ukanda kiunoni pao au iliyofichwa mwilini mwao. Watu fulani wahofu kwamba huenda hiyo ikatokeza mitupiano-risasi kwenye kona za barabara, ikileta kumbukumbu la ile enzi ya uhayawani wa Magharibi. Mwakilishi mmoja wa Mkoa wa Florida alisema: “Ujumbe tunaoutoa ni kwamba, ‘Sisi hatuwezi tena kukulinda wewe, kwa hiyo wewe mwenyewe jipatie bunduki na ufanye yote uwezayo.’” Na kwa kuamua kulingana na mauzo ya bunduki, maelfu wanafanya hivyo hasa.
Kwa nini kuna ukichaa huu wa ghafula wa kutaka bunduki—nyingine zazo zikiwa na nguvu sana hivi kwamba zaweza kupitisha risasi katika kuta za mawe na kufyatusha risasi 900 kwa dakika moja, zikiwa zimeundwa kwa kusudi pekee la kupambana kwenye uwanja wa vita? Wenye mamlaka fulani wasema kwamba bunduki zina “uvutio wa kijinsia” ambao hufanya ziwavutie wanaume kwa njia hususa. “Kuchukua silaha iliyo kubwa zaidi, iliyo mbaya zaidi na yenye nguvu zaidi kuna kadiri fulani ya hisia ya uanaume,” akasema ofisa mmoja wa serikali. “Kwa wanaume hasa, bunduki huamsha uvutio wa kurudia ujana wao,” akaandika ripota mmoja. Mashirika fulani ya benki yameanza kutumia uvutio huu wa bunduki kwa kutolea watu bunduki za mkononi badala ya kulipa faida ya pesa zilizowekwa akibani. Ripoti zaonyesha kwamba mpango huo umependwa mno na wawekaji akiba.
Ulimwenguni pote, mauzo ya bunduki yanasitawi sana. Yataishia wapi? Je! ni wakati kila mshiriki wa kiume wa jamii apatapo angalau bunduki moja au zaidi? Au je! bunduki ni za wanaume peke yao? Fikiria mambo fulani ya kupendeza katika makala inayofuata.