Kwagga Wote Wameenda Wapi?
HEBU tazama kwagga kwa uangalifu sana (Equus quagga)—au sivyo utadanganyika. Akitazamwa kutoka mbele, angedhaniwa kimakosa kuwa punda-milia. Kutoka nyuma, kwagga walifanana na farasi. Kutoka kando, ungeona wanyama hao wawili—kwa sababu hivyo ndivyo kwagga alivyofanana kabisa.
Kwa ubaya, uwezekano wako wa kuweza kuona kwagga ulikwisha katika kao moja la wanyama la Amsterdam mnamo Agosti 12, 1883, kwa sababu wakati huo ndipo wa mwisho wa wanyama hao wa kigeni alipokufa. Yote yanayobaki leo ni mifano 23 iliyotengenezwa kwa kushindiliwa vitu ndani, viunzi saba vya mifupa, na michoro kama huu unaoona hapa.
Ni msiba kama nini! Wakati mmoja makundi makubwa ya Kwagga yalikuwa yakiranda-randa katika kusini mwa Afrika. Makabila ya kwanza ya kusini mwa Afrika Wabushmen na Wahottentot waliposikia mlio wa kwagga uliokuwa kama kukohoa, uliwafurahisha sana hivi kwamba kwa kawaida waliwaita tu kwa sauti waliyotoa—“kwagga kwagga.” Kisha, kwa kusikitisha, wakati wa karne ya 19, mifyatuo yenye kuendelea ya bunduki za wawindaji ilihakikisha kwamba kwagga wangejiunga na wanyama waliotoweka.
Hata hivyo, kulingana na Bw. Reinhold Rau, mkuu wa sehemu ya kushindilia ngozi ya wanyama ya Jumba la Hifadhi la Vitu vya Kale la Afrika Kusini katika Cape Town, bado kuna tumaini. Kwa njia gani? Wataalamu walipochunguza urithi-tabia wa DNA (deoxyribonucleic acid) wa nyama ya misuli iliyokauka na damu iliyotolewa kwa mifano ya kwagga, ilipatikana kwamba kwagga alikuwa tu ni aina ya punda-milia wa kawaida wa nyanda, au Burchell. Hiyo inamaanisha kwamba miongoni mwa punda-milia wa nyanda, ambao bado ni wengi sana, kuna uwezekano mkubwa kwamba chembe za urithi ambazo hazijakomaa za kwagga zinaweza kutokezwa kwa uzalishaji wa kuteua.
Na hilo hasa ndilo jambo Bw. Rau, pamoja na Halmashauri ya Majaribio ya Uzalishaji wa Kwagga, wanajaribu kuchunguza. Kutoka mkoa wa Natal wa Afrika Kusini na mbuga ya wanyama ya Etosha katika Namibia, punda-milia wenye alama hafifu katika miguu yao ya nyuma na sehemu ya nyuma waliteuliwa na kuzalishwa mmoja na mwenzake. Kufikia sasa watoto wa kwanza waliozaliwa wanaonyesha matokeo mazuri.
Tofauti na kwagga, aina nyingi za wanyama hazina nafasi kama hiyo ya kurudishwa. Matabiri yanayotia hofu yanaonyesha kwamba kufikia mwaka wa 2000, kufikia asilimia 15 hadi 20 ya aina zote za wanyama wanaoishi duniani huenda zikatoweka. Upotevu huo mkubwa wa unamna-namna wa wanyama watokana sanasana na mkono wa binadamu wenye uharibifu. Hivyo, programu ya kurudisha tena kwagga ni jambo dogo tu kwa kulinganisha.
Hata hivyo, kuna uhakikisho wenye kufariji. Katika unabii ulioandikwa katika kitabu cha mwisho cha Biblia, Ufunuo, Muumba wa aina tofauti-tofauti zikadiriwazo kuwa milioni 10 hadi milioni 30 ya viumbe vilivyo duniani anaahidi “kuwaharibu hao waiharibuo nchi.” (Ufunuo 11:18) Kwa kutokuwapo kwa waharabu kama hao, wanadamu waaminifu watatimiza ifaavyo fungu lao wakiwa watunzaji wa Dunia yetu.—Mwanzo 1:28; Isaya 11:6-9.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]
Hisani ya Jumba la Hifadhi la Africana, Johannesburg