Bunju-Miba—Samaki Mdogo Mwenye Sifa Nyingi
Na mleta habari za Amkeni! kutoka Japani
“NDOANA yangu ilimezwa na samaki mdogo mwenye kurukaruka. Nilipomvuta, mwanakijiji mwenye urafiki alinihakikishia kwamba nilichoshika kilikuwa kitoweo kitamu sana. Hata hivyo, samaki huyo alikuwa mdogo sana, kwa hiyo nikamrusha tena baharini. Ni baadye tu niligundua kwamba kama ningepika na kumla samaki huyo mdogo mwenye miiba, huo ungekuwa mlo wangu wa mwisho.”
Mgeni huyo aliyekuja Japani alikuwa amenasa bunju-miba, kitoweo kitamu cha wenyeji. Wataalamu wanalipa kuanzia dola 50 hadi 160 za U.S. kila mtu kwa ajili ya mlo kamili wa bunju-miba. Hata hivyo, bunju-miba wana sumu inayoitwa tetrodotoksini, inayopatikana zaidi katika maini, mifuko ya mayai, figo, na wakati mwingine kwenye ngozi ya samaki huyo. Vipimio elfu kumi vya panya mdogo, labda vinavyoweza kutoshea kwenye kichwa cha pini, vinaweza kuua mtu wa kimo cha kadiri.a
Kukiwa na aina 100 za bunju ulimwenguni pote, wote hao hujifurisha. Akivuta maji ndani ya gunia la kipekee katika umio, samaki huyo wa kawaida hupanuka akajiunda kama tufe, akifunikwa kwa miiba mikali ambayo humvunja moyo mwindaji wowote anayefikiria kummeza. Sura yake iliyobadilika yaweza kumduwaza adui, au huenda akatoa maji ili kufanyiza “mlo” wenye kuepa atoke alikojificha katika changarawe chini ya bahari. Hivyo, majina yake yanafaa: samaki-vimba, samaki-tufe, na samaki-fura.
Katika nyakati za sasa, bunju-miba ameua watu kadhaa kila mwaka. Hata hivyo, watayarishaji wa bunju-miba wanasema kwamba visa vilivyo vingi vilihusu watu wasio stadi waliojaribu kutayarisha samaki huyo wenyewe.
Bunju-miba alipata uangalifu wa kimataifa wakati Wajapani walipojaribu kuanzisha kitoweo hicho katika United States. Ruhusa ya kumwingiza huko haikukubaliwa, na vyombo vya habari vikambandika jina “samaki-muuaji,” wakidai kwamba kula bunju-miba ni “ulaji wenye kuleta kifo.” Je! dai hilo lilikuwa la kweli?
Mwenye Kulika Ajapokuwa na Sifa Mbaya
“Ni salama kabisa kula bunju-miba,” asema Shinichiro Nagashima, mpishi wa bunju-miba wa kizazi cha tatu. “Tunajua ni sehemu zipi za samaki huyo zilizo na sumu, na hutolewa na mamlaka zifaazo. Kwa zaidi ya miaka 30 ya utayarishaji wa bunju-miba katika Tokyo, hakuna yeyote ambaye amekufa kutokana na sumu ya bunju-miba kutoka kwa samaki aliyetayarishwa na duka lenye idhini kisheria.”
“Sheria ni kali,” Shinichiro aendelea. “Kwa mfano, ikiwa viungo hivyo haviondolewi kwa njia inayofaa, huenda duka likaadhibiwa kwa kufungwa kwa mwezi mzima. Au hata ikiwa duka ni lenye uuzaji mwingi sana, na liandae sehemu yenye kusababisha kifo, litalazimishwa kufungwa kabisa.
“Sheria za utayarishaji wa bunju-miba na majaribio na idhini ya wapishi katika sehemu hii zilianzishwa mara ya kwanza na babu yangu. Alikuwa wa kwanza kuanzisha upishi wa bunju-miba katika sehemu Kuu ya Tokyo wakati wa miaka ya 1950 [samaki huyo] alipokuwa anajulikana sana katika Japani magharibi.”
Baba ya Shinichiro, Yutaka, ni mwamuzi wa wanaotaka kuwa wapishi wa bunju-miba. Anafanana na mahali pake aongeapo akiwa dukani mwake, kati ya mapambo ya fanusi yaliyojazwa ngozi zilizokaushwa za bunju-miba zikining’inizwa kwenye pao.
“Kujifunza kuwa mpishi wa bunju-miba kwamaanisha kupata ujuzi kamili wa viungo vyote vya bunju-miba na kupita mtihani mgumu unaotia ndani kusafisha bunju-miba na kutaja sehemu zake zote kwa dakika 20.”
Shinichiro achukuapo kisu kuonyesha jinsi ya kusafisha bunju-miba, mara hiyo anaonekana kuwa mtu anayekaza fikira kwenye kazi yake mkononi. Baba yake atazama na kueleza sehemu za huyo samaki. Sufuria mbili zisizo na kutu ziko kando ya ubao wa kukatia. Katika sufuria moja, ini, figo, na sehemu nyingine zenye sumu zawekwa. Katika sufuria ile nyingine kwawekwa sehemu zinazofaa za samaki. Kwa dakika chache tu, nofu nyeupe hukatwa ziwe nyembamba zaidi na kupangwa kama majani ya mauwa yenye kuonekana wazi. Figili iliyosagwa na pilipili huongeza rangi. Chakula hicho kitamu chapendeza vyote macho na ulimi.
Bw. Nagashima mkubwa atabasamu akikumbuka juu ya siku ambazo bunju-miba walikuwa tele. “Nilipokuwa mvulana, bunju-miba hawakuwa ghali kama ilivyo leo. Kwa kuwa baba yangu alikuwa mpishi wa bunju-miba, nilimbeba shuleni katika mfuko wangu wa kuweka chakula cha mchana. Watoto wengine walitamani kubadilishana nami chakula changu kitamu.”
Sifa Iliyokwezwa?
Katika 1988, Shirika la Kusimamia Chakula na Dawa la U.S. lilitambua kuwa bunju-miba waliotayarishwa na wapishi wenye kibali ni salama kwa kuliwa na likaruhusu bunju-miba aingizwe katika United States.
Hata hivyo, utayarishaji wa bunju-miba si upishi ambao mvuvi anaweza kujifanyia mwenyewe tu. Ukimpata bunju-miba, lazima atayarishwe na mpishi mwenye idhini. Hii tu ndio njia salama ya kufurahia mlo wa samaki huyu mdogo aliye na sifa nyingi.
[Maelezo ya Chini]
a Tetrodotoksini hupimwa kwa kipimio cha panya. Kipimio cha panya ni kiwango kinachoweza kuua panya wa gramu 20 kwa dakika 30.