Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 8/8 kur. 22-25
  • Je! Familia Yangu Ichanjwe?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Je! Familia Yangu Ichanjwe?
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Historia ya Nyuma
  • Je! Mtoto Wangu Achanjwe?
  • Vipi Juu ya Athari?
  • Vipi Juu ya Dawa za Kuchanjia za Watu Wazima?
  • Damu Katika Utengenezaji wa Dawa za Kuchanjia
  • Je! Familia Yangu Ichanjwe
  • Matokeo ya Jitihada za Kupambana na Magonjwa
    Amkeni!—2004
  • Ukimwi—Jinsi ya Kupigana Nao
    Amkeni!—1998
  • Kitendeshi cha Rh na Wewe
    Amkeni!—1994
  • Maswali Kutoka kwa Wasomaji
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1990
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 8/8 kur. 22-25

Je! Familia Yangu Ichanjwe?

“NI WAKATI wa sindano za kuchanjia watoto,” daktari anasema. Labda hayo ni maneno makubwa sana kwa mtoto kusikia, lakini kwa ujumla yametokeza tu tabasamu yenye kutoa uhakikishio na ishara ya kuitikia kutoka kwa wazazi.

Hata hivyo, karibuni maswali yamezushwa kuhusu dawa za kawaida za kuchanjia watoto na watu wazima. Ni dawa zipi za kuchanjia ambazo kwa kweli zinahitajika? Namna gani juu ya athari? Je! damu inahusika kwa njia yoyote katika kutengenezwa kwa dawa ya kuchanjia?

Hayo ni maswali mazuri ya kufikiriwa na familia ya Kikristo yenye kujali. Majibu yanaweza kuwa na athari ya moja kwa moja kwa afya na wakati ujao wa watoto wako na vilevile wako mwenyewe.

Historia ya Nyuma

Katika miaka ya 1950 dawa ya kuchanjia yenye kutumika sana ilitokezwa na ikamaliza kihalisi hofu za watu juu ya ugonjwa wa kupooza (polio) katika nchi nyingi. Kufikia 1980 pigo la ugonjwa wa ndui lilitangazwa kuwa limeangamizwa ulimwenguni pote, hilo likiwa tokeo la programu zenye mafanikio za kuchanja. Jambo hilo lilionekana kuthibitisha maneno ya Benjamin Franklin: “aunsi moja ya kinga ni sawa na ratili moja ya ponyo.”

Leo, programu za kuchanja zimekuwa na mafanikio kwa ujumla katika kudhibiti magonjwa mengi—pepopunda, kupooza, ugonjwa wa koo, na kifaduro, tukitaja machache tu. Na zaidi, imeonyeshwa kwamba wakati kuchanja kumepuuzwa kwa sababu fulani, ugonjwa umerudi. Jambo hilo lilitokea katika nchi moja na ugonjwa wa kifaduro.

Kuchanja hutimiza nini? Kwa msingi, kwa njia moja kati ya mbili, kunatia kinga za mwili nguvu dhidi ya mashambulizi ya vijidudu vinavyoitwa pathojeni vinavyosababisha magonjwa, vinavyotia ndani viini na virusi. Njia ya kwanza inaitwa kuchanjwa kunakodumu. Katika kisa hiki dawa ya kuchanjia inakuwa tu na pathojeni iliyodhoofishwa au kuuawa (au sumu yayo) ambayo imerekebishwa kwa njia ya kwamba haiwezi kumdhuru mtu. Kinga ya mwili yenyewe huanza kutengeneza molekuli zenye kuua zinazoitwa viuajisumu vinavyoweza kupigana na vijidudu vya ugonjwa halisi, iwapo ugonjwa huo watokea. Ikiwa dawa ya kuchanjia ina visehemu vya sumu ya pathojeni, hiyo inaitwa toksoidi. Ikiwa inatengenezwa kutokana na pathojeni ambayo imedhoofishwa lakini bado ni hai au vijidudu vilivyouawa, hiyo inaitwa dawa ya kuchanjia.

Kama unavyojua, dawa hizo za kuchanjia hazitokezi kinga ya mara iyo hiyo. Huchukua muda kwa mwili kutengeneza viuajisumu vya ulinzi. Kuchanja kunakodumu kunatia ndani dawa na sindano zote za watoto ambazo huonwa na wengi kuwa za kuchanjia. Dawa hizo za kuchanjia hazihusiki na damu katika hatua yoyote ya kutengenezwa ila tu ya aina moja (inayozungumziwa baadaye).

Njia nyingine ni dawa ya kuchanjia inayotoka kwa mwingine. Hiyo hutumika tu kwa hali ambazo mtu amejihatarisha kwa ugonjwa hatari, kama vile kichaa cha mbwa. Katika hali hiyo, hakuna nafasi kwa mwili kujenga kinga yao wenyewe. Kwa hiyo viuajisumu vya mtu mwingine, ambavyo tayari vimetengenezwa, vinaweza kudungwa kwa sindano mwilini ili vipigane na pathojeni katika mtu huyo aliyehatarishwa. Globulini ya gama, kizuia-sumu, na umaji-maji wa damu wenye kinga ya juu sana ni majina mengine ya dawa zinazotokezwa kwa damu ya watu au wanyama wenye kinga. Dawa hizo za kuandaa kinga zilizoazimwa, au kutolewa kwa wengine hukusudiwa zipatie mwili msaada wa mara iyo hiyo na wa muda tu wa kupigana na vishambulizi. Viuajisumu hivyo huondolewa upesi mwilini vikiwa protini za kigeni.

Je! Mtoto Wangu Achanjwe?

Baada ya kuona historia hiyo ya nyuma, huenda wengine bado wakauliza, ‘Ni dawa gani za kuchanjia ambazo mtoto wangu anapaswa kupokea?’ Katika sehemu nyingi za ulimwengu ambazo dawa za kuchanjia watoto zinapatikana kwa urahisi, kuchanja kwa ukawaida kumetokeza upungufu mkubwa katika visa vya magonjwa yanayowapata watoto hasa.

Kwa miaka mingi Chuo cha Amerika cha Utibabu wa Watoto, kikishirikiana kwa ujumla na mashirika mengine kama hayo ulimwenguni pote, kimependekeza kuchanjwa dhidi ya magonjwa haya yanayofuata: ugonjwa wa koo, kifaduro, na pepopunda. Kwa kawaida dawa za magonjwa hayo matatu huchanganywa pamoja na kutolewa zikiwa dawa moja ya kuchanjia inayoitwa—DPT—ikifuatwa na nyongeza nyingine tatu za DPT zenye kuimarisha ambazo hutolewa baada ya vipindi vya angalau miezi miwili-miwili. Mbali na hiyo, dawa za kuchanjia surua, matubwitubwi (kuvimba mashavu na shingo), na surua ya Ujerumani hutolewa zikiwa moja ikiitwa—MMR—kwa watoto baada ya wao kuwa na umri wa mwaka mmoja. Pia, dawa za kumezwa za kuchanjia ugonjwa wa kupooza (OPV) huandaliwa kwa ratiba inayofanana na ile ya DPT.a

Katika sehemu nyingi, kupokea dawa za kuchanjia kwa kawaida ni lazima, ingawa hesabu ya dawa za nyongeza za kuimarisha zinaweza kutofautiana. Hivi karibuni, kwa sababu ya kutokea mara nyingi kwa ugonjwa wa surua, nyongeza za dawa za kuchanjia zimependekezwa chini ya hali fulani. Unaweza kumwendea daktari katika eneo lenu kwa maelezo zaidi.

Kwa kuongezea hayo, kuna dawa za kuchanjia ugonjwa wa kichomi inayoitwa (Pneumovax). Inaoonekana kwamba hiyo huandaa kinga ya maisha kwa watoto na watu wazima, ambao kwa sababu fulani, hupatwa kwa urahisi na aina fulani za ugonjwa wa kichomi.

Dawa nyingine ya kuchanjia inaitwa Hib. Hiyo hutolewa ili ilinde dhidi ya pathojeni ya kawaida inayosababisha mafua ya Hemofila katika watoto. Kijidudu hicho husababisha magonjwa mengine kadhaa katika watoto, hasa aina mbaya ya ugonjwa wa ngozi ya ubongo. Kwa ujumla dawa hiyo ya kuchanjia imethibitika kuwa salama kutumiwa, na inaendelea kupendekezwa kuwa sehemu ya mfululizo wa dawa za kuchanjia watoto.

Imetukia pia kwamba kufikia sasa bado hakuna dawa ya kawaida ya kuchanjia ugonjwa wa tetekuwanga. Na dawa ya kuchanjia ugonjwa wa ndui haipatikani tena kwa sababu, kama ilivyotajwa mapema, programu ya ulimwengu mzima ya kuchanjia ndui imeondoa kabisa ugonjwa huo hatari.

Vipi Juu ya Athari?

Namna gani juu ya suala la athari za dawa za kuchanjia? Kwa kawaida, athari za dawa nyingi huwa ni ndogo sana na za muda tu, zaidi ya ule mlio wa ghafula wa kawaida na machozi ya muda ya watoto—zikikaa sana ni siku moja hivi ya homa. Lakini wazazi wengi wana wasiwasi mwingi juu ya hatari za dawa hizo za kuchanjia. Uchunguzi mmoja wa kitiba ulichunguza mahangaiko ya wazazi juu ya afya ya watoto wao na kupata kwamba asilimia 57 ya wazazi waliohojiwa walihangaikia athari za dawa za kuchanjia.

Hivi karibuni, hangaiko kubwa limetangazwa juu ya sehemu moja ya dawa ya DPT, ile sehemu ya kifaduro. Kufaulu kwa dawa hiyo ya kuchanjia kumepunguza sana ugonjwa huo ulioogopewa sana—kutoka visa 200,000 kila mwaka katika nchi moja pekee kabla ya dawa hiyo ya kuchanjia kutokezwa hadi visa 2,000 kila mwaka baada ya matumizi makubwa ya dawa hiyo ya kuchanjia. Hata hivyo, athari mbaya sana—kufurukuta na hata madhara ya ubongo—zimetokea kwa karibu kisa 1 kati ya dawa za kuchanjia 100,000 zilizotolewa.

Ingawa athari hiyo hutokea mara chache sana, hiyo hutokeza hangaiko fulani kwa wazazi wengi ambao hawana la kufanya ila kuruhusu watoto wao wachanjwe ndipo wastahili kwenda shuleni. Na kwa sababu ugonjwa wa kifaduro una madhara makubwa sana unapokumba jumuiya, ingawa si ugonjwa wa kawaida, wastadi wameamua kwamba kwa mtoto wa kawaida, “dawa hiyo ya kuchanjia ni salama zaidi kuliko kushika ugonjwa huo.” Wastadi hao wanashauri kwamba dawa ya kuchanjia itumiwe isipokuwa “wakati dawa ya mapema iliposababisha kufurukuta, mchochota wa ubongo, ambukizo lenye kudumu la mishipa ya ufahamu, au kuzimia. Wala watoto ‘wanaosinzia-sinzia sana, wanaolia sana kwa sauti (kulia sana kwa kelele kwa muda wa saa 3 au zaidi wakati mmoja), wala wenye kuwa na joto ya mwili zaidi ya [sentigredi 40.5]’ hawapaswi kupokea dawa za ziada za kuchanjia.”b

Suluhisho halisi la tatizo hilo katika nchi nyingi ni kutumia dawa ya kuchanjia yenye chembe zilizo hai, kama zile zinazotolewa katika Japani wakati huu kukiwa matarajio mazuri sana. Dawa hiyo mpya ya kuchanjia inaonekana kuwa salama zaidi na inaendelea kupatikana katika nchi nyinginezo vilevile.

Dawa nyinginezo za kuchanjia watoto kwa kawaida zimethibitishwa mara kwa mara kuwa zenye matokeo na zenye usalama wa kadiri fulani.

Vipi Juu ya Dawa za Kuchanjia za Watu Wazima?

Mara mtu anapokuwa mtu mzima, kuna dawa chache tu za kuchanjia zenye kudumu ambazo anapaswa kukumbuka. Kwa kufaa, watu wazima wote wanapaswa kuwa na kinga tayari dhidi ya magonjwa ya surua, matubwitubwi, na surua ya Ujerumani kwa sababu ya kupatwa na magonjwa hayo au kuchanjwa dhidi yayo wakati wa utoto. Swali lolote likizuka kuhusu kinga ya jinsi hiyo, daktari anaweza kupendekeza dawa ya kuchanjia ya MMR kwa mtu mzima.

Dawa ya kuchanjia ya toksoidi ya ugonjwa wa pepopunda huonwa kuwa kinga inayofaa dhidi ya pepopunda ikipokewa kila miaka kumi hivi. Watu wenye umri mkubwa zaidi na wale ambao wana magonjwa ya kudumu wanaweza kuwaendea madaktari wao kuhusu dawa za kila mwaka za kuchanjia mafua makali. Wale wanaosafiri kuelekea sehemu nyingine za ulimwengu wanapaswa kufikiria kuchanjwa dhidi ya magonjwa kama homa ya manjano, kipindupindu, kimeta, homa ya matumbo, au tauni ikiwa magonjwa hayo yanapatikana sana katika sehemu wanazoenda.

Dawa nyingine moja ya kuchanjia yenye kudumu inapasa kufikiriwa kwa sababu ndiyo dawa ya pekee ya kuchanjia yenye kudumu inayotengenezwa kutoka damu. Ni dawa ya kuchanjia mchochota-ini aina ya B inayoitwa Heptavax-B. Dawa hiyo ya kuchanjia hukusudiwa itumiwe na watu fulani, kama vile wafanyakazi wa afya, ambao wanaweza kuhatarishwa kiaksidenti na sehemu za damu zinazotoka kwa wagonjwa ambao wameambukizwa na mchochota-ini aina ya B. Ingawa inasifiwa kuwa maendeleo makubwa, dawa hiyo ya kuchanjia ilihangaisha watu wengi kwa sababu ya jinsi inavyotengenezwa.

Kwa msingi, damu za watu waliochaguliwa wenye virusi vya mchochota-ini aina ya B hukusanywa na kutiwa dawa za kuua aina yoyote ya virusi, na aina fulani ya kichochezi cha mchochota-ini aina ya B inakusanywa. Kichochezi hicho kisafi, ambacho hakitendi kinaweza kutumiwa kikiwa dawa ya kuchanjia. Hata hivyo, watu wengi hukataa kupokea dawa hiyo ya kuchanjia wakiogopa kujihatarisha kwa kutwaa sehemu za damu kutoka kwenye watu walioambukizwa, kama vile wale ambao wana upotovu wa kingono. Zaidi ya hayo, Wakristo wengine wenye kudhamiria walikataa dawa hiyo ya kuchanjia kwa sababu ya kuwa imetengenezwa kutoka kwa damu ya mtu mwingine.c

Makatao hayo ya dawa ya kuchanjia mchochota-ini yameondolewa kwa kutokezwa dawa nyingine tofauti lakini yenye nguvu vilevile ya kuchanjia mchochota-ini aina ya B. Hiyo inatengenezwa kupitia tekinolojia ya chembe za urithi ambamo dawa ya kuchanjia inatokezwa katika chembe za hamira bila kuhusisha damu ya binadamu. Ikiwa unafanya kazi katika sehemu za afya au kwa sababu fulani waonwa kuwa unahitaji kuchanjwa dhidi ya mchochota-ini aina ya B, labda utazungumza na daktari wako juu ya jambo hilo.

Damu Katika Utengenezaji wa Dawa za Kuchanjia

Hilo lazusha jambo kuu kwa Wakristo wanaohangaikia katazo la Biblia dhidi ya matumizi mabaya ya damu. (Matendo 15:28, 29) Je! kuna dawa nyinginezo za kuchanjia zinazotengenezwa kutoka damu?

Kwa kawaida, dawa zenye kudumu za kuchanjia hazitengenezwi kutokana na damu ila tu ile ya Heptavax-B. Kwa mfano, dawa hizo zinatia ndani dawa zote za kuwachanja watoto.

Mambo ni kinyume kuhusu dawa ya kuchanjia inayotolewa kwa mwingine. Mtu anaweza kudhania kwamba anaposhauriwa apate dawa ya kuchanjia baada ya kujihatarisha kwa ugonjwa fulani, kama vile baada ya kukanyaga msumari wenye kutu au baada ya kuumwa na mbwa, dawa hizo za kuchanjia (isipokuwa zikiwa nyongezea dawa nguvu) ni zenye umaji-maji wa damu wenye kinga ya juu sana na zimetengenezwa kutokana na damu. Ndivyo ilivyo na globulini ya kinga ya Rh (Rhogam), ambayo mara nyingi hupendekezwa kwa akina mama ambao hawana globulini ya Rh na ambao kwa sababu fulani wanahatarishwa na damu yenye globulini ya Rh, kama vile wakati wa kuzaliwa kwa mtoto mwenye globulini ya Rh.

Kwa sababu dawa hizo za kuchanjia zinazotolewa kwa wengine ndizo zinazohangaisha kwa sababu ya suala la damu, basi ni msimamo gani unaopasa kuchukuliwa na Mkristo anayedhamiria? Makala za awali katika jarida hili na jenzilo, Mnara wa Mlinzi, zimetoa msimamo usiobadilika: Ni juu ya dhamiri ya Mkristo iliyozoezwa kupitia Biblia kama anaweza kukubali utibabu wa aina hiyo kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya familia yake.d

Je! Familia Yangu Ichanjwe

Wakristo wanastahi sana uhai na wanatamani sana kufanyia afya ya familia zao mambo bora zaidi. Kama unaamua kwa kudhamiria kwamba familia yako ichanjwe, huo ni uamuzi unaopaswa kufanya kibinafsi.—Wagalatia 6:5.

Mstadi mmoja ametaja kifupi hali hiyo vizuri: “Wazazi wanapaswa kuambiwa juu ya kila dawa inayokusudiwa apewe mtoto wao. Wao si watunzi wa kisheria tu wa watoto wao. Wana daraka kwa hali njema na ulinzi wa mtoto wao wakati wa kile kipindi cha maisha ambacho mtoto huyo anawategemea.” Katika jambo la kuchanjwa, na vilevile katika mambo mengine ya kitiba, Mashahidi wa Yehova huchukua daraka hilo kwa uzito sana.—Imechangwa na daktari.

[Maelezo ya Chini]

a Shirika la Afya Ulimwenguni sasa linapendekeza kuchanjwa kwa ukawaida dhidi ya mchochota-ini aina ya B kwa vitoto katika sehemu nyingi za ulimwengu.

b Inaonekana kwamba historia ya familia ya kupatwa na kufurukuta haihusiani na athari za dawa. Na ingawa maambukizo ya kupumua hayaonekani yakileta athari, inaweza kuwa bora kutompa mtoto dawa ya kuchanjia hata kama yeye ni mgonjwa kidogo tu.

c Ona “Maswali Kutoka kwa Wasomaji” katika Mnara wa Mlinzi la Juni 1, 1990.

d Ona Mnara wa Mlinzi, Juni 15, 1978, kurasa 30-1, Kiingereza.

[Sanduku katika ukurasa wa 24]

Dawa za Kuchanjia Zisizotokana na Damu

Dawa za kuchanjia watoto (DPT, OPV, MMR)

Dawa ya kuchanjia ya Hib

Pneumovax

Toksoidi

Dawa za kuchanjia mafua makali

Recombivax-HB

Dawa za Kuchanjia Zinazotokana na Damu

Heptavax-B

Rhogam

Vizuiajisumu

Vikinga sumu (vya kukinga sumu za nyoka na buibui)

Globulini za kinga (kwa ajili ya magonjwa kadhaa)

Globulini ya Gama

Mitayarisho ya umajimaji wa damu wenye kinga ya juu sana (kwa mfano, umajimaji wa kukinga ugonjwa wa kichaa cha mbwa)

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki