Nikiwa Mkimbizi, Nilipata Haki ya Kweli
KWA sababu kungali kulikuwa baridi na theluji ilikuwa chini, nilivaa kabuti nzito. Kisha nikameza mchanganyiko wa kitu chochote chenye sumu ambacho ningepata katika kabati yangu, kutia ndani sabuni yenye umaji-maji (Kaboni tetrakloridi). Nikateremka na kwenda Mto Charles katika Cambridge, Massachusetts, nikitumaini kwamba ningekufa huko. Badala ya kifo, matokeo niliyopata tu ya kutamauka kwangu yalikuwa kulazwa kwa siku tano katika idara ya matibabu ya dharura hospitalini. Ni jambo gani lililonifanya nichukue hatua mbaya kama hiyo? Ebu turudie asili yangu.
Nilizaliwa Jaffa, Palestina, katika 1932, nikiwa Mpalestina-Mgiriki. Nililelewa katika dini ya Orthodoksi ya Kigiriki, jambo lililomaanisha kuzuru kanisa na kufunga kula kulipohitajiwa. Lakini hayo yalikuwa ni mambo ya kidesturi ambayo hayakuwa na maana kwangu.
Wazazi wangu walikuwa matajiri sana, kwa kuwa familia yetu ilikuwa na kampuni kubwa ya kuuza vyakula na pombe. Nilipokuwa na umri wa miaka kumi, nilipelekwa Shule ya Bweni ya Friends katika Ramallah na baadaye nikaenda Shule ya Kianglikana ya St. George’s katika Jerusalem. Shule hiyo ya pili ilinivutia sana—kulikuwa na wanafunzi wenye malezi ya Kikristo, Kiarabu, na Kiyahudi wote wakisoma pamoja kwa amani ya kadiri fulani. Shule hiyo ilifundisha upatano, tabia nzuri, na adabu nzuri. Lakini shule na mambo ya hakika yalikuwa mambo mawili yaliyo tofauti.
Wakati wa utoto wangu, msukosuko wa nchini ulikuwa kawaida ya maisha, huku Wayahudi, Waarabu, na Waingereza wakipigana nyakati zote. Nikiwa mtoto mdogo, nilishuhudia kuuawa kwa mtu mmoja nje ya nyumba yetu. Mara nyingi wazazi wangu waliponea chupuchupu wakiwa katikati ya pande mbili zenye kupigana. Kisha Vita ya Ulimwengu 2 ikafanya Haifa, jiji muhimu lenye bandari, kuwa shabaha ya mabomu ya Ujerumani—vifo na uharibifu zaidi.
Mwisho wa utawala wa Uingereza juu ya Palestina ukija katika Mei 1948, msukosuko wa nchini uliongezeka. Katika Julai 1946 King David Hotel, iliyokuwa hoteli mashuhuri zaidi katika Jerusalem ililipuliwa. Watu wa malezi tofauti-tofauti waliuawa—Waarabu 41, Waingereza 28, Wayahudi 17, na wengine 5. Familia yetu iliamua kutoroka hali hiyo mbaya. Katika usiku mmoja tulihamia Saiprasi, ambako mama alikuwa na watu wa ukoo. Baba aliacha nyuma biashara yake na mali zake kadhaa.
Matukio hayo yalibadili mielekeo yangu ya mapema. Nilipokuwa na umri wa miaka 16, nilipendezwa na siasa hivi kwamba nikawa nasoma magazeti ya habari kila siku ili kwenda sambamba na matukio. Kiongozi wa Misri, Gamal Abdel Nasser, alinivutia sana. Alidhoofisha uvutano wa nchi za kigeni katika nchi yake.
Katika 1950 familia yetu ilihamia United States. Ile Vita ya Wakorea illikuwa ikiendelea, na nilitaka nichangie nchi iliyokuwa imeokoa familia yangu kutokana na hali ya uonevu. Nilijitolea kwa Kikosi cha Wanahewa, ambako nilipanda cheo hadi kufikia sajini wa stafu. Lakini, sikupata kwenda Korea—nilifikia tu kituo cha wanahewa katika Omaha, Nebraska.
Mwenye Kupendelea Mabadiliko Katika Shule ya Kitheolojia
Baada ya kuachiliwa kutoka katika Kikosi cha Wanahewa, nilienda Chuo Kikuu cha Teksas na baadaye Chuo Kikuu cha Ohio, nilikopata digrii katika mambo ya uchumi. Nilikuwa msemaji sana dhidi ya ukosefu wa haki katika Mashariki ya Kati na hata nilialikwa kuhutubu juu ya kichwa hicho. Profesa mmoja wa Episkopali, Dakt. David Anderson, aliyenisikia nikisema, alidokeza kwamba nikubali kulipiwa Mtaala wa masomo ya ziada katika Shule ya Kitheolojia ya Kiepiskopali katika Boston. Na kwa sababu sikukubaliana na mfumo wa makasisi wanaolipwa mshahara, sikutaka kuwa kasisi. Hata hivyo, katika 1958, nilikubaliwa kwenda shule hiyo.
Mtaala huo ulitia ndani kufanya kazi katika sehemu zenye watu wenye akili punguani pamoja na makasisi wa kijeshi. Pande za kinadharia na kimasomo za shule hiyo zilipendeza sana, lakini nilitaka kuona hatua zikichukuliwa na haki zikitekelezwa zaidi katika ulimwengu. Kwa hiyo nilianzisha kikundi chenye kutaka mabadiliko kilichoitwa “Jina Lake Litangazwe Miongoni mwa Mataifa Yote.” Nilitaka shule hiyo iwe na mwelekeo wa kuchukua hatua. Nilitaka kufuata Yesu ulimwenguni, si maktabani.
Hata hivyo, upesi niligundua kwamba mabadiliko niliyopendekeza hayangetumiwa. Hatimaye, niliombwa niondoke shule hiyo. Karibu na wakati huo nilipenda sana mwanamke mmoja mchanga aliyekuwa upeo wa utafutaji wangu wa mtu ambaye ningeweza kushiriki naye wakati ujao wangu. Nilihisi tumefaana sana. Kisha nikagundua kwamba hakuwa na hisia kama zangu. Lile pigo la kukataliwa lilikuwa kubwa sana. Likawa jambo la mwisho lililonifanya nijaribu kujiua.
Kazi-Maisha Nikiwa Mwalimu
Baada ya kipindi cha kupata nafuu, nilihudhuria Chuo Kikuu cha Kolumbia cha New York ili kufuatia programu ya shahada ya masta ya kufundisha jiografia na historia. Katika kipindi hicho chote, bado nilikuwa nikitafuta kile nilichokiita Ukristo halisi wenye matendo. Kazi yangu ya kufundisha ilinipeleka South Glens Falls, New York. Nikiwa huko, badiliko kubwa lilitokea maishani mwangu. Nilikutana na mwalimu aliyeitwa Georgia aliyekuja kuwa mke na mwenzi wangu katika 1964.
Bado nilikuwa mtu wa siasa sana na nilikuwa nikifuata hotuba za Mbunge James Fulbright, aliyekuwa akipinga vita katika Vietnam. Mimi pia nilipinga vita hiyo. Nilipata shtuko kubwa sana kwa kifo cha Rais John F. Kennedy mnamo Novemba 1963. Niliathiriwa sana hivi kwamba nilihudhuria maziko yake katika Washington.
Utafutaji Wangu wa Ukristo
Katika 1966 tulihamia Long Island, New York, nilikoanza kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Northport. Nilikuwa nikihangaikia sana matukio ya ulimwengu—kilikuwa kipindi cha kujaribiwa kwa dawa za kulevya, mabaradhuli, na vikundi vya kujitolea kwa Yesu. Nilihudhuria kikundi kimoja cha waabudu wenye kelele nikaona kwamba wao vilevile walikuwa wanapungukiwa na ule ujumbe wa kweli wa Ukristo wakikazia zaidi hisia kuliko matendo. Katika pindi nyingine hata nilimsikia mhudumu mmoja wa Episkopali akitetea vita katika Vietnam. Nikaanza kufikiri kwamba watu fulani wanaokataa kuwapo kwa Mungu walikuwa na hisia ya kibinadamu kuliko watu wa kanisa.
Nilipoteza imani yangu katika Mungu lakini si katika thamani ya kisiasa ya Mahubiri ya Yesu Mlimani. Kwangu alivunja ile kawaida ya chuki kwa mafundisho yake, na niliona hayo kuwa suluhisho la tatizo la Mashariki ya Kati. Nilijaribu dini nyingi sana—Katoliki, Jeshi la Wokovu, Baptisti, Kipentekosti—lakini nyakati zote nikitoka na ile hisia ya utupu kwamba hazikuwa zikifuata ule Ukristo wa Wakristo wa mapema. Kisha, katika 1974, nilikutana na mwakilishi wa mauzo ya ploti aliyebadili maisha yangu.
Aliitwa Frank Born. Nilikuwa na mazungumzo naye kuhusu mali fulani. Katika wakati wa kuzungumza, alitoa Biblia. Mara moja nikakataa, niki-sema: “Huwezi kupata mtu anayefuata kanuni hizo maishani mwake.” Naye akajibu: “Kuja pamoja nami, ujionee mwenyewe katika Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova.” Lakini nilimtaka anijibu baadhi ya maswali ya msingi kabla nizuru Jumba la Ufalme lake.
Swali la kwanza: “Je! mna makasisi wanaolipwa mshahara?” Jibu lake likawa: “La. Wazee wetu wote ni watu wenye kujitolea wanaojitegemeza na kutegemeza familia zao kwa kazi yao ya kimwili.” Swali langu lililofuata likawa: “Je! nyinyi hukutana katika nyumba za faragha kama walivyokuwa wakifanya Wakristo wa mapema ili kujifunza Biblia?” Jibu likawa: “Ndiyo. Tuna mikutano ya kila juma katika nyumba za faragha katika sehemu tofauti-tofauti za ujirani.” Ni lazima swali langu la tatu lilionekana kuwa lisilo la kawaida kwake. “Je! kanisa lenu hupeleka mhudumu kwa sherehe za kutawazwa kwa rais ili kuombea rais?” Frank akajibu hivi: “Sisi hatuungi mkono upande wowote katika mambo ya kisiasa wala hatushiriki. Utii wetu ni kwa Ufalme wa Mungu ukiwa suluhisho la pekee kwa matatizo yanayopata ainabinadamu leo.”
Nilishindwa kuamini yale niliyokuwa nikisikia. Nikawa na hamu sana ya kuona mahali Wakristo hao hukutania. Nilipata nini? Si ibada ya hisia moyo nyingi bali kusababu vizuri kutokana na Biblia. Mikutano yao ilikuwa yenye kuelimisha, ikifanya watu wastahili kueleza na kutetea imani yao ya Kikristo. Kilikuwa kikundi chenye kuchukua hatua, kikienda miongoni mwa watu wanaotamani utawala wa Mungu wenye haki. Hapa palikuwa jibu langu la tatizo la Mashariki ya Kati—watu wa jamii zote, lugha zote, na tamaduni zote wakiungana katika ibada yenye amani ya Bwana Mwenye Enzi Kuu wa ulimwengu wote mzima, Yehova Mungu. Na wanafanya hayo yote kulingana na kielelezo na mafundisho ya Kristo. Hapakuwa na chuki wala msukosuko hapa. Amani na umoja tu.
Nikawa Shahidi aliyebatizwa katika 1975, na Georgia akanifuata miaka mitano baadaye. Tuna wana wawili, Robert na John, wanaotangaza kwa bidii habari njema za Ufalme wa Mungu.
Mielekeo Iliyobadilika
Mielekeo yangu imelainika kwa muda wa miaka ambayo imepita. Hapo awali nilikuwa mtu mkali wa kijeshi ambaye hakujali maoni ya wengine. Kama ilivyo na mamilioni wengi, kufikiri kwangu kulikuwa kumeathiriwa na dini bandia na siasa. Sasa nang’amua kwamba Mungu hana upendeleo na kwamba watu wenye mioyo myeupe wa kila jamii wanaweza kumtumikia kwa amani na umoja.
Miongoni mwa Mashahidi wa Yehova, nimepata watu wa kila aina ya malezi, watu waliochukia wengine hapo awali. Sasa, kama ilivyo na mimi, wamekuja kutambua kwamba kwa kweli Mungu ni upendo, na hilo ni moja ya yale mambo ambayo Yesu alikuja kutufundisha. Yeye alisema hivi: “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:34, 35)—Kama ilivyosimuliwa na Constantine Louisidis.
[Picha katika ukurasa wa 13]
Constantine Louisidis mwenye umri wa miaka kumi akihudhuria Shule ya Wavulana ya Friends
[Picha katika ukurasa wa 14]
Nilipata shtuko kubwa sana kwa kifo cha Rais John F. Kennedy