Wahandisi Stadi
Na mleta habari za Amkeni! katika Afrika Kusini
JE! UMEPATA kuona miundo kama hiyo inayoonyeshwa kwenye ukurasa huu? Vichuguu huonekana sana katika mbuga za Afrika. Vingine vina umbo la mabomba membamba ya moshi ambayo nyakati nyingine hufikia kimo cha meta 6.[11] Vingine huwa ni makuba makubwa ya ardhi ambayo hupendwa sana na wanyama-wawindaji kama simba katika kutafuta mawindo.
Ndani ya kila kichuguu mna vijia vingi na vyumba vingi, viwezavyo kukaliwa na mamilioni kadhaa wa mchwa wadogo-wadogo.[1] Mchwa fulani hukuza mashamba yao wenyewe ya kuvu na wao huweza kuyatia maji mashamba hayo hata katika miaka yenye ukame. Hilo lawezekanaje? Katika kipindi cha miaka ya 1930, wakati ukame mkali sana ulipoharibu kabisa sehemu fulani za Afrika Kusini, mstadi wa wadudu, Dakt. Eugene Marais, aligundua safu mbili za mchwa, moja ikishuka chini na nyingine ikipanda shimo. Viumbe hivyo vidogo vilikuwa vimechimba kina kipatacho meta 30! Vilikuwa vimefikia kisima chenye kujitokeza chenyewe. Kwa njia hiyo Marais aligundua jinsi viliweza kudumisha unyevu katika mashamba yao ya kuvu katika kipindi cha ukame.[2]
Kichuguu cha kawaida, aeleza Michael Main katika kitabu chake Kalahari, “kinaaminiwa kuwa kao la hali ya juu zaidi lililopata kujengwa na mnyama yeyote ulimwenguni. . . . Wote hujitahidi kudumisha unyevu wa asilimia 100 na halijoto za sehemu zote kuwa kati ya digrii sentigredi 29 na digrii sentigredi 31, ifaayo kuvu na mchwa pia. . . . Basi kila kao ni nyumba iliyopasishwa hewa kikamili.”[4]
Sasa fikiria jinsi makao hayo hujengwa. Mchwa hulainisha na kushikanisha kipande kimoja kidogo cha mchanga kwa kingine.[5] Ebu wazia ni mamilioni mangapi ya vipande vya mchanga vitumiwavyo kujenga kichuguu kimoja! “Vitu vikubwa zaidi ambavyo mwanadamu amepata kujenga duniani; zile Piramidi za Misri, mfumo wa Reli ya Chini ya Ardhi ya London, orofa ndefu za New York . . . , vikilinganishwa na kazi za mchwa, . . . vinakuwa kama chungu ya udongo ukilinganishwa na milima,” akaandika Marais katika kitabu chake The Soul of the White Ant. “Ukifikiria kadiri ya ukubwa,” aendelea kusema, “ingelazimu mwanadamu ajenge jengo lenye kimo kama Matterhorn [mlima wenye kilele kinachofika meta 4,478 katika Uswisi][10], kama kazi yake ingetoshana na mnara wa kichuguu chenye kimo cha futi arobaini.”[6]
Lakini mchwa hufaidi mwanadamu na nini? Jambo moja, mchwa hula majani yaliyonyauka na kwa hiyo kuondoa takataka nyingi.[7] “Kwa kuvuruta vitu vilivyokauka chini ya ardhi, wao hupunguza hatari ya kuzuka kwa moto na vilevile kurutubisha mchanga wa chini,” ubao mmoja katika Mbuga ya Kitaifa ya Kruger wasema hivyo.[8]
Labda wewe pia wakubali kwamba mchwa wa hali ya chini wastahili kuitwa wahandisi stadi.