Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 1/22 kur. 13-17
  • Mabwawa ya Ulimwengu—

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mabwawa ya Ulimwengu—
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mabwawa, Sehemu za Ukuzi za Ulimwengu
  • Mbio za Kuangamiza Mabwawa
  • Shida ya Maji
  • Mashambulizi Hayo Yafanywa Ulimwenguni Pote
  • Matokeo Yatakuwa Nini?
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—1995
  • Maji Safi
    Amkeni!—2023
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
  • Je, Dunia Itategemeza Vizazi Vijavyo?
    Amkeni!—2008
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 1/22 kur. 13-17

Mabwawa ya Ulimwengu—

Hazina za Kimazingira Zinazoshambuliwa

WAHINDI wa Amerika waliuita mto huo Baba ya Maji Mengi. Wanajiografia wauita Mississippi. Hata uuite nini, mto huo ulilipiza kisasi kwa wale ambao walikuwa wameusonga sana katika maboma na kuta za kuzuia maji, jambo lililoufanya mto huo ukose yale mabwawa yao. Ukiwa umefurishwa na mvua kubwa ya majuma kadhaa, mto huo ulifagilia mbali magunia ya mchanga yakadiriwayo kuwa milioni 75 yaliyokuwa yamepangwa kuuzuia na kuvunjilia mbali kuta 800 kati ya zile 1,400 zilizoshindwa kuuzuia. Maji mengi sana ya gharika yalifagilia mbali nyumba, barabara, madaraja, na sehemu za reli na kufanya majiji mengi yafurikwe na maji. “Labda ndilo furiko baya zaidi lililopata kutukia katika United States,” The New York Times, la Agosti 10, 1993, likaripoti.[1]

Gazeti Times lilieleza kwa ufupi baadhi ya uharibifu uliotokea: “Katika pigo lalo kubwa la muda wa miezi miwili, furiko hilo kubwa la Magharibi ya Kati la 1993 lilitokeza uharibifu mkubwa zaidi. Liliua watu 50, na kuacha watu karibu 70,000 bila makao, likafunika eneo lenye ukubwa kushinda New Jersey mara mbili, likatokeza uharibifu wa mali na wa ukulima unaokadiriwa kuwa wenye thamani ya dola bilioni 12 na kutokeza mjadala mpya juu ya mfumo wa kudhibiti furiko la taifa hilo na sera zalo.”[1a]

Kuacha mfumo wa kiasili wa mabwawa yaliyo karibu na kando-kando ya Mississippi bila kuguswa kungeokoa maisha ya watu 50 na dola bilioni 12. Watu watajifunza lini kwamba kushirikiana na hali ya asili ni bora kuliko kujaribu kuidhibiti? Mabwawa yaliyo karibu na mto hutumika kuwa tambarare za kunasa furiko zinazotoa na kuweka akiba maji ya ziada ya mito iliyofurika kwa sababu ya mvua nzito.[2]

Kutumika kuwa njia ya asili ya kudhibiti furiko ni moja ya utumishi mwingi mzuri ajabu unaofanywa na mabwawa ya dunia yenye ukubwa unaozidi kilometa za mraba 8,500,000—yanayoshambuliwa na kuharibiwa sasa ulimwenguni pote.[2A]

Mabwawa, Sehemu za Ukuzi za Ulimwengu

Kuanzia mabwawa makubwa yenye chumvi katika sehemu za pwani hadi mabwawa madogo yenye maji yasiyo na chumvi na mabwawa yenye tope-tope katika sehemu za bara, hadi mashimo ya nyanda za United States na Kanada,[3] mfanyizo wa msingi wa mabwawa ni maji. Mabwawa ni maeneo ambayo ardhi imefunikwa na maji nyakati zote au katika vipindi vya mafuriko pekee. Aina nyingine ni bwawa la pwani, au la kutokezwa kwa kujaa na kupwa kwa bahari.[4] Na kwa sababu mabwawa mengi huwa na ukuzi mwingi sana wa mimea—nyasi, mafunjo, kangaja, miti, na vichaka—hayo hutegemeza aina mbalimbali za mimea, samaki, ndege na maisha ya wanyama ulimwenguni pote.[5]

Idadi fulani ya ndege wanaopenda pwani na ndege wa maji hufanyiza makao yao katika mabwawa. Aina zao zaidi ya mia moja hutegemea mabwawa hayo yasiyo na vina virefu.[6] Mabwawa mengi ni sehemu za ukuzi za idadi kubwa za bata-bukini na bata—bata-mwitu, bata-mdogo, na bata-mdomo mrefu.[7] Maeneo hayo pia huandaa chakula na makao kwa wanyama kama aligeta, biva, muskrati, cheche wa maji, na musi. Wanyama wengine kutia ndani dubu, paa na rakuni, pia hutumia mabwawa.[8] Mabwawa hayo hutumika yakiwa sehemu za kutaga mayai na sehemu za ukuzi wa samaki wengi wanaotegemeza biashara ya uvuvi ya Amerika yenye thamani ya dola bilioni tatu.[9] Yakadiriwa kwamba aina mbalimbali 200 za samaki na[9A] idadi kubwa ya kaa hutegemea mabwawa kwa mzunguko wote au sehemu ya maisha yao.[10]

Kwa kuongezea kuwa sehemu zenye kutokeza sana za ukuzi wa maisha, mabwawa yana mafaa mengi ya kimazingira. Hayo ni vichungi vya asili vya kuondoa takataka na vichafuzi kutoka kwa mito na vijito na kusafisha maji yaliyopo chini ya ardhi.[11] Mabwawa huweka akiba ya maji katika msimu wa mvua na mafuriko na baadaye kuyaingiza kidogo-kidogo katika vijito, mito, na chini ya ardhi.[14] Mabwawa yatokezwayo kwa kujaa na kupwa kwa bahari hulinda ukingo wa bahari usimomonyolewe na mawimbi.[15]

Kwa sababu ya asili yayo ya kuwa na mimea ya aina nyingi, mabwawa hutimiza mambo mengi ya maana, yaliyo muhimu. Kwa kielelezo, katika mfumo wa usanidimwanga (fotosinthesisi) mimea yote ya kijani-kibichi hufyonza karboni-dioksidi kutoka hewani na kuirudishia hewa oksijeni. Jambo hilo ni muhimu katika kuendeleza uhai. Hata hivyo mimea katika mabwawa ni ya kipekee kwa sababu mimea hiyo hasa ni bora sana katika kufanyiza mfumo huo.[17]

Kwa karne nyingi nchi nyingi zimetambua thamani kubwa sana ya usimamizi wa mabwawa kwa ajili ya ukuzaji wa chakula. Kwa kielelezo, Uchina na India zaongoza katika ukuzaji wa mpunga ulimwenguni, huku nchi nyinginezo za Asia zikifuata kwa ukaribu. Ukikuzwa katika mabwawa ya mashamba ya mpunga, mchele ni mojawapo mazao muhimu zaidi ya chakula ulimwenguni. Karibu nusu ya idadi ya watu ulimwenguni hula wali ikiwa chakula chao kikuu.[18] Baadaye United States na Kanada zilianza kuona umuhimu wa mabwawa na kwa ajili ya ukuzi wao wa mpunga na aina fulani za beri.[19]

Wanyama wa pori vilevile hushiriki karamu iandaliwayo na mabwawa. Si mbegu na wadudu pekee wanaopatikana kwa wingi wakiwa chakula kwa ndege bali ndege hao pia hula samaki na kamba wanaotaga mayai na kukua katika mabwawa. Bata, bata-bukini na ndege wengine wa majini vilevile hula viumbe vingi vinavyoishi chini ya maji katika mabwawa hayo yenye viumbe vingi. Mazingira ya sasa husawazisha mambo kwa njia fulani kwa kutokeza aina kadhaa za ndege kuwa mlo kwa wanyama wenye miguu minne ambao huenda wakaja kwenye mabwawa kutafuta chakula. Katika mabwawa hayo kuna kitu fulani kwa kila kitu. Kwa kweli hizo ni sehemu za ukuzi za ulimwengu.

Mbio za Kuangamiza Mabwawa

Katika United States, yule mtu aliyekuja kuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo alianzisha maangamizo makubwa ya mabwawa wakati alipoanzisha kampuni moja katika 1763 ya kuondoa maji kutoka kwenye Bwawa la Dismal lenye ukubwa wa ekari 40,000—bwawa la pori lenye wanyama wengi wa pori—katika mpaka wa Virginia na North Carolina.[20] Tangu wakati huo, mabwawa ya Amerika yameonwa kuwa vitu visivyofaa, yakizuia maendeleo, chanzo cha ugonjwa na maradhi, mazingira mabaya ya kudhibitiwa na kuangamizwa kwa hali yoyote ile.[21] Wakulima walitiwa moyo waondoe maji kutoka kwenye mabwawa hayo na wayalime na hao walilipwa kwa kufanya hivyo. Barabara kuu zilijengwa sehemu ambazo zamani zilikuwa zimejaa viumbe vingi vya ajabu. Sehemu nyingi zilikuja kuwa sehemu za maendeleo ya miji na vituo vya biashara ama zilitumiwa zikiwa mabonde yafaayo ya kutupia takataka.

Katika miongo michache iliyopita ya karne hii, United States imekuwa ikiharibu mabwawa yayo kwa kiwango cha ekari 500,000 kila mwaka.[22] Kufikia leo ni ekari milioni 90 pekee zinazobaki.[23] Kwa kielelezo, fikiria eneo la mashimo-mashimo la Amerika Kaskazini. Katika kizingo cha ardhi cha kilometa za mraba 800,000 kinachotokea Alberta, Kanada, hadi Iowa katika United States, maelfu ya mabwawa ya nyanda yalikuwa sehemu za mamilioni na mamilioni ya bata kutagia mayai.[24] Yasemekana kwamba wakiwa angani, wangetia anga giza kama mawingu mazito.[25] Leo idadi yao imepungua sana.[26]

Hata hivyo, tatizo litakalotokea baadaye ni hili: Mabwawa yakiharibiwa, sehemu za chakula hutoweka. Bila chakula cha kutosha, bata hutaga mayai machache zaidi, na kiwango cha kuangua mayai huathiriwa sana.[27] Makao yao yakiharibiwa, bata wengi zaidi humiminikia makao machache yanayosalia, jambo linalofanya washikwe kwa urahisi na mbweha, koyote, nyegere, rakuni, na wanyama wengine wanaowala bata hao.[28]

Katika United States, asilimia 50 ya mabwawa ya eneo la mashimo ya maji yametoweka.[29] Kanada yafuatia nyuma kwa kuwa na asilimia zaidi ya 40, lakini mashambulizi yayo yenye uharibifu mkubwa yaendelea kuongezeka.[30] Sehemu kadhaa za North Dakota katika United States zilikuwa kavu kwa asilimia 90, gazeti Sports Illustrated liliripoti hivyo.[31] Wakulima huona mabwawa kuwa hayana faida na kuwa ni vitu visivyofaa vinavyozuia vifaa vyao vya ukulima,[32] wasijue thamani yao ya kimazingira.

Hata hivyo, makelele ya umma ya kuhifadhi makao ya wanyama ya mabwawa yanatokezwa zaidi na watu mmoja-mmoja pamoja na mashirika yanayoshughulikia wanyama wa pori. “Mashimo hayo ya maji ni muhimu sana,” akasema ofisa mmoja mwenye kuhangaika. “Ikiwa tutakuwa na tumaini lolote la muda mrefu kwa bata, ni lazima tuhifadhi mabwawa.”[33] “Ndege wa majini ndio kipimo cha hali ya bara,” akasema ofisa mmoja wa shirika la hifadhi la Ducks Unlimited.[34] Gazeti U.S.News & World Report laongezea maoni yalo: “Idadi ipunguayo [ya bata] yaonyesha mashambulizi kwa mazingira yenye kutoka pande nyingi tofauti-tofauti: Mvua ya asidi, dawa za kuua wadudu, na kubwa kuliko mashambulizi yote, ule uharibifu wa mamilioni ya ekari za mabwawa yenye thamani kubwa sana.”[35]

“Asilimia 90 ya mabwawa ya maji ya chumvi yaliyoko pwani ya California yameangamizwa,” laripoti gazeti California, “na ekari 18,000 hutoweka kila mwaka. Mnyama elki-tule hupatikana tu katika sehemu chache mbalimbali. Idadi ndogo sana ya bata na bata-bukini hurudi kila mwaka katika kipupwe kwenye sehemu hizo zao zenye kuendelea kutoweka. Aina nyingi za ndege wa mabwawa wanakaribia kutoweka.”[37] Ndege hao ambao uhai wao wategemea mabwawa ya ulimwengu waomba msaada kwa ukimya.

Shida ya Maji

Kitu kibaya zaidi kimetokea wakati mwanadamu amekuwa akiharibu mabwawa ya dunia. Ameathiri kitu chake chenye thamani kubwa zaidi na chenye umuhimu zaidi—maji. Maji ni muhimu kwa kila kiumbe chenye uhai. Wanasayansi wengi wametabiri wakati ambapo maji safi yatakapokuwa nadra zaidi ya vitu vingine vyote duniani. “Ama tupunguze kutumia maji vibaya ama kufikia mwaka 2000 tutakuwa tukifa kwa kiu,” Mkutano wa Ulimwengu wa UM juu ya maji ukatangaza hivyo katika 1977.[38]

Kwa kutokea kwa maonyo hayo ya uwezekano mkubwa wa kukosa maji yenye thamani kubwa, hekima ya kawaida yapasa iongoze watu watumie maji ya dunia ifaavyo. Hata hivyo, katika mbio za mwanadamu za kuangamiza mabwawa, yeye amehatarisha sana maji yenye kuhitajiwa zaidi. Mabwawa husaidia kusafisha maji yaliyoko juu ya ardhi—mito na vijito. Akiba fulani za maji sasa hazipokei tena maji safi bali sasa zimechafuliwa na takataka na vichafuzi, yote hayo kwa madhara ya mwanadamu. Maji ambayo wakati fulani yalikuwapo katika mabwawa mengi yamekwisha kuondolewa, jambo linaloongezea upungufu huo.

Je! watu walio na madaraka watasikia vilio vyenye majonzi vya kusaidia uhai unaotegemea mabwawa? Je! hatua itachukuliwa ya kuokoa uhai kama huo kabla ya kuchelewa mno? Ama wanadamu wataendelea kupuuza vilio hivyo, wakisikiliza tu vilio vya watu wenye pupa?

Mashambulizi Hayo Yafanywa Ulimwenguni Pote

Katika mwanzo wa kampeni ya ulimwenguni pote yenye kudhaminiwa na Umoja wa Mataifa ili kuokoa mabwawa, hatari zikabilizo mazingira ya bwawa la Pantanal la Brazili zilitajwa. Ni mojapo mabwawa makubwa zaidi ulimwenguni. Gazeti BioScience lilisema hivi: “Pantanal, likiwa na wanyama wa pori wengi sana na wa aina mbalimbali, ni eneo linalokabili hatari. Kukatwa kwa misitu; ukulima wenye kuendelea kupanuka; uwindaji na uvuvi haramu; na kuchafua maji kwa dawa za kuua magugu, za kuua wadudu, na vitu vitokanavyo na utengenezaji wa mafuta ya kileo umesababisha upungufu unaoendelea kuongezeka wa mazingira ya asili, jambo linalohatarisha mmoja wa mfumo wa kimazingira ulio muhimu zaidi katika Brazili.”[39]

Gazeti The New York Times lilitaja hatari zinazokabili mabwawa yaliyoko kando-kando ya Mediterania. “Kupungua kwa mabwawa kumeongezeka katika miongo mitatu ya mwisho kwa sababu pwani ya Mediterania imekuja kupendwa zaidi na mwendo mbali wa ufuko umekuja kufunikwa na simiti kwa ajili ya ibada ya jua, starehe na faida. Uchunguzi mbalimbali wa Umoja wa Mataifa wataja upungufu mkubwa sana [wa mabwawa] katika Italia, Misri, Uturuki na Ugiriki.”[40]

Mabwawa ya Mbuga ya Kitaifa ya Doñana ya Uhispania iliyo maridadi zaidi na yenye ukubwa wa ekari 125,000 huwa kiwanja cha ndege katika kipindi cha masika wakati ndege wapatao mamia ya maelfu kutoka Afrika kuelekea Ulaya wanapotua hapo katika mabwawa yayo na sehemu zayo za miti-miti ili kujenga viota na kutaga mayai na kula chakula. Lakini hoteli nyingi, viwanja vingi vya kuchezea gofu, na mashamba yazungukayo mbuga hiyo yanatumia maji mengi sana hivi kwamba kuwapo kwa mbuga hiyo kumo hatarini. Katika miaka 15 iliyopita, miradi kama hiyo tayari imeondoa maji mengi sana kiasi cha kwamba kiwango cha maji kimepungua kwa meta 2 hadi 9, na nyanja kadhaa zimekauka. “Ukuzi wowote hapa,” mkurugenzi wa utafiti wa mbuga hiyo asema, “utaua Doñana kabisa.”[40a]

Gazeti State of the World 1992 laripoti: “[Mabwawa ya] mikoko, mojapo aina ya mabwawa yaliyo hatarini zaidi na yenye thamani kubwa zaidi yameharibiwa sana katika Asia, Amerika ya Latini, na Afrika magharibi. Kwa kielelezo, karibu nusu ya misitu hiyo ya mabwawa yenye ulinzi katika Ekwedori yamekatwa, mara nyingi kwa ajili ya vidimbwi vya uduvi, na kuna mipango ya kubadili eneo lenye ukubwa uo huo wa sehemu zilizobaki. India, Pakistan, na Thailand zote zimepoteza angalau sehemu tatu kwa nne za mikoko yazo. Yaonekana Indonesia imeazimia kufanya vivyo hivyo: katika Kalimantan, mkoa wayo mkubwa zaidi, asilimia 95 ya mikoko yote hukatwa kwa ajili ya utengenezaji wa mbao.”[41]

Thamani ya mikoko ilionyeshwa katika gazeti la Thailand la Bangkok Post la Agosti 25, 1992: “Misitu ya mikoko ina aina mbalimbali ya miti inayokua sana katika miinuko ya juu ya kujaa na kupwa kwa bahari kando-kando za fuko za kitropiki zenye usawa mmoja na zilizo upande wa demani. Miti hiyo [imesitawi] katika mazingira mabaya ya maji yenye chumvi kidogo na kujaa na kupwa kwa bahari kunakobadilika-badilika. Mizizi yao ya kipekee iliyoko nje na mizizi mikuu yenye kuchunga chumvi imesitawisha mfumo wa kimazingira wenye vitu vingi na wenye utata. Mbali na kulinda maeneo makubwa ya ufuko yasimomonyolewe, mikoko ni muhimu sana kwa uvuvi wa karibu na ufukoni, viwanda vya kutengeneza vitu vya mbao, na wanyama wa pori.

“Kuna viumbe vingi viishivyo katika msitu wa mikoko. Waweza kupata ndege wapendao kuwa kando-kando ya bahari, tumbili walao kaa, paka wavuao samaki na samaki kirukatope ambaye hurukaruka kuvuka bwawa lenye tope kuelekea mashimo ya maji wakati wa kupwa kwa bahari.”[42]

Matokeo Yatakuwa Nini?

Tatizo hilo ni la ulimwenguni pote. Gazeti International Wildlife lasema hivi: “Mabwawa ya tope, hori, mabwawa ya mikoko, mabwawa ya chumvi, mashimo ya nyanda na wangwa ambazo wakati mmoja zilifunika zaidi ya asilimia 6 ya uso wa Dunia zimo katika matatizo makubwa. Mabwawa mengi yameondolewa maji ili yafanyiwe ukulima, yameharibiwa na uchafuzi au kujazwa na watu wenye kuleta maendeleo katika sehemu hizo hivi kwamba karibu nusu ya ekari za mabwawa zimetoweka.”[43]

Je! watu watafanya amani pamoja na dunia? Kufikia sasa ishara zilizopo si nzuri. Lakini, watu fulani wanajitahidi kwa bidii na kudai kwamba watafaulu. Yehova, Muumba wa dunia, asema kwamba hawatafua dafu. Yeye aahidi kwamba ataingilia mambo na kukomesha mashambulizi ya uumbaji wake mzuri ajabu wa dunia. Yeye ‘atawaharibu wao waiharibuo nchi,’ na badala yao ataiachia wale ‘watakaoitunza.’ Kwa watu wenye kuthamini kama hao, atawapa dunia ikiwa zawadi: “Na mbarikiwe ninyi na BWANA [Yehova, NW], Aliyezifanya mbingu na nchi. Mbingu ni mbingu za BWANA [Yehova, NW], bali nchi amewapa wanadamu.”—Ufunuo 11:18; Mwanzo 2:15; Zaburi 115:15, 16.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Mabwawa katika Uswisi

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mbali kushoto na juu: Mabwawa katika United States

[credit Line]

H. Armstrong Roberts

Kushoto: Misitu ya mikoko katika Thailand

[Hisani]

Kwa hisani ya Halmashauri ya Utafiti ya Thailand

Wakazi wa mabwawa: mamba, chura-mkuu, kereng’ende, kasa-boksi achimba shimo la kutagia mayai

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki