Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 1/22 kur. 10-12
  • Nyumba Yenye Furaha—

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Nyumba Yenye Furaha—
  • Amkeni!—1994
  • Habari Zinazolingana
  • Baada ya Siku ya Harusi
    Kufanya Maisha ya Jamaa Yako Yawe Yenye Furaha
  • Ndoa Yako-Yaweza Kuokolewa
    Amkeni!—2001
  • Imarisha Ndoa Yako Kupitia Mawasiliano Mazuri
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2013
  • Jinsi ya Kumsikiliza Mwenzi Wako kwa Makini
    Amkeni!—2013
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 1/22 kur. 10-12

Nyumba Yenye Furaha—

Mahali Ambapo Watu Wawili Wapatana

IKIWA ungetaka kujenga nyumba iliyo imara, yenye usalama, na yenye kustarehesha, ungetumia vifaa gani? Mbao? Matufali? Mawe? Hapa pana pendekezo la kitabu cha Biblia cha Mithali: “Nyumba hujengwa kwa hekima, na kwa ufahamu huthibitika, na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vyote vya thamani na vya kupendeza.” (Mithali 24:3, 4) Naam, hekima, ufahamu, na maarifa huhitajiwa ili kujenga nyumba yenye furaha.

Ni nani aijengaye? “Mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.” (Mithali 14:1) Ndivyo ilivyo na mtu mwenye hekima aonaye kwamba aweza kufanya ndoa yake iwe yenye nguvu na yenye furaha au iliyodhoofika na yenye taabu. Ni mambo yapi hutokeza tofauti? Lapendeza kama nini kwamba madokezo ya washauri fulani wa kisasa wa ndoa yafanana sana na hekima ya kale ya Neno la Mungu, iliyoandikwa maelfu ya miaka iliyopita.

Kusikiliza: “Kusikiliza kwelikweli ni mojapo mambo makuu uwezayo kumpa mtu mwingine na ni muhimu sana katika kujenga na kudumisha uhusiano wa karibu,” chasema kitabu cha ndoa.[1] “Sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa,” yasema Mithali. (Mithali 18:15) Kwa kuwa masikio yaliyofunguka hayaonekani kama jinsi ambavyo macho yaliyofumbuliwa au kinywa kilichofunguliwa kinavyoonekana, waweza kuonyeshaje mwenzi wako kwamba kwa kweli unamsikiliza? Njia moja ni mtazamo wa kioo.—Ona sanduku katika ukurasa 11.

Kusema waziwazi na ukaribiano: “Utamaduni wetu hupinga kusema waziwazi,” chasema kitabu One to One—Understanding Personal Relationships. “Sisi hufundishwa kutokea umri wa mapema tusiingilie sana mambo ya wengine—tuweke ikiwa siri mambo yahusuyo fedha, mawazo, hisia, . . . jambo lolote la binafsi. Somo hilo halipotei hivyo tu, hata kama ‘tumebanwa na mapenzi.’ Jitihada za kusema waziwazi zisipoendelea, basi ukaribiano hauwezi kuwapo.”[2] “Pasipo mashauri makusudi hubatilika,” yaonelea Mithali, “bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.”—Mithali 13:10; 15:22.

Uaminifu-mshikamanifu na tumaini: Mume na mke huapa mbele ya Mungu kuwa waaminifu washikamanifu. Mume na mke wanapotumaini kwamba kila mmoja wao amejitoa kwa mwenzake, upendo hauwi na shuku, kiburi, roho ya kushindana, kushughulika mno na mambo ambayo mmoja aona kuwa ni haki yake.[3]

Kushiriki mambo: Uhusiano huongezeka kwa kushiriki pamoja maono mbalimbali. Baada ya muda mume na mke waweza kufanyiza historia yao yenye thamani ambayo kila mmoja wao athamini sana. Hawawazii hata kidogo kuharibu kifungo hicho cha upendo. “Yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu.”—Mithali 18:24.[4]

Fadhili na wororo: Matendo yenye fadhili hupunguza mizozo ya maisha na kupunguza kiburi. Matendo ya fadhili, yakibaki bila kusahauliwa, hayaharibiwi hata wakati wa hasira katika pindi za kukosana, hivyo yakipunguza madhara yatokeayo. Wororo hutokeza hali changamfu iwezayo kukuza upendo. Ingawa yaweza kuwa vigumu kwa mwanamume hasa kuonyesha upole, Biblia yasema: “Haja ya mwanadamu ni [fadhili-upendo, NW] yake.” (Mithali 19:22) Kwa mke mzuri, “sheria ya wema [fadhili-upendo, NW] i katika ulimi wake.”—Mithali 31:26.[5]

Unyenyekevu: Ukiwa dawa kwa sumu ya kiburi, unyenyekevu hutokeza maneno ya msamaha mara tu jambo litokeapo na vilevile maneno ya kila mara ya kuonyesha shukrani. Vipi ikiwa kweli wewe huna hatia kwa kosa fulani linalotajwa? Mbona usiseme hivi kwa upole, “Nasikitika kwamba umekasirika”? Onyesha hangaiko kwa hisia za mwenzi wako, kisha pamoja mwone jinsi ya kurekebisha kosa. “Mtu kujitenga na ugomvi ni heshima kwake.”—Mithali 20:3.[6]

Staha: “Neno kuu katika kutambua tofauti za kila mmoja na kuzisuluhisha ni staha. Jambo muhimu kwa mwenzi mmoja huenda lisiwe muhimu kwa kadiri ileile kwa mwenzi mwingine. Hata hivyo, kila mwenzi wa ndoa aweza nyakati zote kustahi maoni ya mwingine.” (Keeping Your Family Together When the World Is Falling Apart) “Kiburi huleta mashindano tu; bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.”—Mithali 13:10.[7]

Ucheshi: Tatizo kubwa laweza kuondolewa kwa kucheka pamoja. Huo huingia ndani ya kifungo cha upendo na kuondoa mikazo ambayo huzuia kufikiri kuzuri. “Moyo wa furaha huchangamsha uso.”—Mithali 15:13.[8]

Kutoa: Anza kutafuta mambo mazuri ya kuthamini kwa mwenzi wako na mpongeze sana. Vitu hivyo vyenye thamani vyaweza kutokeza mwitikio wa moyo kuliko zawadi ya tai ya shingoni na shada la maua. Bila shaka bado mwaweza kununuliana vitu ama kufanyiana mambo mazuri. Lakini “zawadi bora zaidi uwezayo kutoa,” chasema kitabu Lifeskills for Adult Children, “si vitu vya kimwili. Ni maneno yako ya upendo na uthamini, kitia-moyo chako, na msaada wako.” “Neno linenwalo wakati wa kufaa. Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.”—Mithali 25:11.[9]

Kama sifa hizo zingelinganishwa na mawe ya kujenga uhusiano wa ndoa, basi uwasiliano ungekuwa saruji ihitajikayo kuyashikanisha mawe pamoja. Kwa hiyo, waume na wake waweza kufanya nini wanapotofautiana maoni? “Badala ya kuona maoni yaliyo tofauti ya mwenzi wako kuwa kisababishi cha hitilafiano, . . . uyaone kuwa chanzo cha kupata ujuzi. . . . Mambo madogo-madogo yawa kama chanzo kikubwa cha habari,” chasema kitabu Getting the Love You Want.[10]

Basi, ona kila pindi ya kutokubaliana kuwa fursa nzuri ya kupata utambuzi zaidi wa mtu huyo umpendaye badala ya kuiona kuwa mwito wa shindano. Mkiwa pamoja mkubali mwito wa kusuluhisha tofauti zenu na kuingia katika upatano wenye amani, na hivyo kuimarisha vifungo vyenu, kuongeza zaidi upendo unaowafanya nyinyi wawili mpatane.

Yehova Mungu hufurahia sana ushirikiano na hivyo aliuweka katika uumbaji wake—katika mzunguko wa oksijeni wa nipe-nikupe kati ya mimea na wanyama, mzunguko wa maumbo ya angani, uhusiano wa kupokezana kati ya wadudu na maua. Na katika muungano wa ndoa vilevile, kwaweza kuwa na mzunguko mchangamfu ambamo mume, katika neno na tendo, amhakikishia mke wake upendo wake, naye mke mwenye upendo na mwenye tumaini afuata ukichwa wake kwa kuridhika. Kwa njia hiyo, wawili kwa kweli waungana, wakileta shangwe kwa kila mmoja na kwa Mwanzilishi wa ndoa, Yehova Mungu.

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

‘Jiangalieni Jinsi Msikiavyo.’—Luka 8:18

Kusikiliza msemaji kwa uangalifu ni njia ya kuhakikisha kwamba msemaji na msikilizaji wanaelewana vizuri. Nyakati nyingine huitwa mtazamo wa kioo, kwa sababu msikilizaji ajaribu kufikiria maneno kana kwamba kutazama kwa kioo na kujaribu kupata maana ya maneno hayo. Hizi ndizo hatua za msingi:

1. Sikiliza kwa uangalifu sana; sikiliza jumbe zenye maana.

2. Sikiliza hisia zinazotokana na maneno hayo.

3. Rudia maneno unayosikia kwa msemaji. Usihukumu, usichambue, wala usibishane. Acha mtu huyo ajue kwamba umeelewa vema ujumbe wake. Kubali hisia zake.

4. Labda msemaji atathibitisha ama kusahihisha jambo usemalo na labda hata aweza kupanua habari hiyo zaidi.

5. Ikiwa hukuelewa vizuri, jaribu tena.

Kusikiliza kwa uangalifu kuna matokeo hasa katika kupunguza ukali wa uchambuzi. Kubali uhakika wa kwamba mara nyingi uchambuzi hutegemea ukweli wa kadiri fulani. Huenda uchambuzi ukatolewa kwa njia yenye kuumiza, lakini badala ya kumrudishia mchambuzi uchungu huo, mbona usisikilize kwa uangalifu ili kupoza mambo? Kubali kwamba wewe unaelewa hisia zozote zile ambazo huenda ulisababisha, na uone jinsi jambo hilo laweza kurekebishwa.[11]

[Sanduku katika ukurasa wa 12]

“Mtu Akiwa na Sababu ya Kumlaumu Mwenzake.”—Wakolosai 3:13

Unapokuwa na lalamiko, waweza kulisemaje bila kuanzisha ugomvi? Kwanza, msifu mwenzi wako wa ndoa kwa sababu ya kuwa na makusudi mazuri. Waweza kuhisi kwamba yeye hakujali, hakufikiria vizuri, alitenda kwa njia ya kimbelembele, hakutenda kwa hekima—lakini kwa ujumla yawezekana kwamba hakuwa na kusudi mbaya. Eleza kwa utulivu hisia zako bila kushtaki: “Ulipofanya hivyo, basi mimi nilihisi . . .” Hakuna jambo lolote la kuanzisha mabishano hapo. Maneno yaonyesha tu hisia zako na hayashtaki mwenzi wako. Na kwa sababu huenda mtu huyo hakukusudia kamwe kukukasirisha kamwe, yeye aweza kukataa au kujitetea. Lakini zingatia tatizo hilo na uwe tayari kupendekeza suluhisho.[12]

[Picha katika ukurasa wa 10]

Kusikiliza kwelikweli ni mojapo mambo makuu uwezayo kumpa mtu mwingine

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki