Saidia Mtoto Wako Akabili Matatizo ya Shuleni
HALI za ulimwengu zinazozorota hutuathiri sote, kutia na watoto wetu. Neno la Mungu, Biblia, lilitabiri sahihi kwamba katika siku yetu ‘kungekuwako nyakati za hatari’ na kwamba ‘watu wabaya na wadanganyaji wangeendelea, na kuzidi kuwa waovu.’ (2 Timotheo 3:1-5, 13) Hivyo, shule leo imejawa na magumu huku wanafunzi wakiminyana na hali ambazo zilipata wazazi wao mara haba. Wazazi waweza kufanya nini wasaidie watoto wao kuzikabili?
Mbano wa Marika
Watoto walio wengi hubanwa na marika nyakati fulani. Mwanafunzi mmoja kijana aliye Mfaransa aomboleza: “Wazazi na jamii hujaribu wawezavyo kutoa msaada, lakini hautoshi. Waasi vijana hulazimisha vijana wengine. . . . Wazazi wasiodhibiti watoto wao si wazazi.”[1]
Wazazi wenye kujali daraka hujaribu kusaidia watoto wao wasitawishe sifa za kiroho ziwapazo nguvu za ndani wahitajizo kukinza mbano wa marika wenye kudhuru. “Sisi hujitahidi sana kusaidia watoto wetu wajenge kujistahi,” aeleza baba mmoja, “ili wasilazimike kutafuta kibali cha marika wao. Ikiwa kufanana na watoto wengine si kwa maana kwao, wataona ni rahisi zaidi kukataa wapaswapo kukataa.”[2] Kufundisha watoto wake washughulikie hali ngumu, mzazi huyu hupanga wakati ili familia yake iigize uhusiano wa mwanafunzi na mwalimu, kuigiza kihalisi hali ngumu ambazo zingeweza kutokea na kuonyesha njia za kuzikabili.[3] Uwe mzazi mwenye kuunga mkono, na usaidie mtoto wako asitawishe ujihakikishio.
Usemi Mbaya
Viwango vya maadili vishukapo ulimwenguni pote, usemi mbaya wazidi kuwa kawaida. Katika nchi nyingi usemi huo husikiwa mara nyingi saa zile ambazo watu wengi zaidi hutazama televisheni. Hivyo, viwanja vya michezo shuleni, vipito vya majengo, na madarasa huvuma maneno machafu.
Walimu fulani hutetea kuapa na kulaani kwao wenyewe, wakibisha kwamba wanafunzi wao waweza kujiamulia mitazamo watakayofuata kuelekea usemi huo.[4] Lakini sera ya jinsi hiyo huruhusu wanafunzi wafuate tu misemo hii iliyoshuka tabia kuwa sehemu ya usemi ukubalikao wa kila siku.
Mzazi mwenye hekima hueleza kwa fadhili kwa nini hairuhusiwi katika familia kutamka maneno ya jinsi hiyo. Aweza pia kuzuia tatizo la usemi mbaya masomoni kwa kuchunguza mpangilio wa masomo ya shule ajue mtoto wake atajifunza vitabu gani. Ikiwa kitabu chochote cha marejezo kilichochaguliwa kina usemi mbaya au chakazia ukosefu wa adili, aweza labda kuomba mwalimu wa mtoto achague kitabu-badala chenye mambo yakubalikayo. Mfikio uliosawazika huonyesha kiasi.—Wafilipi 4:5, New World Translation.
Ukosefu wa Adili na Dawa za Kulevya
Uchunguzi mbalimbali wafunua kwamba wazazi wengi hukiri kuwa “wenye haya au aibu mno kuzungumza habari hiyo [ya elimu ya ngono] nyumbani.”[5] Badala ya hivyo, wao hutegemea shule iwape watoto wao habari sahihi. Lakini The Sunday Times la London laripoti kwamba, kulingana na mwalimu mmoja mzee-wa-kazi, mavuno ya leo ya mimba za matineja ‘yahusiana hasa na ukosefu wa adili kuliko kutojua njia za kuzuia mimba.’[6] Wazazi ndio wenye hali bora zaidi ya kuweka viwango vya mwenendo ambao wawatarajia watoto wao kudumisha.
Ni sawa na utumizi mbaya wa dawa za kulevya. Ukosefu wa mwelekezo wa wazazi huzidisha tatizo hili. “Kadiri maisha ya familia yazidivyo kutomvutia mtoto,” chasema Francoscopie 1993, “ndivyo aelekeavyo zaidi kujitafutia maisha ya namna nyingine. [Kutumia] dawa za kulevya ni moja la hayo.”[7] “Uzazi ni kazi ngumu,” akiri Micheline Chaban-Delmas, msimamizi wa shirika Toxicomanie et Prévention Jeunesse (Utumizi wa Dawa za Kulevya na Ulinzi wa Vijana). “Lazima ujihadhari daima; mara nyingi dawa za kulevya ni njia ya kutahadharisha wazazi kwamba kuna kasoro. Ikiwa mbalehe ahisi kwamba mama au baba yake hamwangalii, atolewapo dawa za kulevya, zingeweza kuonekana kama utatuzi ajabu wa matatizo yake.”[8]
Mzazi Mkanada mmoja aeleza jinsi yeye na mkewe wapendezwavyo kikweli na masomo ya shule ya binti yao tineja: “Sisi humpeleka Nadine shuleni na kumrudisha kwa gari. Mara nyingi, tukiisha kumchukua, maongezi huanza yakifunua alivyoshinda. Tukigundua jambo zito kidogo, sisi ama huongea naye wakati huo juu yalo ama hulitaja tena kwenye chakula cha jioni au katika mazungumzo ya familia.”[9] Vivyo hivyo wewe waweza kuonyesha hangaiko na upendo wa kweli kwa mtoto wako kwa kuweka wazi mawasiliano.
Uchokozi na Jeuri
Uchokozi ni “moja la matatizo ya shule yasiyoonekana wazi sana,” ataarifu Maureen O’Connor katika How to Help Your Child Through School. Pia ataarifu kwamba “hata huo uwe wawahuzunishaje wadhulimiwao, mara nyingi hawana nia ya kueleza mtu mzima kwa kuogopa kubandikwa jina ‘goigoi.’”[10]
Kwa kusikitisha, walimu fulani huona uchokozi kuwa tabia ya kawaida tu.[11] Lakini wengine wengi hukubaliana na mwelimishi Pete Stephenson, aaminiye kwamba uchokozi ni “namna ya kutendwa vibaya” na kushikilia kwamba “kuuruhusu uendelee hakuwafaidi wachokozi.”[12]
Basi, waweza kufanyaje mtoto wako akidhulumiwa na mchokozi? “Ulinzi wa kwanza,” aandika O’Connor, “lazima uwe ni jumuiya ya watu wazima ambamo [wadhulumiwa] huishi.”[13] Ongea na mwalimu mwenye huruma. Hii itahakikishia mtoto wako kwamba nyote wawili mwaona tabia hiyo ya kutafuta matata kuwa haikubaliki. Shule nyingi zimefuata sera ya wazi dhidi ya uchokozi, ambayo walimu huizungumza peupe darasani.[14]
Natalie alidhulumiwa na wachokozi kwa sababu ya dini yake. “Kwa sababu nilikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova, nilitusiwa, na nyakati fulani vitu vyangu vikararuliwa,” asimulia msichana huyo. Kutatua tatizo, aliongea na wazazi wake, wakadokeza aseme na walimu wake. Akafanya hivyo. “Pia nilichukua hatua ya kwanza kuwapigia simu wazazi wa wanadarasa wenzangu wawili waliokuwa wakinichokoza,” aongezea. “Kwa sababu niliweza kuwaeleza tatizo, sasa mambo ni nafuu. Hivyo nilipata kutumainiwa na walimu wangu na wengi wa wanadarasa wenzangu pia.”[15]
Nyakati fulani, wazazi hugundua kwamba mtoto wao ndiye mchokozi, siye mchokozwa. Hapo, basi, yawapasa wachunguze sana yatukiayo nyumbani. “Watoto wenye tabia ya kutaka matata zaidi huelekea kutoka kwenye familia ambazo wazazi hawatatui mikosano kadiri ya kutosha,” laripoti The Times la London, likiongezea hivi: “Mwenendo wa jeuri ni jambo la kujifunza.”[16]
Jeuri huenea sana mahali fulani-fulani. Msukosuko wa kisiasa ufanyapo iwe ni kama haiwezekani kufanya masomo shuleni, watoto wathaminio hali ya kutokuwamo wameona ni hekima pindi kwa pindi kukaa nyumbani. Lakini matata yatokeapo wakiwa shuleni, wao huepa kwa busara na kurudi nyumbani hadi hali irudiapo shwari.[17]
Ufundishaji Mpungufu
Uwasiliano mwema kati ya mtoto wako na walimu wa mtoto wako waweza kusaidia iwapo ufundishaji mpungufu wasababisha matatizo. “Sikuzote sisi humtia moyo binti yetu awe na mtazamo chanya kuelekea masomo yake,” mume mmoja na mke wake waeleza hivyo.[18] Lakini walimu washindwapo kufanya somo lipendeze, watoto hukosa upendezi upesi. Mtoto wako akiona iko hivyo, mbona usimtie moyo kuongea na mwalimu kwa faragha?
Saidia kijana wako atayarishe maswali ambayo, yajibiwapo, yatarahisisha kuelewa maana ya somo na kujifunza jinsi ya kutumia yafunzwayo. Ingawa hivyo, hiyo tu haihakikishi kuwa na upendezi halisi na wa kudumu katika somo. Mengi yategemea kielelezo chako mwenyewe mzazi. Onyesha wajali kwa kuzungumza masomo na mtoto wako, na ujitolee kumsaidia migawo ya utafiti apewayo na mwalimu.
Shuleni, kuna watoto ambao hutoka nyumba zilizovunjika, au waishio chini ya hali za kutendwa vibaya na kutojaliwa, na hivyo wao hawajitumaini na kujiheshimu. Wao huchangamana na watoto ambao huenda ikawa wana hali bora. Wazazi walio wengi wang’amua yawahitaji wadumu kusaidia watoto wao kukabili matatizo yatokeayo shuleni. Lakini namna gani mishughulikiano ya wazazi na walimu? Yawapasa kusitawisha uhusiano wa aina gani, na jinsi gani?
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Je, Mtoto Wako Hudhulumiwa na Mchokozi?
WASTADI wawashauri wazazi waangalie katika mtoto wao dalili za kuonya. Je, yeye hukataa kwenda shuleni, huepuka wanashule wenzake, huja nyumbani amechubuka au na mavazi yaliyoraruka?
Mtie moyo mtoto wako akuambie lililotokea hasa. Hii itakusaidia ujue kama kweli uchokozi ndilo tatizo. Ikiwa ndivyo, basi ongea na mwalimu mwenye huruma.
Msaidie mtoto wako akabili hali kwa kudokeza kwamba akae karibu na wanadarasa wa kutegemeka na aepuke mahali na pindi ambapo uchokozi waweza kutokea tena. Mtoto mwenye hali nzuri ya ucheshi na ajuaye kutumia maneno ya kuzima matata atafanikiwa mara nyingi.
Epuka kuhangaika mno, na usitie moyo kulipa kisasi.[19]