Wazazi—Iweni Watetezi wa Mtoto Wenu
WAZAZI huwatakia wana na binti zao yaliyo bora. Kwa kweli, mtume Mkristo Paulo aliagiza akina baba walee watoto wao katika nidhamu ya Mungu. (Waefeso 6:4) Mfalme Sulemani wa kale alishauri vijana: “Angalia akuambialo baba na mama yako. Fundisho lao litaboresha tabia yako.”—Mithali 1:8, 9, Today’s English Version.
Basi, shule zatimiza fungu gani katika mipango ya wazazi ya kuelimisha? Na uhusiano kati ya wazazi na walimu wa shule uwe nini?
Mafungu ya Wazazi na Walimu
“Wazazi ndio . . . waelimishi walio wa maana zaidi wa watoto wao wenyewe,” ashikilia Doreen Grant, mwanzishi wa kuchunguza jinsi shule iathirivyo mazingira ya nyumbani.[1] Lakini wewe uliye mzazi, huenda ukaona ni vigumu kukubali wazo hilo.
Labda waona kwamba njia za kufundisha zimebadilika sana tangu ulipoenda shuleni. Siku hizi, shule hukazia masomo yasiyojulikana zamani, kama mafunzo ya vyombo vya habari, elimu ya afya, na elektronififi. Hii imeongoza wazazi fulani wasipashane habari sana na shule.[2] “Kuongea na walimu wa mtoto kwaweza kufanya mtu mzima mwenye kujiamini sana ajihisi kama mtoto wa miaka mitano mwenye kimo cha futi nne tu,” aandika Dakt. David Lewis katika Help Your Child Through School. “Badala ya kuzungumza na walimu juu ya magumu au mahangaiko kwa mamlaka inayolingana, wengine hujiendesha kwa tabia ya kitoto.”[3]
Kwa kweli, wazazi fulani hupashana habari na walimu wa watoto wao matatizo mazito tu yatokeapo. Isitoshe, mara nyingi lengo huwa ni kulalamika. Hata hivyo, wazazi waweza kuchangia sana elimu ya watoto wao, na wengi wamefanya hivyo, kwa kushirikiana na walimu.
Daraka la uzazi lataka uchunguze na kupendezwa na ajifunzayo mtoto wako shuleni. Kwa nini? Kwa sababu walimu hukuwakilisha wewe katika kuelekeza maadili ya watoto wako.[4] Kanuni wadumishazo huathiri wanafunzi wao, maana watoto hutegemea walimu kuwa vielelezo vya kuigwa. Kwa upande wao, walimu walio wengi hufurahia ushirikiano wa wazazi wa wanafunzi wao.
Mwalimu mkuu mmoja kusini mwa Ujerumani aliandikia wazazi hivi: “Imekuwa wazi kwetu walimu, kuliko ilivyokuwa mwaka wowote uliotangulia, kwamba wanafunzi wetu wengi, hasa wale wanaoanza shule [katika Ujerumani, katika umri wa miaka sita], sasa hata wako sugu sana-sana na wasio na huruma, wakosa-adabu kwelikweli. Wengi hawajizuii, wasijue kupambanua wema na ubaya; hawahisi hatia; ni wabinafsi kupindukia, wasiofanya urafiki; nao huchokozeka bila sababu, wakikaba [wengine] koo na ku[wa]piga teke.”
Mwelimishi huyu aliendelea kusema: “Hata ingawa sisi walimu hutatizika zaidi kutokana na hilo, hatutaki kulalamika. Lakini lazima tutambue kwamba, jitihada yote ijapofanywa, shule haiwezi kuelimisha na kulea watoto ikiwa peke yayo. Tungependa kuwatia moyo nyinyi wazazi wapendwa mkate maneno kujihusisha zaidi nyinyi wenyewe katika malezi ya watoto wenu na msiache televisheni wala mitaa iwanyang’anye fungu lenu wenyewe la [daraka la] kukuza utu wao, kuwafundisha viwango vya mwenendo.”—Italiki ni zetu.[5]
Hata walimu wasihipo kuwe na ushirikiano huo, wazazi wengi bado hawataki kusaidia. “Si kwa sababu ya kutojali, kuwa na shughuli mno au kutojitumaini,” adai David Lewis, “bali kwa sababu ya kuamini sana kwamba kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mtoto darasani hakutegemei sana malezi bali hutegemea kabisa uwezo waliozaliwa nao.”[6] Lakini wazo hili si kweli kamwe.
Sawa na vile matatizo nyumbani yaathirivyo kazi ya mtoto darasani, ndivyo maisha mema nyumbani yawezavyo kusaidia mtoto afaidike kabisa na shule. “Hali ya familia huchangia kufanikiwa na kutofanikiwa kielimu kuliko vile shule ichangiavyo,” uchunguzi mmoja wa kielimu waamua hivyo.[7] Kitabu How to Help Your Child Through School chakubali hivi: “Hata mzazi aliye na shughuli nyingi zaidi apaswa kukubali kwamba mtazamo wao—upendezi na kitia-moyo waonyeshacho, na utegemezo wautoao, hata kwa mbali—waweza kuathiri sana maendeleo ya mtoto.”[8]
Basi, ni jinsi gani uwezavyo kupata ushirikiano mwema na walimu wa mtoto wako?
Uwe Mtetezi wa Mtoto Wako
(1) Pendezwa kwa bidii na yale ajifunzayo mtoto wako shuleni. Wakati bora wa kuanza ni wakati mtoto wako aanzapo kuhudhuria shule. Kwa ujumla watoto wachanga zaidi hukubali usaidizi wa wazazi kuliko vile wabalehe waukubalivyo.[9]
Soma na mtoto wako. “Asilimia kama 75 ya kujifunza rasmi,” kulingana na David Lewis, “hufanyika kupitia kusoma.”[10] Hivyo wewe waweza kushiriki fungu kuu katika kusitawisha ufasaha wa kusoma wa mtoto wako. Utafiti wadokeza kwamba maendeleo ya watoto wasaidiwao kusoma nyumbani mara nyingi huzidi ya vijana wasaidiwao na walimu wataalamu shuleni.[11]
Vivyo hivyo, waweza kusaidia mtoto wako kuandika, naam, hata kufanya hesabu. “Huhitaji kuwa bingwa wa hisabati ili kusaidia kwa hisabati za msingi,” aeleza mwelimishi Ted Wragg.[12] Bila shaka, ikiwa wewe mwenyewe wahitaji msaada katika maeneo haya, usiache ukosefu wa ujuzi ukuzuie kutopendezwa kikweli na anayojifunza mtoto wako.
(2) Shauriana na mwalimu wa mtoto wako juu ya mtaala wa masomo. Kwa kusoma ratiba ya masomo ya shule, pata kujua mtoto wako atafundishwa nini. Kufanya hivyo kabla muhula wa shule haujaanza kutakuweka macho kuona maeneo yenye matatizo. Halafu, kuzuru mwalimu kuzungumza jinsi matakwa yako wewe mzazi yawezavyo kustahiwa kutatengeneza njia ya ushirikiano mwema. Tumia vizuri mikutano ambayo shule hupanga ili walimu wafahamiane na wazazi. Katika siku za kutembelea madarasa, zuru shule, na uongee na walimu wa mtoto wako. Mapashano hayo ya habari huwa ya thamani kubwa, hasa matatizo yatokeapo.[13]
(3) Saidia mtoto wako afanye machaguo yake. Yajue masomo yampendezayo na yasiyompendeza mtoto wako. Ongea naye juu ya miradi ifaayo. Shauriana na walimu upate kujua machaguo yote yawezekanayo kufanywa. Wao watajua matatizo yoyote yawezayo kutatiza chaguo la masomo.[14]
Hisia mbaya zaweza kuepukwa kwa uwasiliano wa wazi. Shule nyingi huwakaza wanafunzi wenye akili zaidi wafuatie elimu ya juu zaidi. Lakini wanafunzi wachaguao huduma ya Kikristo kuwa wito wao huepuka kwa ujumla kufanya elimu ndefu ya chuo kikuu.[15] Badala ya hivyo, wakichagua elimu ya nyongeza, wao hupendelea kujifunza masomo yawatayarishayo kujiruzuku. Walimu wenye kudhamiria mambo nyakati fulani huchukua hilo kimakosa kuwa ni katao la mambo yote ambayo wamejaribu kufundisha.[16] Ukiwaeleza walimu kwa subira juu ya mawezekano ya elimu ya ziada iliyo wazi kwa mtoto wako katika mipaka ya upendezi uliochaguliwa na mtoto wako utawapa walimu uhakikishio kwamba wazazi Wakristo hutaka watoto wao waendelee kujifunza.a
Mfikio Ufaao
Waweza kuepuka hangaiko jingi na maumivu ya moyo juu ya elimu ya mtoto wako kwa kukumbuka kwamba ushirika wenye mafanikio hutegemea uwasiliano mwema.—Tafadhali ona lile sanduku lenye kichwa “Hatua za Uwasiliano Mwema Kati ya Mzazi na Mwalimu.”
Badala ya kulalamika na kuchambua, uwe mtetezi wa mtoto wako kupitia ushauriano na ushirikiano na walimu. Ukifanya hivyo, utasaidia mtoto wako afaidike kabisa na shule.
[Maelezo ya Chini]
a Mashahidi wa Yehova wachaguao huduma ya Kikristo kuwa kazi-maisha yao na kutumikia wakiwa wahudumu wa wakati wote huwa na fursa ya kuhudhuria mtaala wa majuma mawili kwenye Shule ya Utumishi wa Painia. Baadhi yao baadaye hustahili kuandikishwa katika mtaala wa miezi mitano wa mazoezi ya mishonari yaendeshwayo na Shule ya Biblia ya Gileadi ya Watchtower kuwatayarisha kuwa wamishonari.
[Sanduku katika ukurasa wa 10]
Hatua za Uwasiliano Mwema Kati ya Mzazi na Mwalimu
1. Pata kuwajua walimu wa mtoto wako.
2. Chunguza mara mbili juu ya uhakika wa hoja zako kabla ya kufanya malalamiko yoyote.
3. Ukiudhika au kukasirika, sikuzote poa kabla hujasema na mwalimu.
4. Kabla hujakutana na mwalimu, andika maswali utakayo kuuliza, na uorodheshe miradi utumainiyo kutimiza.
5. Taarifu msimamo wako kwa uthabiti na wazi, kisha shirikiana na mwalimu kuona ni hatua gani zenye kutumika ziwezazo kuchukuliwa kushinda matatizo yoyote.
6. Jitie katika hali ya mwalimu. Jiulize ungefanya nini ukiwa katika hali yake. Hii itakusaidia utafute masikilizano juu ya tokeo la kuridhisha.
7. Sikiliza na pia useme. Usiogope kuuliza maswali ikiwa huelewi jambo. Ikiwa hukubaliani na lisemwalo, sema hivyo, na ueleze sababu kwa uungwana.
—Msingi ni Help Your Child Through School, cha Dakt. David Lewis.[17]
[Picha katika ukurasa wa 9]
Soma pamoja na mtoto wako
[Picha katika ukurasa wa 9]
Zuru walimu kuzungumza mtaala wa masomo ya shule
[Picha katika ukurasa wa 9]
Saidia mtoto wako afanye machaguo yake