Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g94 10/22 kur. 16-18
  • Kubuni Kazi Katika Nchi Zinazositawi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kubuni Kazi Katika Nchi Zinazositawi
  • Amkeni!—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Biashara ya Chakula—Mtindo wa Kiafrika
  • Kazi za Kuhudumia
  • Kutumia Akili ya Kubuni
  • Kujulisha Tumaini la Kikristo Nchini Senegal
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2000
  • ‘Kuandalia Watu wa Nyumbani mwa Mtu’—Kukabiliana na Huo Ugumu Katika Nchi Zinazositawi
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1996
  • Naweza Kuchumaje Pesa?
    Amkeni!—1998
  • Njoo Ujionee Soko la Kiafrika
    Amkeni!—2010
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1994
g94 10/22 kur. 16-18

Kubuni Kazi Katika Nchi Zinazositawi

NA MLETA-HABARI ZA AMKENI! KATIKA SENEGAL

BABA ya msichana tineja huyo alikufa alipokuwa mtoto, akimwacha mama yake na familia kubwa ya watoto wanane. Kwa kuwa sasa mama yake anazeeka, ni lazima tineja huyo achangie kuiruzuku familia kwa kutafuta kazi. Ndoto yake ya kuendelea na shule imekwisha. Lazima afanye kazi, hata ingawa hana stadi zozote wala elimu rasmi.

Hali zilizo kama hii ni za kawaida katika nchi zinazositawi. Kazi ni haba, hata kwa wale walio na digrii za chuo kikuu. Hata hivyo, kwa kupiga moyo konde na kuwa na akili nzuri ya ubuni, wengi wameweza kujifanyizia kazi. Kazi hizo huenda zisichumie mtu donge nono sana, lakini Biblia husema hivi kwenye 1 Timotheo 6:8: “Tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo.”

Kwa kukumbuka sana ushauri huo wenye kuleta usawaziko, acheni tutazame baadhi ya njia za akili ambazo Wakristo katika nchi zinazositawi wamekuwa wakijihifadhi na kufanikiwa.

Biashara ya Chakula—Mtindo wa Kiafrika

Chakula huhitajika sana sikuzote. Hapa katika Afrika Magharibi, wanawake wenye bidii ya kazi wamepata njia mbalimbali kusisimua za ili kutumia uhitaji huo kujifaidi. Kwa kielelezo, wengine wao hujenga kibanda kidogo karibu na mahali pa ujenzi na kuwapikia wafanyakazi mlo wa adhuhuri. Wengine huwaandalia chakula wale wanaoelekea kazini asubuhi. Wao hupanga meza ndogo yenye mbao za kukalia, huchemsha maji juu ya jiko la makaa, na kuandaa kiamsha-kinywa sahili—kahawa moto pamoja na mkate wa karibuni na siagi. Jioni wao hufungua biashara tena na kuwaandalia wafanyakazi mlo mdogo mwishoni mwa siku. Kuendesha mkahawa wa aina hii humaanisha kupanga ratiba kali, lakini hiyo huwaruhusu wenye bidii wapate fedha za kulipia mahitaji yao.

Pia kuna fursa ya kuuza kumbwe. Wanawake fulani hutafuta mahali penye msongamano wa watu karibu na soko na kukaanga njugu. Fataya—pai za nyama zipakuliwazo katika mchuzi moto—huuzwa kwa urahisi pia. Ndivyo na mikate iliyopachikwa nyama katikati iliyotayarishwa kwa mchuzi wa nyama wenye vikolezo. Vitu hivi huenda sana katika nchi za Kiafrika kama vile Gambia na Mali.

Katika Guinea-Bissau na Senegal, vijana wengi walio Mashahidi wa Yehova hujiruzuku katika huduma ya wakati wote kwa kuoka na kuuza kitu kingine kipendwacho na wengi: keki ndogo-ndogo. Moses, mkaaji wa Dakar, jiji kuu la Senegal, aeleza hivi: “Mke wangu na mimi tulikuwa tukitumikia tukiwa mapainia wa pekee [waevanjeli wa wakati wote] tulipoanza kupata watoto. Sasa nililazimika kutafuta njia ya kuwaruzuku, kwa hiyo wazo likanijia nitengeneze na kuuza keki ndogo-ndogo.

“Nilikuwa na fedha chache za kuanzia, kwa hiyo nililazimika kuwa mwangalifu kupambanua kati ya fedha ambazo ningeweza kuweka kuwa faida na fedha ambazo nilihitaji kurudisha katika biashara kupata vifaa tena, kama unga na mayai. Sasa naweza kuuza keki za kutosha kutunza yaliyo mengi ya mahitaji ya familia yangu ndogo.

“Ili kusaidia, mke wangu, Esther, hushona mavazi ya kike nyumbani. Hii humwezesha kuwa nyumbani pamoja na wavulana wetu wadogo wawili. Kwa hiyo kati ya sisi wawili, twaweza kuitunza familia yetu vizuri sana, tujapoishi katika nyakati ngumu.”

Hapa pana wazo jingine la biashara ndogo: Kwa kuwa watu walio wafanyakazi huwa na shughuli na mara nyingi hawana wakati wa kusafiri mbali kwenda sokoni, wao hujishusha kutumia vibanda vidogo vya kwao viuzavyo matunda au mboga. Wenyeji wa vibanda fulani wana huduma ya kupelekea watu vitu, wakipeleka mboga za karibuni hadi kwenye makao ya wateja. Habari zaweza kusambaa upesi kwamba wewe ni mfuata-haki na kwamba wewe huuza bidhaa bora. Hata hivyo, uwe mwangalifu usitoze fedha nyingi mno, au sivyo watu watarudi upesi kwenye lile soko la kawaida.

Kazi za Kuhudumia

Ikiwa kuuza vitu hakukuvutii, fikiria kutolea watu huduma mbalimbali. Kazi ya nyumbani, kama kusafisha, kupika, na kufua nguo na kuzipiga pasi, sikuzote huhitajika kwa wingi. Na kuna fursa nyingine nyingi sana.

Kwa kielelezo, je, wewe waishi karibu na bahari kuu au karibu na soko la samaki? Kwa nini usijitokeze kusafisha samaki—upesi na kwa gharama ya chini? Vitu uhitajivyo tu ni ubao mzuri na kisu kikali cha kutayarisha samaki. Kuosha magari ni kazi nyingine yenye faida. Ni vifaa gani vihitajiwavyo? Ndoo, maji, sabuni kidogo, na kitambaa kizuri. Katika Dakar, vijana wenye kujali kazi waweza kuonekana kwenye karibu maegesho yote ya magari na kwenye barabara nyingi zilizoezekwa juu wakifanya huduma hii.

Je, maji ya mfereji ni haba katika sehemu yenu ya ulimwengu? Nyakati fulani wanawake hupiga mstari saa nyingi kwenye bomba la maji ya kishirika ili mitungi yao ijazwe. Halafu wao hulazimika kusafirisha karai zao nzito zikiwa juu ya vichwa vyao safari yote ya kwenda nyumbani. Hivyo wengi huwa tayari kulipa mtu fulani atakayewapelekea maji. Mbinu pale ni kufika kwenye bomba la maji mapema asubuhi ili uweze kujaza mitungi yako na kuipandisha juu ya mkokoteni wa kuvutwa kwa mkono au kwa punda. Hapo sasa uko tayari kuyapeleka maji kwenye nyumba za watu au mahali pa kazi.

Je, wewe una masomo fulani ya shule ya kilimwengu? Labda ungeweza kujitolea kuwapa watoto wachanga mafunzo ya ziada katika miisho-juma. Madarasa huelekea kusongamana katika nchi zinazositawi, na huenda wazazi wakawa tayari kulipia mtoto wao ili apokee uangalifu fulani wa kibinafsi.

Ustadi mwingine wenye mafaa ambao huenda ukawa umeupata tayari ni ustadi wa kusuka nywele. Kwa kuwa mitindo ya kusuka nywele hupendwa sana miongoni mwa wanawake katika Afrika, kuna soko kwa watu walio wastadi wa ufundi huu.

Kutumia Akili ya Kubuni

Katika nyakati za Biblia, mke mwenye uwezo angeweza kupata njia za akili za kutokeza mapato. Yasema hivi Mithali 31:24: “Hufanya nguo za kitani na kuziuza; huwapa wafanya biashara mishipi.” Vivyohivyo, wengi katika mabara yanayositawi wamepata mafanikio kwa kujiendeshea kazi ndogo-ndogo za kinyumbani, au biashara ndogo-ndogo. Kwa kielelezo, seremala aweza kuanzisha duka dogo na kutengeneza vibago sahili, mbao za kukalia, na vitu vingine vya kinyumbani. Ni zana zile za msingi sana tu za useremala zihitajiwazo. Ikiwa una stadi fulani za ukulima, labda ungeweza kuanza biashara ya kufuga kuku na kuuza mayai na kuku.

Akili ya kubuni ni takwa la maana la kuanza kazi ndogo-ndogo. Watu fulani wamegeuza mikebe iliyotupwa kuwa mikoba na sanduku zenye kuvutia. Wengine wametengeneza sapatu kutokana na tairi za magari. Na bado wengine wamejenga ndoo kutokana na mipira mikuukuu ya ndani ya tairi. Mawezekano hayana mipaka ila wewe mwenyewe tu ukose kuyawazia.

Katika mabara yanayositawi ustadi na uwazio vyahitajiwa vyote viwili ili kujihifadhi, lakini pia wahitaji subira na mtazamo chanya. Usikate tamaa kwa urahisi. Uwe mwenye kupindikana, tayari kubadili kazi ikiwa lazima. Ikiwa unaanza biashara au unajitokeza kufanya huduma fulani, hakikisha wachunguza sheria na ilani za kwenu. Wakristo watakwa waistahi sheria ya bara.—Warumi 13:1-7.

Kabla ya kujaribu kutolea watu kitu au huduma, jiulize hivi: ‘Ni nini mahitaji na desturi za mahali? Ni nini hali ya uchumi wa mahali? Je, wateja wana uwezo wa kulipia ninachowatolea? Ni wengine wangapi wanaotoa kitu au huduma kama hiyo? Je, kweli nina stadi, nishati, uwezo wa kuchukua hatua ya kwanza, ujitiaji nidhamu, na mwelekeo uhitajiwao wa kupanga mambo vizuri ili kuendesha shughuli hii? Ni kadiri gani ya akiba itakayohusika? Je, nitalazimika kukopa? Je, nitaweza kumaliza kulipa mkopo?’

Swali la Yesu kwenye Luka 14:28 lafaa: “Ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?”—Italiki ni zetu.

Ni kweli, si wote walio na stadi au tabia-moyo ya kujiajiri kazi. Hata hivyo Yehova Mungu aweza kubariki uwezo wako wa kuchukua hatua ya kwanza na kufanya jitihada ya kujibidiisha wakati hilo lifanywapo kwa kusudio lifaalo. (Linganisha 2 Petro 1:5.) Kwa hiyo fanya yote uwezayo kutafuta kazi—hata ikiwa utalazimika kujibunia kazi hiyo!

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kushona mavazi ya kike, kuosha magari, kupelekea watu maji safi, na kusafisha samaki ni baadhi ya njia ambazo watu hujitafutia riziki

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki