Vijana Huuliza . . .
Naweza Kuchumaje Pesa?
“Nataka kazi ambayo itanipa pesa za kutosha.”—Tanya.
VIJANA wengi wana maoni kama ya Tanya. “Nataka pesa ili ninunue gari na niweze kwenda dukani na kununua nguo,” asema kijana aitwaye Sergio. “Sitaki kuwategemea wazazi wangu kwa kila kitu.” Laurie-Ann mchanga anataka kufanya kazi kwa sababu kama hiyo. “Mimi ni msichana, na mimi hupenda kununua vitu,” yeye asema.
Basi, haishangazi kwamba kulingana na gazeti U.S.News & World Report, “vijana 3 kati ya 4 wa shule za upili [Marekani] sasa hufanya kazi baada ya shule na katika miisho-juma.” Kwa kiwango fulani, hii huonyesha mwelekeo usiosawazika wa ‘upendo wa fedha’ ambao umeenea sana katika ulimwengu wa leo wenye kupenda vitu vya kimwili. (1 Timotheo 6:10) Hata hivyo, si vijana wote watafutao riziki ambao huangukia katika utafutaji wa vitu vya kimwili.
‘Fedha ni ulinzi,’ yasema Biblia. (Mhubiri 7:12) Na huenda kukawa na sababu nyingi halali ambazo ukiwa kijana Mkristo huenda ukataka kuchuma pesa.a Kwa kielelezo, Avian mchanga aeleza kwa nini yeye hufanya kazi siku mbili kwa juma: “Huniruhusu kujitegemeza nikiwa painia wa kawaida [mhudumu wa wakati wote].”
Kwaweza kuwa na sababu zinazofanana na hizo zinazokufanya utamani kujipatia kazi ya nusu-wakati. Labda una mradi wa kuhudhuria mkusanyiko wa Kikristo. Au labda unahitaji mavazi zaidi ambayo yangefaa kwa mikutano ya kutaniko. Kwa vyovyote vile, vitu hivi huhitaji pesa. Kweli, Yesu aliahidi kwamba Mungu angeandalia wale ‘wanaotafuta kwanza Ufalme wa Mungu.’ (Mathayo 6:33) Lakini hili halimaanishi kwamba hupaswi kuchukua hatua ya kwanza katika jambo hili. (Linganisha Matendo 18:1-3.) Basi, ni hatua gani zinazoweza kutumika uwezazo kuchukua ikiwa wahitaji kuchuma pesa?
Kuanza
Tuseme kwamba wazazi wako wanakubali ufanye kazi fulani, kazi yako ya kwanza yaweza kuwa kuwafikia jirani zako, walimu, na jamaa zako na kuwajulisha kwamba unatafuta kazi. Ikiwa unaona haya kuwauliza moja kwa moja, waweza tu kuwauliza walifanya kazi gani walipokuwa matineja. Huenda wakakupa maoni yawezayo kutumika. Kadiri watu wengi wajuavyo kwamba unatafuta kazi, ndivyo utakavyopata habari zaidi yenye kutumika na kupata mwelekezo zaidi.
Halafu, jaribu kutafuta matangazo ya magazeti, na ubao wa habari katika maduka makubwa, shuleni kwenu, na sehemu nyingine za umma. “Ndivyo nilivyopata kazi yangu,” asema kijana aitwaye Dave. “Nilitazama katika gazeti la habari, nikawapa habari zangu kwa ufupi, kisha nikawapigia simu.” Je, umewahi kujua kwamba kazi nyingi hazitangazwi? Kulingana na gazeti Seventeen, watu fulani hukadiria kwamba “nafasi za kazi zifikazo tatu kati ya kumi huwa hazipo mpaka mtu anayestahili ajapo na kuuliza juu ya uwezekano wa kupata kazi.” Labda unaweza kumsadikisha mwajiri kwamba anahitaji kukutafutia kazi!
Lakini jinsi gani? ‘Sina uzoefu,’ waweza kufikiri. Fikiria tena. Je, umewahi kumtunza ndugu yako mdogo wazazi wako walipoondoka au kuwatunza watoto wa watu wengine? Hili huonyesha kuwa wewe ni mtu mwenye kuchukua madaraka kwa uzito. Je, umewahi kumsaidia baba yako kutengeneza gari? Hiyo huonyesha kwamba huenda ukawa na kipaji cha umekanika. Je, unajua kutumia taipureta au kompyuta? Au je, ulipata maksi nzuri katika somo fulani la uvumbuzi? Hizi ni hoja nzuri za kuwasadikishia watu wawezao kukuajiri kazi.
Wala usipuuze mambo uyapendayo. Mathalani, ikiwa wewe hucheza ala ya muziki, jaribu kutafuta kazi katika duka la muziki. Bila shaka unapendezwa na bidhaa zilizo katika duka hilo na kwa kweli ungeweza kufaulu kujibu maswali ya mteja.
Kupeleka Ombi la Kazi
Tuseme umeweka miadi kwa mahojiano ya kazi. Angalia mavazi na mapambo yako, kwa kuwa sura yako hueleza mengi kukuhusu. Yaweza kusema “mwenye kuchukua madaraka kwa uzito, safi, mwenye utaratibu”—au kinyume kabisa cha hilo. Biblia ni yenye mafaa inapowatia moyo wanawake Wakristo “wajirembe wenyewe katika mavazi yenye mpangilio mzuri, pamoja na kiasi na utimamu wa akili.” (1 Timotheo 2:9) Shauri hilo hutumika kwa wanaume pia. Kamwe usivalie mavazi ya kimtindo sana au kuvalia kiholela unapoenda kwenye mahoji ya kutafuta kazi, hata iwe kazi hiyo yahusisha nini.
Mtazamo na tabia zako pia husema mengi kukuhusu. Jizoeze Kanuni Bora: Watendee wengine kama utakavyo kutendewa. (Mathayo 7:12) Wahi kwenye miadi yako. Uwe mwenye shauku na chonjo. Uwe na adabu. Bila kujisifu na kutilia chumvi, eleza kwa nini wahisi unastahili kupata hiyo kazi. Taja mambo kihususa.
Wataalamu fulani hupendekeza kwamba ubebe (au upeleke kimbele) habari fupi kukuhusu iliyoandikwa kwa njia nadhifu na iliyopangwa vizuri. Habari hiyo inapaswa kutia ndani jina lako, anwani, nambari ya simu, kazi ya kuajiriwa hususa (kutia ndani masomo yoyote ya kipekee uliyopata), ujuzi katika kazi ya zamani (kutia ndani kazi ya kulipwa na ya kujitolea), stadi za kipekee, mapendezi ya kibinafsi na hobi (haya yaweza kuonyesha uwezo wako), na maelezo mafupi ya kwamba hati za kufuzu zaweza kupatikana zinapoombwa. Pia waweza kuandika orodha nyingine ya majina, anwani na nambari za simu za watu wanaoweza kukupendekeza upate kazi. Bila shaka uhakikishe kuomba idhini yao kimbele. Watu hawa wangeweza kutia ndani waajiri wa zamani, mwalimu, mshauri wa shule, rafiki mkubwa kwa umri—mtu yeyote awezaye kushuhudia stadi zako, uwezo, au tabia zako.
Kujifanyia Kazi ya Kibinafsi
Namna gani ikiwa japo jitihada zako zote unashindwa kupata kazi? Hii ni kawaida katika nchi nyingi. Lakini usivunjike moyo. Kuanzisha biashara yako kungeweza kusuluhisha tatizo hili. Faida zake ni zipi? Unaweza kujipangia ratiba yako na uweze kufanya kazi kwa kadiri kubwa au ndogo upendavyo. Bila shaka, kazi ya kujiajiri hutaka uweze kujimotisha, kujitia nidhamu, na kuwa tayari kuchukua hatua ya kwanza.
Lakini ungeweza kuanzisha biashara ya aina gani? Fikiria ujirani wako. Je, kuna uhitaji wa bidhaa na huduma ambazo hakuna mtu yeyote anayeandaa? Kwa kielelezo, tuseme unapenda wanyama. Ungeweza kujitolea kuosha au kunyoa wanyama rafiki wa jirani yako na kulipwa. Au labda unacheza ala ya muziki. Je, labda ungeweza kuwafundisha wengine kucheza? Au labda kufanya kazi ambayo mara nyingi hudharauliwa na wengine, kama vile kuosha madirisha au kufanya usafi. Mkristo haoni haya kufanya kazi kwa mikono yake. (Waefeso 4:28) Huenda ukajaribu kujifunza stadi mpya. Tafuta vitabu vinavyoandaa mwongozo katika maktaba, au mwulize rafiki akufunze. Kwa kielelezo, Joshua mchanga alijifunza sanaa ya kuandika vizuri. Kisha akaanzisha biashara ndogo ya kutengeneza kadi za mialiko ya arusi na ya karamu.—Ona sanduku “Kazi Unazoweza Kubuni.”
Tahadhari: Usikimbilie biashara yoyote kabla ya kuhesabu gharama na mambo yote yanayohusika. (Luka 14:28-30) Kwanza, zungumzia jambo hili pamoja na wazazi wako. Pia, zungumza na wengine ambao wamewahi kufanya biashara kama hizo. Je, utahitajika kulipa kodi? Je, utahitajika kulipia leseni au vibali? Tafuta habari zaidi kutoka kwa wenye mamlaka wa mahali penu.—Waroma 13:1-7.
Dumisha Usawaziko Wako!
Bila shaka, kuna hatari ya kutafuta kazi nyingi zaidi ya uwezavyo kufanya. Laurie-Ann alisema hivi kuhusu vijana fulani walioajiriwa: “Hawafanyi sana mgawo wa masomo, na huwa wamechoka sana kuweza kusikiliza darasani.” Kweli, katika sehemu fulani za ulimwengu, vijana hulazimika kufanya kazi kwa muda wa saa nyingi ili kusaidia kuruzuku familia zao. Lakini ikiwa hauko katika hali kama hiyo, kwa nini upite kiasi katika jambo hili? Kulingana na wataalamu wengi, kufanya kazi kwa muda uzidio saa 20 kwa juma ukiwa shuleni kunachosha na huleta matokeo yasiyofaa. Wengine hupendekeza kufanya kazi kwa muda unaopungua saa nane au kumi kwa juma.
Ukitumia sana wakati wako, nguvu zako, na kumakinika kwako kwa kazi ya baada ya shule, afya na maksi zako na hasa hali yako ya kiroho itaanza kudhoofika. Ndiyo, si watu wazima tu ambao wamesongwa na “nguvu ya udanganyifu ya mali na tamaa za mambo yale mengine.” (Marko 4:19) Kwa hiyo dumisha usawaziko wako. Solomoni alionya dhidi ya kufanya kazi kupita kiasi, akisema: “Heri konzi moja pamoja na utulivu, kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo.”—Mhubiri 4:6.
Ndiyo, huenda kutafuta pesa kukawa jambo la lazima. Na ikiwa madhumuni yako ya kufanya hivyo yanafaa na ni ya kimungu kama ya Avian aliyetajwa mwanzoni, waweza kuwa na uhakika kwamba Yehova atabariki jitihada zako. Ingawa hivyo, hakikisha kwamba, hufungwi sana na kazi yako hivi kwamba unasahau “kuhakikisha mambo yaliyo ya maana zaidi,” yaani, masilahi ya kiroho. (Wafilipi 1:10) Ingawa pesa zaweza kuwa “ulinzi,” ni uhusiano wako na Mungu utakaokufanya ufanikiwe kikweli.—Mhubiri 7:12; Zaburi 91:14.
[Maelezo ya Chini]
a Makala “Vijana Huuliza . . . ” katika matoleo ya Amkeni! ya Novemba 22, 1990 (la Kiingereza); Desemba 8, 1990 (la Kiingereza); na Septemba 22, 1997 huonyesha faida na hasara za kazi za baada ya shule.
[Sanduku katika ukurasa wa 22]
Kazi Unazoweza Kubuni
• Kusafisha madirisha
• Kuuza au kupelekea watu magazeti ya habari
• Kuondoa theluji
• Kulima bustani au kukata nyasi
• Kutunza watoto
• Kulisha, kutembeza, au kuosha wanyama rafiki
• Kupaka viatu rangi
• Kushona au kupiga nguo pasi
• Kupanda mazao na kuyauza
• Kufuga kuku au kuuza mayai
• Kupiga taipu au kutumia kompyuta
• Kutumwa
• Kugawa vitu
• Kufundisha muziki au masomo mengineyo
[Picha katika ukurasa wa 21]
Kazi ipitayo kiasi yaweza kufanya maksi zako zishuke