Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 4/22 kur. 25-27
  • Tumeoana Mapema Mno—Je, Tunaweza Kufaulu?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Tumeoana Mapema Mno—Je, Tunaweza Kufaulu?
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Je, Hakuna Njia ya Kutokea?
  • Msimamizi Ni Nani Hapa?
  • Matatizo ya Fedha
  • Tunaweza Kuongea?
  • Biblia Inasema Nini Kuhusu Ndoa?
    Maswali ya Biblia Yajibiwa
  • Fanya Ndoa Yako Iwe Muungano Wenye Kudumu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Je! Ndoa Yako Yaweza Kufanikiwa?
    Kupata Faida Zote za Ujana Wako
  • Jenga Ndoa Imara na Yenye Furaha
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—2015
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 4/22 kur. 25-27

Vijana Huuliza...

Tumeoana Mapema Mno—Je, Tunaweza Kufaulu?

“Tulikuwa tukipeana miadi ya kijinsia tangu nilipokuwa na miaka 16. Nikiwa na miaka 18 tulioana. Ilielekea kuwa shwari—daima dawamu! Lakini baada ya karibu miezi minne, nilikasirishwa sana chini ya msongo.” —Tonya.a

NDOA kwenye umri wowote yaweza kuwa yenye kusumbua. Biblia yasema hivi: “Wale wanaooa watakuwa na umivu na msononeko.” (1 Wakorintho 7:28, The New English Bible) Lakini kwa wengi wanaoingia katika kifungo cha ndoa katika “uzuri wa ujana,” mara nyingi umivu na msononeko huonekana kuwa vima visivyovumilika.—1 Wakorintho 7:36.

Hili ni kwa sababu matineja bado wanakua; ni mara haba sana wao huwa tayari kuchukua fungu la mume au mke. Dakt. Jane K. Burgess aonelea hivi: “Vijana huwazia mno kuhusu ndoa. Wao huwa hawafikirii kuhusu aina ya kazi na jitihada za kila siku ambazo ndoa yenye mafanikio huchukua.” Mambo ya hakika ya ndoa basi yaweza kushtua mume na mke kama kofi usoni.

“Watazamia kila kitu kiwe shwari na murua, kama vile fantasia,” asema kijana Kim. “Ingawa hivyo, uupya wa kuwa bwana na bibi arusi unafifia, na kisha ni kupika, kuosha vyombo, kununua vyakula, na kufua nguo—mume wako akiwa amekaa kwenye kochi. Hakuhitaji kamwe kufanya kazi hizo kwani mama yake alimfanyia yote hayo. Mnapopeana miadi ya kijinsia kamwe hufikirii kuhusu kuchoka na kuchokozeka. Na unapokuwa na mimba, yote yanakuwa mabaya mara kumi!”

Mara nyingi, matineja huoa haraka bila kuangalia matokeo. “Niliolewa na mwanamume niliyefikiria kuwa Mkristo wa kweli,” akumbuka Helen. “Kwa sababu ya ukosefu wangu wa uzoefu, sikupata kumjua vizuri vya kutosha. Baada ya miezi kumi ya ndoa, singeweza kumvumilia zaidi kwa sababu ya tabia zake zisizo za Kikristo.” Kufeli kwa ndoa ya Helen si jambo la ajabu. Katika Marekani, ndoa nyingi za matineja hufeli mnamo miaka mitano.

Japo tarakimu zenye kutisha, mamilioni ya matineja wamejitumbukiza katika muungano wa ndoa. Labda wewe ni mmoja wao. Ikiwa ndivyo, huenda tayari ukahisi kushindwa na misongo ya ndoa.

Je, Hakuna Njia ya Kutokea?

Hata ingawa kuoa ukiwa kijana huenda kusiwe busara, si lazima kuwe ni dhambi. Ndoa yaheshimika machoni pa Mungu. (Waebrania 13:4) Ni kweli, baadhi ya hali zenye kupita kiasi huenda zihalalishe mtengano ama talaka. (Mathayo 19:9; 1 Wakorintho 7:12-15) Ingawa hivyo, kwa ujumla, Mungu hutaka kwamba mume na mke washikamane. (Mathayo 19:6) Ingawa hilo huenda lionekane kuwa kitanzi, pia lamaanisha kwamba Mungu ataka ufanikiwe.

Mume mmoja tineja asema hivi: “Ni kuchelewa mno kuuliza, ‘Je, nilikuwa mchanga mno? Kwa kweli sisi twafaana?’ pamoja na zile dhana zote za badala. Umeoa!” Kwa hivyo badala ya kusikitikia masaibu yako, kwa nini usijaribu kutafuta njia fulani ili kufanya ndoa yako itende kazi?

Msimamizi Ni Nani Hapa?

Biblia huambia waume na wake hivi: “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu . . . Mume ni kichwa cha mkewe.” (Waefeso 5:22, 23) Hata hivyo, mwanamume mchanga ametumia maisha yake yote chini ya uvuli wenye ulinzi wa mama na baba, kuwa kichwa cha familia kwaweza kuwa daraka lenye kuhofisha.

Mke mmoja mchanga akumbuka kuhusu mume wake: “Tom hakutaka niende mahali popote nikiwa peke yangu. Nilijihisi kunasika, kufungiwa. Alifikiri kwamba wakati wowote nilipojaribu kumwuliza, ulikuwa ushindani kwa mamlaka yake.” Kwa upande ule mwingine, wake wengine huona vigumu kuwaona waume zao wachanga kuwa kichwa chao. Wengine wanaudhika wakati mume anapotoa uamuzi, wakikataa kushirikiana wanapokosa kuafikiana na uamuzi.

Hili laweza kusumbua mno ikiwa wewe ni mume mchanga. Lakini kwa hakika hakuna uhitaji wa kuvurugika kwa sababu tu mwenzi wako hatii kwa wepesi kila amri yako. Itachukua muda kwa mke wako kujihisi salama chini ya ukichwa wako. Kwa wakati huu, fanyia kazi kujipatia staha yake, si kwa kujaribu kumdhibiti, bali kwa kuongoza na kujaribu kufanya maamuzi yaliyosawazika.—Linganisha 1 Wakorintho 16:13.

Biblia hutuhimiza zaidi hivi: “Kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu.” (Warumi 12:10) Ndiyo, stahi mke wako kwa kuweka mapendezi yake mbele ya yako. (Wafilipi 2:4) Mpe uhuru wa kutenda, ukimtendea kama mwenzi anayestahiwa, si kama mtumwa. (Ona Malaki 2:14.) Inapowezekana, wasiliana naye maamuzi makubwa yanapolazimika kufanywa. (Mithali 13:10) Hili litamrahisishia kujitiisha chini ya ukichwa wako.

Iweje, ikiwa wewe ni mke mchanga? Huenda nyakati fulani ikajaribu saburi yako kujinyenyekeza kwa mume mchanga ambaye hana ukomavu maamuzi yake yanapoaibisha ama kukosa ubora. Hata hivyo, kumfokea ama kuasi hakutasaidia kuboresha daraka lako. “Kadiri alivyonifokea, ndivyo nilivyozidi kuwa mnyamavu,” akakiri mume mmoja mchanga. Jaribu kuonyesha heshima kwa kumpa nafasi ya ukosefu wa uzoefu. Huenda aitikie kwa kuonyesha staha zaidi kwa maoni yako. Akifanya uamuzi unaokuudhi—lakini hauvunji sheria yoyote ya maadili—kwa usahili kwa nini usishirikiane nao? ‘Hekima itokayo juu . . . iko tayari kusikiliza maneno ya watu.’ (Yakobo 3:17) Kwa kuwa mwenye kuunga mkono ukichwa wake, unaweza kumsaidia kuwa mwenye kufaa zaidi.

Matatizo ya Fedha

Wengine husema kwamba tatizo nambari moja la waume na wake walio wachanga ni fedha. Mara nyingi waume na wake hushangaa kujua kiasi wagharimikacho ili kuishi. Kwa kielelezo, Ray na Lora, “hawakuwa na chakula wala fedha” baada ya arusi yao. “Tulilala sakafuni,” wao wakiri. Brad na Tonya walipatwa na misongo ya kiuchumi ifananayo na hiyo Brad alipofutwa kazi—na Tonya alilazimika kugharimia matumizi.

Ingawa ni kweli kwamba vijana mara nyingi huwa na tatizo la kupata kazi inayolipa mishahara mizuri, matatizo ya fedha nyakati fulani huwa ni tokeo la usimamizi mbaya wa fedha. Ebu fikiria mwanamke mchanga anayesema hivi: “Mimi hutumia fedha mpaka ninabaki mikono mikavu na kisha nawa bila zozote kwa ajili ya juma la mwisho la mwezi.” Waume na wake wengine huumia kwa kukosa kuwasiliana. “Niliondoka nami nikanunua gari bila kuzungumza na mke wangu,” akiri mume fulani aitwaye Jake. “Kwa kweli tulichohitaji ni fanicha,” alalama mke wake.

Je, hilo lasikika kuwa lenye kufahamika kwako? Basi, labda hujaondoa “vitabia vya kitoto” kuhusu kushughulika na fedha. (1 Wakorintho 13:11) Je, wewe hufanya ununuzi wako kwa kushtukia? Basi jifunze kufanya orodha ya ununuzi, na ushikamane nayo. Zungumza ununuzi wako mkubwa. (Mithali 15:22) Andika matumizi yako, na ubuni matumizi yatumikayo.b Kufanya hivyo kwaweza kukupunguzia mikazo mingi ya kifedha.

Tunaweza Kuongea?

Hilo latuleta kwa kile wengine hukiita tatizo nambari mbili miongoni mwa waume na wake wachanga: uwasiliano. Waume na wake wengine hujirudia kwenye pango la ukimya. Wengine hujiingiza katika jeuri ya maneno. “Mabishano makubwa ambayo [tu]likuwa nayo yalikuwa juu ya mambo ya kishenzi,” akumbuka Sylvia, mtalikiwa fulani. “Mambo kama vile kuacha kwake viatu vikiwa vimetapakaa nyumbani, ama kuchukua kwangu donge kutoka sahani yake ya mlo mkuu.”

Kutoelewana na kutoafikiana kwa kweli kutatokea. Lakini “uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano” kwa kweli hubomoa ndoa. (Waefeso 4:31) Iweni na zoea la kuzungumza mambo wakati kuudhika kukiwa kungali kudogo. Mfanyapo hivyo, shambulieni tatizo—si mtu. Mambo yanapovuka mpaka, msichochee bishano. “Moto hufa kwa kukosa kuni,” yasema Mithali 26:20. Baadaye, wakati nyinyi nyote mnapokuwa mmetulia, jaribuni kuzungumza mambo tena.

Uwasiliano mzuri pia ni ufunguo wa kusuluhisha tatizo jingine lililo la kawaida: kutoridhika kingono. Nyakati nyingine mume na mke wachanga kwa kweli wamechoka mno kutokana na kawaida yao mpya kiasi cha kukosa kufurahia uhusiano wa ndani wa kindoa. Kitabu Building a Successful Marriage chasema hivi: “Waume na wake huingia katika ndoa wakiwa na uelewevu usiofaa kuhusu fungu na kazi ya ngono.” Wakiwa wamehadaiwa na propaganda za ulimwengu, waume na wake wengi huja kupata matazamio yasiyo hakika katika jambo hili. Ubinafsi na kukosa kujidhibiti pia huchangia. Uwasiliano wa wazi, pamoja na wakati na subira, ni muhimu. Wakati kila mmoja ‘atafuta faida . . . ya mwenzake,’ ngono mara chache sana huwa tatizo zito.—1 Wakorintho 10:24.

Kwa wazi basi, ndoa si kwa ajili ya watoto. Ikiwa tayari umeoa, haimaanishi utafeli. “Mwaka wangu wa kwanza wa ndoa kwa kweli ulikuwa na msukosuko,” asema mwanamke mmoja aliyeolewa. “Lakini kwa sababu ya kutumia kanuni za Biblia, sasa twaishi maisha ya ndoa yenye uradhi na furaha.” Nawe waweza.

[Maelezo ya Chini]

a Baadhi ya majina yamebadilishwa.

b Makala “Panga Matumizi ya Pesa Zako—Kwa Njia Iliyo Rahisi!” iliyotokea katika toleo letu la Aprili 8, 1986, lina madokezo fulani yenye kusaidia.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kumwunga mkono mwanamume mchanga katika fungu lake la kimume kwaweza kutokeza mazuri katika yeye

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki