Mchwa—Rafiki au Adui?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KENYA
“KUMBE! Mchwa!” Ndivyo alivyopaaza sauti mhudumu mmoja Mkristo huku yeye na kikundi cha wengine wakinyanyua kidimbwi cha mbao kiwezacho kuchukulika. Walitumaini kukitumia kuwa kidimbwi cha ubatizo kwenye kusanyiko la mzunguko la Mashahidi wa Yehova katika Kenya. Hata hivyo, kwa fadhaiko lao, walikuta kwamba sehemu kubwa ya mbao ilikuwa imeliwa. Hiyo ikitokeza wonyesho wake wa mfadhaiko.
Huenda hakuna mdudu mwingine ambaye mara nyingi huhusianishwa na uharabu wa mali kama mchwa aliye mdogo sana. Lakini je, mdudu huyu ni adui wa mwanadamu kweli? Katika kujibu, acheni tumtazame mchwa kwa ukaribu zaidi.
Ngome ya Mchwa
Katika Kenya, mara nyingi mtu huona makao ya mchwa yenye kupanda juu. Haya ni maumbo yaliyo kama dohani yanayotokeza kufikia urefu wa kuanzia meta tano hadi sita juu ya ardhi. Vichuguu, vifananavyo na ngome ya saruji, hutengenezwa kwa umakini mwingi hivi kwamba mchwa wameitwa waunda-majengo stadi. Je, hakupingi mawazo kufikiri kwamba wadudu wadogo mno wangeweza kujenga ngome zenye kupendeza jinsi hiyo, hata ingawa si wepesi katika kutembea—na ni vipofu?
Ndani ya kichuguu mna mizingo iliyopangwa ya vitundu na mahandaki. Jiji hili lenye shughuli nyingi pia lina mfumo ufaao wa uondoaji maji, upishaji hewa safi, na hata usawazishaji wa hewa. Hewa yenye joto hutoka kupitia vishimo vidogo vilivyoko juu ya kichuguu. Hewa yenye ubaridi huja kupitia chini. Upishaji baridi zaidi hufanywa kwa mfumo sahili wa kuvukiza: Mchwa hupulizia kuta zao kwa maji kwa kuzitemea mate. Maji yavukizapo, hufanya hewa kuwa baridi na kusaidia mzunguko wa hewa. Hivyo makao ya mchwa hubaki kwenye digrii 30 Selsiasi saa 24 kwa siku!
Jamii ya Mchwa
Ya kushangaza hata zaidi ni jamii ya mchwa. Vichuguu fulani vya mchwa hukaa jumuiya kubwa zenye ustadi, au milki, ikifikia idadi ya hadi wakazi milioni tano. Mbali na kuwa wenye fujo, milki ni kielelezo cha ustadi. Familia ya mchwa hufanyizwa kwa tabaka tatu, vibarua, askari, na wazaaji. Vibarua hufanya ujenzi hasa wa kichuguu, wakitumia mate yao kuwa saruji.
Askari huwa washiriki wa familia wakali mno. Wakiwa na mataya yenye nguvu na meno makali, wao hulinda ngome kutokana na maadui, kama vile askari siafu. Wao pia hutenda kama walinzi ili kulinda vibarua wanaotembea nje ya kichuguu kutafuta chakula. Ikihitajika, askari hugeukia vita ya kikemikali; tezi maalumu hutenda kama bastola ya kurushia maji, ikitoa kimiminiko chenye kufisha.
Askari hulipwaje kwa utumishi wao? Yaonekana mataya yao ni makubwa mno hivi kwamba hawawezi kutafuna chakula ili kujilisha. Kwa hiyo askari ahisipo njaa, husugua kichwa cha kibarua kwa kipembe chake. Hilo humaanisha, “Nilishe!” Kibarua huitikia kwa kuweka chakula kilichotafunwa katika mdomo wa askari.
Katika chumba cha kifalme, kilichofunikwa na kiza, huishi wazaaji—mfalme na malkia. Malkia ni jitu akilinganishwa na mwenzi wake mdogo mno. Fumbatio lake, lililofura kwa mayai, ni uthibitisho wa nguvu zake za uzaaji zisizo za kawaida. Yakadiriwa kwamba aweza kutaga mayai kuanzia 4,000 hadi 10,000 kwa siku. Si ajabu kwamba watu fulani wamemwita malkia huyo “mashine inayojiendesha ya kutaga mayai.”
Ingawa hivyo, hakuna usiri mwingi kwa wenzi hawa wa kifalme kwa kuwa wanahudumiwa na kikundi cha vibaruamchwa. Hawa humzingira malkia, wakishughulikia mahitaji yake ya wakati huo na kumwandalia chakula. Mayai yatokezwapo, vibarua huyabeba kati ya mataya yao hadi kwenye chumba cha kuangulia.
Marafiki au Maadui?
Ingawa ni watu wachache wangekataa kwamba wadudu hawa ni wenye kuvutia, wengi bado huwaona kama wadudu waharabu—maadui! Dakt. Richard Bagine, mkuu wa Idara ya Zuolojia ya Wanyama Wasio na Uti wa Mgongo ya Hifadhi ya Kitaifa ya Kenya, aliambia Amkeni! hivi: “Ni kweli kwamba mchwa huonwa na watu kuwa mojapo wadudu waharabu zaidi ya wote. Lakini wanasayansi huona mchwa kwa njia tofauti. Katika makao yao ya asili, mchwa ni washiriki muhimu wa jumuiya ya mimea na wanyama.
“Kwanza, wao huvunja-vunja mimea iliyonyauka hadi kuwa misombo sahili. Katika njia hii, mchwa hufanyiza upya lishe ambayo mimea yahitaji. Pili, wao ni chanzo muhimu sana cha chakula. Wao huliwa na karibu kila aina ya ndege na mamalia wengi, wanyama-watambazi, amfibia, na wadudu wengine. Watu wengi katika magharibi na kaskazini mwa Kenya pia hufurahia ladha yao iliyo nyingi na tamu; wao wana shahamu nyingi na protini. Tatu, wao husaidia kufanyiza mchanga. Mchwa huchanganya mchanga wa chini na wa juu wanapojenga na kurekebisha viota vyao. Wao huvunja-vunja vipande vikubwa vya mimea iliyonyauka hadi kuwa vipande vidogo zaidi, wakifanyiza mboji. Wakitembea ndani ya mchanga, wao hutengeneza vipitio kwa ajili ya hewa na maji yanayohitajiwa na mizizi ya mimea. Hivyo mchwa huboresha umbo la mchanga, mfanyizo, na rutuba.”
Kwa nini basi, mchwa huvamia makao ya binadamu? Dakt. Bagine asema hivi: “Kwa kweli, watu wameingia katika makao ya asili ya mchwa na kuondoa nyingi za rasilimali za mimea zitumiwazo na mchwa. Mchwa lazima wale ili waishi, na kwa kawaida hujilisha kwa mimea iliyonyauka. Wanaponyang’anywa mimea hii, mchwa hujilisha kwa majengo yaliyofanywa na wanadamu, kama vile nyumba na ghala za nafaka.”
Kwa hiyo ingawa mchwa nyakati fulani aweza kuonekana kuwa mdudu mharabu, kwa kweli yeye si adui yetu. Kwa hakika, mchwa ni kielelezo chenye kugusa moyo cha ustadi wenye kutokeza wa uumbaji wa Yehova. (Zaburi 148:10, 13; Warumi 1:20) Na katika ulimwengu mpya wa Mungu unaokuja, mwanadamu ajifunzapo kuishi kwa upatano na ulimwengu wa wanyama, bila shaka atakuja kuona mchwa mdogo sana kuwa rafiki, si adui.—Isaya 65:25.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kichuguu halisi cha mchwa kilicho kama kasri
Picha ndogo: Vibaruamchwa
[Picha katika ukurasa wa 18]
Askarimchwa, na kichwa chake kikubwa na tezi ambazo hutokeza kemikali zenye kufisha, akiwa tayari kutetea milki ya mchwa
[Picha katika ukurasa wa 18]
Malkia, fumbatio lake likiwa limefura kwa mayai
[Picha katika ukurasa wa 18]
Malkia akiwa na kikundi chake cha watumishi