Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g95 10/22 uku. 20
  • Kusuluhisha Tatizo la Taka Nyingi—Kwa Uozeshaji

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kusuluhisha Tatizo la Taka Nyingi—Kwa Uozeshaji
  • Amkeni!—1995
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kiwanda cha Kipekee cha Kubadili Hali ya Taka
  • Mazoea ya Kutupatupa Vitu
    Amkeni!—2002
  • Wadudu Wanaoondoa Takataka kwa Ustadi
    Amkeni!—2002
  • Je, Kuna Suluhisho?
    Amkeni!—2002
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1995
g95 10/22 uku. 20

Kusuluhisha Tatizo la Taka Nyingi—Kwa Uozeshaji

NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA FINLAND

TAKA ya wanadamu inapozidi kuongezeka, inatokeza moja ya matatizo magumu mno ya muhula wetu. Tekinolojia ya kisasa, ingawa ni yenye bidii sana katika kutokeza taka, huonekana ikitatanishwa inapohusu kuiondoa. Masuluhisho ya kawaida ya muda mrefu yamejaa matatizo. Kwa kuwa kurundika taka mahali pamoja kwaweza kuchafua maji ya ardhini yaliyo karibu, nchi nyingi zimelazimisha mahali pa kurundikia taka pakomeshwe. Na kuchoma taka hiyo kwaweza kutokeza kemikali zenye sumu na kuacha jivu, yote hayo yakitokeza matatizo yayo yenyewe ya kuyaondolea mbali. Kwa hiyo tanuru za kuchomea taka za tekinolojia ya hali ya juu hazitumiwi katika maeneo mengi.

Ni kibadala kipi kinachobaki? Wengine wanadokeza njia ya asili ya kuondoa uchafu mkavu—namna ya “moto” wa kibiolojia uitwao uozeshaji. Kama moto, uozeshaji huvunja mata ya kikaboni kuwa vitokezwaji kadhaa, ikitokeza joto katika taratibu hiyo. Vitokezwaji hivyo vya uozeshaji vyaweza kuwa vyenye manufaa. Hizo gesi na joto vyaweza kutumiwa kuwa vyanzo vya nishati. Na kitokezwaji kikavu, mboji, ni mbolea ya mchanga yenye thamani katika kilimo.

Uozeshaji ni jambo maarufu lenye kuenea sana. Kwa kielelezo, katika Finland, mji wa Korsholm na jiji jirani la Vaasa yameanzisha kiwanda cha hali ya juu cha kufanyia kazi taka kupitia njia ya uozeshaji. Wabuni wa kiwanda hicho waligundua njia ya busara ya kusuluhisha matatizo mawili ya eneo hilo kwa wakati mmoja. Changarawe kwa ajili ya ujenzi na barabara ni rasilimali isiyopatikana kwa urahisi. Na kwa sababu ya hilo, lile wazo la kupasua katika mwamba shimo pana lenye urefu wa meta 40 likazuka. Baada ya kutokeza kiasi kikubwa mno cha changarawe, shimo hilo lilifanyiza mahali pafaapo kwa ajili ya kifaa kikubwa ambacho katika hicho bakteria huvunja-vunja dutu zenye kudhuru ili kufanya uchafu wa manispaa usiwe wenye kudhuru. Kuzingirwa na mwamba mgumu husaidia kifaa hicho kidumishe halijoto ileile ambayo ni muhimu kwa taratibu ya uchachushaji.

Tokeo ni nini? Kwa kiwango kikubwa, kiwanda hiki cha kisasa kilisuluhisha tatizo la taka la eneo hilo. Hicho hupunguza kiasi cha taka kwa asilimia 75 na uzito kwa asilimia 66. Hili lawezekanaje? Ebu tuzuru kiwanda hicho.

Kiwanda cha Kipekee cha Kubadili Hali ya Taka

Picha ya kwanza tunayopata baada ya kufika ni kwamba mahali hapa hapafanani na mahali pa mirundiko ya taka zote. Hakuna panya, na hakuna harufu ya uvundo. Hapa ushughulikiaji wa uchafu waonekana kuwa utendaji mwingine wenye utokezaji.

Meneja wa hicho kiwanda kwanza atuonyesha chati inayoeleza kile kitukiacho katika hicho kiwanda. Taratibu yenye hatua mbili hupunguza wingi na kiwango cha taka—kwanza kufanyiza mbolea kisha kuivundisha. Katika uozeshaji, huo uchafu unavunjwa-vunjwa kikemikali katika kuwapo kwa hewa; katika uvundishaji, huo huchachuka bila kuwapo kwa hewa. Lakini kabla ya yoyote ya taratibu hizi kuanza, uchafu huo hupondwa-pondwa.

Kutoka kwenye dirisha la chumba cha kudhibitia vifaa vya kiwanda, twaona lori la kubeba taka likirudi nyuma kupitia mlango mkubwa. Hilo laimwaga taka ndani ya shimo lililo na umbo la dohani ambapo mshipi fulani waimwaga ndani ya kiraruzi. Vitu vikubwa zaidi, kama vile fremu za baiskeli, magurudumu ya gari, mabomba ya kutolea moshi, na vipande vingi vya plastiki, hutolewa na kreni. Mkaribishaji wetu aeleza kwamba friji na friza kuukuu ziletwapo, hupelekwa kurekebishwa na baadaye huuziwa nchi zinazoendelea.

Baada ya upondaji wa kwanza, uchafu hupitia chungio kisicho chororo ambapo chochote kilicho kidogo kuliko milimeta 50 hupita. Hii huwa nusu hivi ya taka, na hupitia hatua ya kwanza ya kuvunjwa-vunjwa kwayo kwa kibiolojia, uozeshaji. Hili hutukia katika tangi kubwa ambapo uchafu uliopondwa unachanganywa na tope kutoka kwenye kiwanda cha jiji cha kutia dawa kinyesi.

“Tulipokuwa tukianzisha taratibu hii, sikuzote tulikuwa tukifikiria mazingira,” asema mkaribishaji wetu, “kwa hiyo, sisi hata hutenga vumbi linalotokana na upondaji. Isitoshe, tunapuliza hewa ndani ya tangi la uozeshaji ambapo mchanganyiko wa uchafu na tope huchujwa na kupashwa joto hadi digrii zipatazo 40 Selsiasi. Hewa inayotoka ingenuka vibaya mno kwa sababu ya kuoza kama hatungeipitisha katika kichujio kwanza.”

Baada ya siku moja au mbili katika tangi la uozeshaji, vitu hivyo huingia katika kitendanishio kikuu cha biogesi chenye kimo cha meta 40. Ni nini kinachotendeka hapa? Vifanyizo vya kikaboni vya mchanganyo huu huvunjwa na viini vidogo mno ambavyo vyaweza kuishi katika mazingira haya yasiyo na oksijeni. Hatua hii ya hiyo taratibu huitwa, kisahili sana, uvundaji. Hiyo huchukua siku 15 kukiwa na digrii 35 Selsiasi. Vitokezwaji vya mwisho ni biogesi na mboji, ambayo ni asilimia 85 hadi 90 maji. Mengi ya maji haya hukamuliwa na kurudishwa ndani ya kitendanishio.

Lakini ni nini kilichotukia kwa ile nusu ya taka ambayo haikupita chungio? Mwongozi wetu asema kwamba sehemu hii yaweza kuwaka moto kwa sababu hasa ina karatasi na plastiki. Lakini ili kuchoma uchafu huo kwa njia salama zaidi ingehitaji halijoto ya zaidi ya digrii 1,000 Selsiasi—na hakuna tanuri aina hiyo katika ujirani huo. “Ndiyo sababu tunaponda-ponda uchafu uliobaki mara nyingine tena na kuurudisha katika hiyo taratibu,” yeye asema. “Ni kweli kwamba hiyo taratibu ya kibiolojia haiwezi kuharibu kabisa plastiki, lakini uchafu huo sanasana huwa karatasi, ambazo mwishowe huwa msombo wa mboji.”

Taratibu hii inayotatanisha hutokeza nini? Mkaribishaji wetu ajibu: “Kwa msingi tunapata vitu viwili, msombo wa mboji na biogesi. Tunauza mboji kwa maeneo yanayokuza miti na nyasi, na mahali pa kuzikia taka ambapo hapatumiwi. Kuna uhitaji mkubwa wa mboji sasa kwa kuwa mahali pengi pa kurundikia taka pamefungwa. Kwa wakati ujao tutaona ikiwa itatumiwa katika kilimo baada ya kutoa chupa na plastiki. Hiyo biogesi hufanyizwa kwa asilimia 60 methani na asilimia 40 kaboni dioksaidi. Katika ubora huwa ileile na gesi asili na hutumika katika njia sawa. Tuna mfumo wa mabomba ya kuisambaza hadi kwenye viwanda vilivyo karibu zaidi.”

Namna gani tatizo la vyuma vizito katika taka na tope? Mkaribishaji wetu aendelea hivi: “Vyuma hivi vizito hukusanywa majini. Kwa hivyo, tunanuia, kwa wakati ujao, kupata kifaa cha kuondolea vyuma vizito kutoka majini. Kisha kitokezwaji chetu kitakuwa kizuri kwa makusudi yote. Tunaposema juu ya wakati ujao, lazima niwaeleze kuhusu tamaa yangu, ambayo ni kwamba nyumba zote zingetenganisha taka zao ili tusipate wala chupa, plastiki, wala chuma. Vyote hivyo vyaweza kutengenezwa upya. Hata vitambaa vya kuundwa kutokana na vitu visivyo vya asili, plastiki na mipira vyaweza kutengenezwa upya.”

Kiwanda hicho kina uwezo wa kushughulikia uchafu unaotokezwa na watu 100,000. Hili ni la maana katika Finland. Kufikia mwaka 2000, nchi hii yapanga kutumia nusu ya taka yayo—ikiwa ama mali ghafi au nishati.

Ziara yetu imetupa ithibati ya kweli kwamba inawezekana kufanya jambo fulani kuhusu tatizo la taka. Kila mmoja wetu anaweza kushirikiana na sheria zozote za utengenezaji-upya wa vitu ambavyo vinatumika mahali tunapoishi. Hata hivyo, kabla ya kumwacha mwongozi wetu, tunauliza ikiwa kuna viwanda vingi vinavyoshughulikia taka kama kifanyavyo hiki. “Hilo ni gumu kusema,” ajibu mwongozi wetu. “Sijui kuhusu kiwanda chochote kama hiki. Labda matatizo ya taka ni makubwa sana katika sehemu nyingi hivi kwamba hakuna mtu amedhubutu kujaribu hili.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki