Mmea Wenye Rangi Nyangavu, Ulio na Matumizi Mengi
MAFUTA ya dizeli, chakula cha ng’ombe, sabuni na siagi vinashiriki nini? Katika mabara fulani vitu hivi vyote hutokezwa kwa msaada wa mmea aina ya rape, wenye maua ya manjano nyangavu.
Mmea huu wenye rangi nyangavu wa familia ya haradali, unaokuzwa katika sehemu za Ulaya, Asia, na Amerika Kaskazini, huthaminiwa hasa kwa mbegu zao zenye mafuta mengi. Kufikia asilimia 40 ya mbegu ya rape ni mafuta, ambayo yanaweza kutumiwa kwa vitu vingi.
Mafuta mengi ya mbegu ya rape—labda hata asilimia 90—hutumiwa kwa kutengeneza chakula. Hutumiwa katika kutengeneza siagi, biskuti, supu, aisikrimu, na vyakula vitamu-vitamu. Lakini mafuta ya mbegu ya rape pia yaweza kutumiwa kutengeneza mafuta ya dizeli ambayo hayachafui hewa sana, hivyo yakizuia kuharibiwa kwa mazingira. Yanaposafishwa, mafuta hayo yanaweza pia kutumiwa kulainisha mashine ziwezazo kuharibika upesi, na baada ya kuziduliwa, sehemu iliyobaki ya mmea huo yaweza kupondwa-pondwa kuwa bonge ambalo lina protini nyingi na lenye mafaa likiwa chakula cha wanyama.
Ni mmea wenye matumizi mengi kama nini! Kwa hakika, twaweza kusema kama alivyosema mtunga-zaburi: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia.”—Zaburi 104:24.