Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g96 11/22 kur. 3-4
  • Kuwasiliana na Makao ya Roho

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuwasiliana na Makao ya Roho
  • Amkeni!—1996
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Milango ya Ulimwengu wa Roho
  • Ni Nani Wanaoishi Katika Makao ya Roho?
    Amkeni!—1996
  • Chifu Afikiria Wakati Wake Ujao
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1995
  • Ukweli Kuhusu Wale Wanaoishi Mbinguni
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova (Toleo la Watu wote)—2016
  • Wazazi Wetu wa Kale Wako Wapi?
    Je, Umeipata Barabara Inayoongoza Kwenye Uhai wa Milele?
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1996
g96 11/22 kur. 3-4

Kuwasiliana na Makao ya Roho

KATIKATI ya mji wa kawaida wa Afrika Magharibi pamesimama jengo linalovutia lenye orofa moja, lililopakwa rangi nyeupe na kijani. Katika chumba cha mapokezi, makarani wawili walifanya kazi katika mashine zao za kupiga taipu. Watu kadhaa waliketi vitini, wakingoja kumwona babaláwo, yule mwaguzi.

Nyuma ya dawati katika ofisi inayopakana, kando ya mashine ya faksi, alikaa babaláwo mwenyewe. Akiwa pandikizi la mtu, mwenye mvi, alivalia majoho marefu meupe—yaliyo ghali, yaliyotariziwa. “Baba yangu alikuwa mwaguzi,” akasema. “Nilipangiwa kuwa katika desturi hiyo. Nililelewa katika hiyo. Nilipofika umri wa miaka mitano, wakati baba yangu alipokwenda kuagua, nilikwenda naye. Nilitazama jinsi alivyofanya, nami nikaiga alivyofanya hadi ilipokuwa sehemu yangu muhimu.”

Huyo babaláwo alionyesha ishara kuelekea ubao mkubwa ulioorodhesha mfumo ulio tata wa kuagua ambao watu wake walikuwa wameutumia kwa vizazi visivyohesabika. Ukitegemea kurusha mbegu 16 za mawese, huo ni mfumo ambao umeenea kotekote katika Afrika Magharibi na ng’ambo ya hapo. “Watu hunijia wakiwa na matatizo ya aina zote,” akasema. “Matatizo na wanawake, utasa, ukosefu wa kazi, kurukwa kichwa, afya, na kadhalika. Ikitegemea matokeo ya uaguzi, ombi linafanywa kwa ama wazazi wa kale ama watu wa kimbingu [miungu]. Vyovyote vile, ni lazima aina fulani ya dhabihu itolewe.”

Mazoea ya kidesturi ya kidini, kutia ndani uaguzi, yamesitawi sana katika eneo hilo, lakini ndivyo ilivyo pia na makanisa ya Jumuiya ya Wakristo. Karibu tu na ofisi za babaláwo kuna majengo yaliyopakwa chokaa yenye ishara mbele yayo: Kanisa la Mfalme Sulemani 2, Kerubimu na Serafimu, Kanisa la Kimbingu la Kristo, Kanisa la Kristo la Kimitume, Kanisa la Wapiga Tarumbeta wa Kristo. Makanisa haya yapo pamoja na nyakati fulani hukubali mazoea ya dini ya kimapokeo. Akasema babaláwo: “Hivi majuzi nilikuwa nikiongea na askofu. Alikuja hapa. Baada ya kuzungumza mambo kwa dakika 30 hivi, yeye alisema kwamba alitaka tufanye mpango wa mazungumzo fulani ambamo Wakristo na wanamapokeo wanaweza kukutana na kujadiliana na kuondosha ukosefu wa uelewevu.”

Milango ya Ulimwengu wa Roho

Ukosefu huo wa uelewevu mara nyingi huhusisha utambulisho wa wale wakaao katika makao ya roho. Kotekote katika Afrika iliyo kusini ya Sahara, kuna itikadi iliyoenea sana kwamba kuna vikundi viwili vya viumbe ambao hukaa katika ulimwengu wa roho. Kikundi cha kwanza ni cha watu wa kimungu, au miungu, ambao hawajapata kuwa binadamu. Cha pili ni cha wazazi wa kale, au roho za wafu, ambao daraka lao ni kuhakikisha kusalimika na ufanisi wa familia zao duniani. Wote miungu na wazazi wa kale inaaminika kuwa wana uwezo wa ama kusaidia ama kudhuru wale walio duniani. Hivyo basi, ni lazima wote waonyeshwe staha na heshima ifaayo.

Itikadi kama hizo zapatikana katika sehemu nyingi za ulimwengu. Wakitumia njia tofauti-tofauti watu kila mahali hufikia kani za viumbe wapitao uwezo wa kibinadamu, wakitafuta ujuzi juu ya wakati ujao na msaada na mwongozo katika matatizo ya kila siku ya maisha. Je, inawezekana kweli kupata msaada kutoka kwa makao ya roho? Yesu Kristo, ambaye aliishi huko, alionyesha kwamba inawezekana. Yeye alisema hivi: “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.” (Mathayo 7:7) Lakini ili kupata msaada huo, ni lazima tumwombe mtu afaaye, tutafute katika njia ifaayo, na kubisha kwenye mlango ufaao. Ikiwa tutabisha kwenye mlango usiofaa, huenda ukafunguliwa na mtu ambaye atatudhuru, badala ya kutufaidi.

Kwa hiyo, ni jambo la muhimu sana kujua ni nani anayeishi katika makao ya roho na asiyeishi huko. Twahitaji kujua pia tofauti kati ya wale watakaotusaidia na wale watakaotudhuru. Hatimaye, twahitaji kujua tutakacholazimika kufanya ili kupata msaada kutoka kwa wale wawezao kutupatia msaada huo. Makala zifuatazo zitachunguza mambo haya.

[Credit Line katika ukurasa wa 3]

Picha kwenye kurasa 3-4: The Star, Johannesburg, S.A.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki