Kuutazama Ulimwengu
Uwe Mchangamfu—Na Ubaki Mwenye Afya!
“Kupitia ucheshi, watu huwa wastahimilivu zaidi, hukabili vizuri mafadhaiko, na hudumisha afya ya kimwili na kiakili,” ataarifu Profesa wa Chuo Kikuu cha São Paulo, Sueli Damergian. Kulingana na ripoti moja katika gazeti la habari la Brazili O Estado de S. Paulo, mtu aweza kujifunza ucheshi mzuri—kama tu vile kusoma na kuandika. Kwa wazi, hili huhitaji badiliko katika kufikiri kwa mtu aliye na kinyongo. Profesa wa saikolojia Raquel Rodrigues Kerbauy aeleza hivi: “Ikiwa mtu afikiri kwamba ataweza kutabasamu tu wakati ulimwengu utakuwa mwadilifu, atakuwa mwenye kinyongo milele. Kwa vyovyote, kuna ukosefu wa haki kila mahali.” Hata wakiwa na ratiba yenye shughuli nyingi, watu walio wachangamfu hufurahia ushirika wao wa kijamii, yataja ripoti hiyo. Wao huthamini vitu vidogo kama vile “kupiga gumzo, peremende, au dakika tano za muziki mzuri.” Hata hivyo, Damergian atahadharisha hivi: “Mtu apaswa kutambua tofauti kati ya ucheshi mzuri na upuzi na ucheshi mchafu.”
Ndege Wahatarishwa na Wapenda Ndege?
Wapenda ndege huenda wakawa wanafanya madhara badala ya mazuri kwa kuacha chakula katika bustani zao ili kiliwe na ndege, laripoti Sunday Times la London. Usumishwaji wa chakula utokanao na bakteria salmonella, vimelea, na vijiumbe-maradhi vinginevyo visivyojulikana hivi majuzi vimeua maelfu ya ndege wa Uingereza wapendwao sana ambao hupatikana bustanini. James Kirkwood, daktari mkuu wa mifugo wa Hifadhi ya Wanyama ya London, ana wasiwasi kwamba huenda spishi fulani zikatoweka kabisa katika maeneo fulani. Bakteria na vimelea hivyo visivyo kufa haraka huendelea kuishi kwa siku nyingi kwenye kinyesi cha ndege, kwenye viwekeo vya chakula cha ndege au ardhini. Kokwa zenye ukungu hasa ndizo hatari, aonya Profesa Chris Perrins, wa Chuo Kikuu cha Oxford. “Serikali yapiga marufuku kokwa zilizoambukizwa zisiuzwe kwa binadamu lakini yaziruhusu katika chakula cha ndege,” yeye ataja, akiongeza: “Hizo zaua ndege wengi sana.”
Makao Yenye Starehe kwa Ajili ya Viroboto
Hali-hewa mbaya ya kipupwe ilikuwa ikimaanisha kifo kwa idadi za viroboto. Lakini mambo yanabadilika, laripoti gazeti la Uingereza New Scientist. “Kwa mwongo ambao umepita kumekuwa na ongezeko la viroboto wa paka,” asema John Maunder, wa Cambridge Medical Entomology Centre. Nyumba za kisasa wakati huu hutumika zikiwa maskani yenye starehe ya viroboto hawa, ambao huishi pia katika mbwa. Wakati uliopita, halihewa baridi ilipunguza unyevuanga—msiba wenye kufisha kwa mabuu ya viroboto. “Sasa,” asema Maunder, “mwangahewa katika nyumba nyingi ni wa hali ya chini sana hivi kwamba unyevuanga wabaki juu, na hata halihewa baridi yenye kuendelea haiui viroboto.”
Jinsi ya Kukabiliana na Wachokozi wa Shuleni
Kufuatia kutangazwa sana kwa hivi majuzi kuhusu uchokozi katika shule, Wizara ya Elimu ya Japani ilifanya uchunguzi wa watoto 9,420 na wazazi wao na walimu. Matokeo yalifunua kwamba hadi asilimia 70 ya wazazi wa wanafunzi waliochokozwa wa shule ya msingi na shule ya sekondari ama hawajui kuhusu tatizo hilo au hawajachukua kwa uzito malalamiko ya watoto wao. Wakihofu kulipizwa kisasi, wahasiriwa wengi hawamwelezi mwalimu kwamba wanachokozwa. Hata hivyo, uchunguzi huo ulionyesha kwamba mwalimu ashughulikiapo tatizo hili kwa uzito, ni asilimia 2 tu ya wahasiriwa wanaolipizwa kisasi na uchokozi hukoma kwa asilimia 40 hivi kati ya wanafunzi wenye kuchokozwa. Profesa Yoji Morita, wa Chuo Kikuu cha Osaka City, alionelea hivi: “Nasadiki sana kuliko wakati mwingineo wote kwamba uchokozi waweza kushindwa ikiwa wahasiriwa wanaripoti kwa walimu na walimu wanashughulikia tatizo hilo ifaavyo.”
Wanachopenda na Wasichopenda Watoto
Ni nini ambacho watoto hawafurahii sana kufanya? Katika uchunguzi wa watoto wenye umri wa miaka 6 hadi 11 uliofanywa na Profesa Gustavo Pietropolli Charmet, wa Chuo Kikuu cha Milan, Italia, watoto wengi walisema: “Kukaa nyumbani ukitazama televisheni,” au “Kukaa nyumbani pamoja na mama ukifanya mgawo wa masomo ya nyumbani.” Jambo lisilopendeza kupita yote wafanyayo, lasema gazeti la habari La Repubblica, ni “kuwa na miadi,” yaani, kukimbia-kimbia sehemu tofauti-tofauti kwa ajili ya masomo ya dansi, Kiingereza, kucheza piano, na kadhalika. Pia kinachochukiwa kwa ujumla ni “mtu kuwa peke yake.” Kwa upande ule mwingine, asilimia 49 ya wavulana hutaka wazazi “waruhusu watoto wacheze nje,” huku wasichana hutaka wazazi “wacheze pamoja na watoto wao.” Kama ilivyo, wao husema: ‘Mama anapocheza nami, lazima aigize sana kwamba anacheza. Unaweza kujua ikiwa hafurahii, kisha nami sifurahii pia.’
Kadinali Alipendekeza Utendaji wa Mashahidi
Kadinali Suenens, wa Ubelgiji, mwendelezaji wa harakati za kidini za Kikatoliki, alikufa hivi majuzi akiwa na umri wa miaka 91. Gazeti la habari la Ubelgiji Het Belang van Limburg lilitaja kwamba ingawa Suenens alitimiza mambo mengi, hakutimiza lengo lake alilotamani sana maishani. Mwandamizi wake, Kadinali Danneels, alitaarifu kwamba Suenens “sikuzote alikuwa ametamani kwamba Wakristo wawe watendaji zaidi. Yeye . . . alijiuliza ikiwa twapaswa kuenda mlango hadi mlango, kama tu vile Mashahidi wa Yehova wafanyavyo. Na hatimaye, alipata kwamba hiyo kwa kulinganishwa ilikuwa njia nzuri. Taarifa iliyosikiwa mara nyingi kutoka kwake ilikuwa: ‘Unakuwa Mkristo wa kweli tu ikiwa umemfanya mtu mwingine kuwa Mkristo vilevile.’”
Kusafisha Bahari-Kuu
Hata katika siku isiyo na mvua, mamilioni ya galoni za maji machafu na takataka kutoka barabara za jiji hutiririka kuingia maji ya pwani katika eneo la Los Angeles, California. Katika siku yenye mvua, maji hayo yaweza kufika mabilioni ya lita! Mamlaka ya jiji ilidhamini programu ya kuwajulisha wakazi kwamba kila kitu kinachotupwa, kusafishwa, au kufagiliwa kuingia katika barabara huenda moja kwa moja hadi kwenye bahari-kuu kupitia mfumo wa utiririshaji maji—bila kutiwa dawa! Hii hutia ndani mafuta na vioevu vinginevyo kutoka kwenye magari, majani yaliyokatwa bustanini, takataka, na kinyesi cha wanyama rafiki. Ili kuepuka kuharibu ikolojia iliyo karibu na Santa Monica Bay, wakazi wanasihiwa: Msitupe kamwe takataka barabarani; fagieni vijia vilivyo kando ya barabara badala ya kuvipulizia maji: ondoeni kinyesi cha wanyama rafiki kisiingie barabarani; rekebisheni magari yanayovuja; na kurejesha oili ya gari. The Wall Street Journal huripoti kwamba watu wanaoogelea karibu na mfumo wa utiririshaji wa maji machafu walielekea kupatwa na homa, kutapika, maambukizo ya mfumo wa upumuaji, na kuumwa na masikio kwa asilimia 50 kuliko wale walioogelea angalau meta 360 mbali na mifumo hiyo.
Nyambizi Zenye Manyoya-Manyoya
Jeshi la Majini la Sweden ladumisha mfumo wa maikrofoni za chini ya maji ili kutambua sauti za viputo vifanyizwavyo na parapela zenye kuzunguka za nyambizi, kulingana na gazeti New Scientist. Ikichunguza ripoti 6,000 za “utendaji wa wageni chini ya maji,” kwa kutegemea mfumo wa maikrofoni na mambo yanayoonwa na umma, tume ya serikali ilipata uthibitisho wenye msingi mzuri wa utendaji wa nyambizi katika pindi sita tu. Nyingi za kengele huenda zilifanywa zilie kwa sababu ya “kupiga kafi kwenye bidii kwa miguu midogo,” yasema ripoti hiyo. Yaonekana kwamba mingi na fisimaji wenye kuogelea hutokeza mvumo unaofanana sana na ule wa parapela za nyambizi, hilo likiwakanganya wasikilizaji wa jeshi la majini.
Watoto Watenda Vibaya Watoto
Maelfu ya watoto katika Afrika Kusini hutendwa vibaya kingono na watoto wengine, laripoti gazeti la habari la Johannesburg Saturday Star. Evanthe Schurink, wa Baraza la Utafiti wa Sayansi za Binadamu, husema kwamba utendaji vibaya huu husababishwa kwa sehemu na kutendwa vibaya na kikatili kwa wakosaji hao pia. Marilyn Donaldson, mshauri wa watoto kwenye Centre for the Study of Violence and Reconciliation’s Trauma Clinic, akubali, na kusema: ‘Katika nyumba nyingi sana, watoto hawa hupatwa na jeuri yenye kuogofya ya nyumbani na mara nyingi wahasiriwa wao huwa sehemu ya familia yao iliyopanuka.’ Yeye pia hulaumu uchoshi na upuuzaji wa kimzazi kwa ajili ya utendaji mbaya mwingi. “Hakuna mtu nyumbani kwa ajili ya watoto wakati mzazi yuko kazini,” yeye aonelea, “kwa hiyo wako chini ya uwezo wa wenye kuwatenda vibaya.” Akitaja hatari nyingineyo, Donaldson alisema kwamba aona watoto wengi zaidi na zaidi “wenye umri wa miaka 6 hadi 10 wakija kwenye kitovu hicho wakiwa na Ukimwi, ambao umepitishwa kingono.”
Alkoholi Wakati wa Ujauzito
“Utafiti mpya umehakikisha mlingano kati ya utumizi wa alkoholi wa mama na hatari yenye kuongezeka ya lukemia ya vitoto,” laripoti The Medical Post, la Kanada. Uchunguzi huo ulihusisha wahasiriwa 302 wa lukemia ambao walikuwa na umri wa miezi 18 au chini ya hapo wakati ugonjwa huo ulipododoswa, pamoja na kikundi cha kufanyiwa majaribio cha watoto wengineo 558. Kwa watoto ambao mama zao walikunywa alkoholi wakati wa mwezi wa nne hadi sita na mwezi wa sita hadi tisa wa ujauzito, hatari ya kupatwa na lukemia ya myeloid ilikuwa ya juu karibu mara kumi kuliko kwa wale ambao mama zao hawakunywa. Utafiti huo mpya ulisemekana kwamba ulipatana na uchunguzi mwingine kuhusu akina mama wajawazito ambao hunywa alkoholi na hatari iliyoongezeka ya watoto wao kupatwa na lukemia.